Dar es Salaam. Benki ya CRDB imetoa gawio la Sh51.7 bilioni kwa Serikali, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.8 ya gawio lililotolewa mwaka 2022 la Sh45.8 bilioni.
Taarifa iliyotolewa na benki hiyo Juni 21, 2024 imeleza gawio hilo limetokana na matokeo mazuri ya fedha ambayo benki imeyapata kwa mwaka 2023.
Akikabidhi gawio hilo serikalini, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dk Ally Laay amesema hilo ni sehemu ya faida ya Sh423 bilioni, baada ya kodi ambayo benki hiyo imeipata katika mwaka wa fedha 2022.
“Katika mkutano wa wanahisa uliofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) Mei mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la Sh50 kwa hisa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11 na hivyo kufanya jumla ya gawio la mwaka huu kufikia Sh130.6 bilioni, sawa na asilimia 31.8 ya faida halisi iliyopatikana,” amesema Laay.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kukua kwa thamani ya uwekezaji wa wanahisa wa benki hiyo kunatokana na mafanikio ambayo benki imeyapata katika utekelezaji wa mkakati wake wa biashara wa muda wa kati wa mwaka 2023 hadi 2027.
Nsekela amebainisha mbali na gawio lililotolewa katika mwaka wa fedha 2023, benki hiyo pia imelipa jumla ya kodi za Sh403.2 bilioni.
Hata hivyo, akizungumza katika hafla ya upokeaji wa gawio hilo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema ongezeko hilo ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa benki inazidi kuimarika kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea.
Profesa Mkumbo amesema Sh27.4 bilioni kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja na Serikali ya Denmark (DIF) zitakwenda kusaidia kuboresha zaidi sekta ya afya.
“Makubalino yetu ni kuwa fedha hizi zinaelekezwa katika kuimarisha sekta ya afya, kwa maana ya kuimarisha miundombinu na kusaidia upatikanaji wa dawa na vifaatiba,” amesema Profesa Mkumbo ambaye katika hafla hiyo alimwakilisha Waziri wa Fedha.
Aidha, Profesa Mkumbo amesema Serikali katika kipindi chake kifupi, tayari imeongeza vituo vya afya kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 9,693 mwaka 2024.
“Fedha hizi zitakwenda kusaidia jitihada hizi ikiwa ni mpango wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya,” amesema.
Akielezea namna Serikali inavyoridhishwa na umahiri wa Benki ya CRDB katika kutanua wigo wa huduma zake ndani na nje ya nchi, Profesa Mkumbo ameipongeza benki hiyo kwa kupanua wigo wake kwa kuanzisha kampuni tanzu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kampuni tanzu ya CRDB Insurance Co. Ltd, pamoja na taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo imeonyesha kuwa mstari wa mbele katika kuchochea ujumuishi wa kiuchumi kupitia programu ya IMBEJU.
Aidha, ameihakikishia benki hiyo na wadau wengine wa maendeleo nchini kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta nyinginezo, ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.
Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Usimamizi na Uchumi), Japhet Justine, ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki ya CRDB kwa kazi wanayoifanya katika kusimamia benki hiyo na kuchangia matokeo mazuri ya kifedha na kukua kwa gawio kwa wanahisa, ikiwamo Serikali.
Pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali kuu kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA, CRDB pia imekabidhi gawio kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwamo PSSSF, NSSF, ZSSF, NHIF, Local Government Loans Board, Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Umoja Unit Trust Scheme pamoja na Halmashauri za Mbinga, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe.
Hata hivyo, CRDB inatoa gawio hilo wakati ambapo Juni 11, 2024 Serikali ilipokea gawio lililowasilishwa kwenye mfuko mkuu, kiasi cha Sh637 bilioni linalojumuisha gawio la Sh279 bilioni kutoka mashirika ya biashara na Sh358 bilioni za taasisi nyingine.
Katika hafla iliyofanyikia Ikulu, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema makusanyo hayo ni kuanzia Julai 2023 hadi Mei 2024, huku kiwango kikitarajiwa kuongezeka mwishoni mwa mwaka huu wa fedha kufikia Sh850 bilioni.