Dk Nchimbi aitaka China kuwekeza katika sekta zinazoendelea

Dar es Salaam. Wakati uhusiano wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ukifikia miongo sita, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ameitaka Jamhuri ya Watu wa China kuunga mkono uwekezaji katika sekta zinazoendelea nchini.

Katika ombi lake hilo, Dk Nchimbi amehusianisha na ushirikiano wa muda mrefu wa mataifa hayo katika sekta za afya, ujenzi, utalii, kilimo, dawa, biashara na uchumi, akisema urafiki huo unapaswa kuendelea katika sekta zinazoendelea.

Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo jana Jumamosi, Juni 22, 2024 alipokutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPC, Tang Dengjie aliyewasili nchini kwa ziara ya siku tatu na kukutana na viongozi wa CCM.

Amesisitiza umuhimu wa kudumisha ushirikiano uliopo kati ya vyama hivyo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

Dk Nchimbi  amesema ni miaka 60 sasa CCM na CPC zimekuwa na urafiki na uhusiano wa kidiplomasia.

Siri ya urafiki huo, amesema ni kuendana kwa kanuni za kiitikadi, kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya vyama hivyo na kwa sasa uhusiano wa CCM na CPC umekuwa mfano wa kuigwa Afrika na duniani.

“CCM na CPC vina urafiki wa kindugu uliobadilika na kuwa msingi imara wa kukuza fursa za kiuchumi na uwekezaji, unaolenga kuimarisha ustawi wa wananchi wetu,” amesema Dk Nchimbi.

Pia, ameeleza uhusiano uliopo ulianzishwa na waasisi wa vyama hivyo na mataifa hayo yaani Mwalimu Julius Nyerere kwa Tanzania na Mao Zedong kwa China.

Katika maelezo yake, amegusia mazungumzo ya hivi karibuni ya wakuu wa nchi za Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan na China, Rais Xi Jinping yaliyoongeza hadhi ya ushirikiano na kuwa wa kimkakati.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dengjie amesema dhamira ya China ni kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kuunga mkono mipango inayowanufaisha wananchi wa pande zote.

“Miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania ni ushahidi wa urafiki wetu wa kudumu na kuheshimiana, tumejitolea kuimarisha zaidi uhusiano huu kwa manufaa ya watu wetu,” amesema.

Hata hivyo, kwa sasa China ndiyo mashirika mkuu wa biashara wa Tanzania, hali iliyodumu kwa miaka minane mfululizo.

Mwaka 2023, urari wa biashara kati ya nchi hizo ulifikia Dola 8.78 bilioni za Marekani, ikionyesha ongezeko la asilimia 5.66 kutoka mwaka uliopita.

China pia imewekeza miradi 260 katika sekta mbalimbali nchini, hivyo kuimarisha nafasi yake ya kuwa mwekezaji mkubwa wa kigeni wa Tanzania.

Ishara ya urafiki wa mataifa hayo, inajengwa pia na Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), iliyojengwa kwa msaada wa Taifa hilo.

Related Posts