Chilo: Safari ya Ulaya inanukia

BEKI wa kati wa Tanzania Prisons, Chilo Mkama amethibitisha kuwa katika mazungumzo na timu ya Ulinzi Stars ya nchini Kenya huku akieleza kuwa dili hilo likitiki inaweza kuwa safari yake ya kulisaka soka la kulipwa Ulaya.

Nyota huyo aliwahi kuzichezea timu kadhaa kwa mafanikio ikiwamo Toto Africans, Mbao, Polisi Tanzania na msimu uliopita alikuwa beki tegemeo kwa Wajelajela aliomaliza nao nafasi ya tisa.

Kwa sasa staa huyo asiye na masihala awapo uwanjani, mkataba wake na Prisons uliisha baada kumalizika kwa Ligi Kuu na sasa yupo huru kujiunga na timu yoyote itakayokubaliana naye.

Hata hivyo, tayari Prisons wameshaanza mazungumzo na beki huyo kisiki kwa ajili ya kuongeza mkataba mpya ili kuendelea kuitumikia timu hiyo msimu ujao na kufanya vita kuwa nzito.

Mkama aliliambia Mwanaspoti kuwa tayari yupo kwenye mazungumzo na Ulinzi Stars ya nchini Kenya, ambapo kama watakubaliana muda wowote atapaa kuanza maisha mapya.

Alisema iwapo dili hilo litatiki, huenda ikawa ni njia rasmi ya kulisaka soka la kulipwa Ulaya, akieleza kuwa uwezo na kipaji cha kucheza kabumbu anacho na hana hofu na ushindani.

“Ni kweli Ulinzi Stars wamenitafuta, mazungumzo yapo na kama tutakubaliana naweza kutimka muda wowote, Prisons nao tumezungumza hivyo nasubiri yeyote”

“Sio hao tu, zipo ofa nyingine kwa timu za Championship hivyo naangalia kwanza maisha yangu itakuaje, mpira ndio kazi yangu na sina hofu kwani uwezo ninao kucheza popote” alisema Beki huyo.

Akielezea msimu uliopita, Mkama alikiri ugumu kwa namna timu zilivyoonesha upinzani akibainisha kuwa anashukuru kwa jinsi alivyoweza kuaminiwa na makocha wote walioiongoza Prisons.

Related Posts