Dar es Salaam. Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam zimeanzisha operesheni ya wiki mbili ya kukusanya mapato ya maegesho ya magari, baada ya kubaini wadau kukaidi kutokutii zingatio la kutoa ushuru huo.
Hata hivyo, Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), umekuja na mapendekezo matatu wakitaka maridhiano yafanyike kwanza, ikiwamo kufanyiwa kazi makosa mtambuka yanayojitokeza kwa daladala zinazofanya kazi halmashauri mbili tofauti.
Pili, wapewe elimu na wanataka uadilifu kwa watumishi na wanaobambikia makosa watu waondolewe, huku wakieleza hawapingi kulipa kodi hiyo ila ni muhimu mambo hayo yakaanza kufanyiwa kazi kabla ya kuendelea na mchakato huo kwani ilivyo sasa wanaumia.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Juni 23, 2024 Ofisa Ukaguzi Ofisi ya Rais ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Falesy Kibassa amesema kutokutekeleza sheria hiyo ya Serikali za mitaa namba 288 ya mwaka 2021, kumeendelea kuzigharimu halmashauri hizo kwa kuwa na madeni kiasi cha kutokufikia malengo.
Akitaja mgawanyo wa madeni hayo, kwa mkoa wa Dar es Salaam amesema Ilala inadaiwa Sh7.5 bilioni, Kinondoni Sh2.9 bilioni, Temeke Sh1.5 bilioni, Ubungo Sh6.4 milioni na Kigamboni Sh371.4 milioni.
Amesema operesheni ya urejeshaji fedha hizo ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri za majiji, miji na wilaya hadi kufikia Juni 30 mwaka huu vyanzo vyote vya mapato vifikie asilimia 100.
Vilevile, madeni yote ya nyuma yakusanywe ili kujibu hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuwa halmashauri hazikusanyi mapato na eneo kinara lenye udhaifu ni maegesho ya magari.
Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa (Darcoboa), Shifwanya Lema amesema hawana shida katika ulipaji wa ushuru huo isipokuwa kila mtu afanye majukumu kwa wakati wake huku wakieleza si vyema kusababisha foleni kwa sababu ya kukusanya kodi barabarani.
“Daladala tunalipa ushuru wa Sh2,000 kwa siku, sasa unakuta wakati mwingine tunaandikiwa ushuru wa wa gari Sh1.1milioni, sasa tunashangaa na tunashindwa kuelewa zinatoka wapi,” amehoji.
Amesema kwa kuwa jambo hilo lipo ndani ya mkoa huo ni muhimu likatazamwa upya kuona ni halmashauri pamoja na Jiji na Mkuu wa mkoa kulitazama kwa pamoja na kuja na suluhisho.
“Unakuta mtu anafanya kazi Kigamboni lakini faini anaandikiwa Ubungo au Ilala wakati haijawai kufika maeneo hayo hata siku moja tufanye marejeo. Tunataka wanaofanya makosa hayo wawajibishwe.
Unakuta mtu amepiga picha gari ndogo lakini inasoma gari ya daladala inaleta kero muda wote inasimamishwa, wakati kosa limefanywa na mtu aliyepewa dhamana ya kusimamia,” amesema.
Amesema kwa daladala zinazofanya kazi halmashauri mbili tofauti ni muhumu maridhiano yafanyike zikubaliane kila upande uchukue Sh1,000 ili kuepusha usumbufu kwa wamiliki wa daladala.
Vilevile, wadau hao wamesema jambo lingine wanapaswa kupewa elimu ya mara kwa mara mathalani walikuwa hawajui kama gari ikiwa gereji inapaswa kulipiwa ushuru.
“Wakati mwingine inatokea vurugu kwa jambo ambalo tulitakiwa kupewa elimu watu waweze kuelewa kwamba nikipaki hapa natakiwa kutoa ushuru wa jiji,” amesema.
Akijibu hoja za wadau wa daladala, Kibassa amesema ushuru wa maegesho hauhusiani kabisa na ule wa vituo vya daladala zao, kwa kuwa umejikita kama mtu amepaki kwenda kula, gereji au sehemu nyingine.
“Sisi hatuingilii ruti zao wala kwenye vituo vyao vya daladala isipokuwa kama gari umepaki sehemu tutakulipisha kulingana na muda uliokaa, kama umeenda kula, gereji na gharama hizo zinategemeana na halmashauri na halmashauri,” amesema
Amesema mathalani kama Dar es Salaam wanatoza Sh500 kwa saa moja lakini Iringa inaweza kuwa Sh1,000 kwa muda huo huku akieleza halmashauri zingine zinaweza zikatoza zaidi ya hapo.
“Mfumo wa kulipia ni rahisi na unamuwezesha mteja kulipa na kujua kiasi cha deni analodaiwa, unaweza kulipia kupitia mfumo wa (GePG) au mfumo wa Tamisemi,” amesema.
Amesema hakuna mtu anayebambikiwa bili na kama ikijitokeza mhusika anapaswa kwenda kwenye halmashauri aliyoandikiwa na hakwenda kufanya marejeo ya picha iliyochukuliwa kuangalia uhalali.
“Mifumo hiyo inaonesha kama ni kweli alikwenda au hakwenda na changamoto yake kutatuliwa. Lakini mtu hawezi kubambikiwa ushuru,” amesema.
Wakati wadau hao wakieleza hayo, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekiri kufanyia kazi upungufu yaliyopo, huku ikitoa siku tano kuhakikisha wale wote wanaodaiwa fedha za maegesho wanalipa.
“Nachukua nafasi hii kusisitiza wale wote wenye madeni ya fedha za maegesho, wahakikishe katika kipindi cha siku tano, hizo fedha wawe wamelipa,” amesema Mkuu wa Wilaya hiyo Saad Mtambule.
Amesema ili kuhakikisha wadaiwa wanalipa fedha hizo tayari wameshapeleka vikosi kazi ikiwamo Tegeta, ili wasimamishe magari wakague kama walishalipa tozo za maegesho.
“Gari za abiria kwa maana zile za daladala tumeweka utaratibu maalumu badala ya kuzisimamisha barabarani zikiwa na abiria wakifika kwenye vituo kama Makumbusho na Mwenge watakaguliwa na walipe kwa utaratibu uliopo,” amesema
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wote wanaodaiwa kutoa ushirikiano kwa maofisa wakusanya ushuru huo, lakini watatoa matangazo mahususi ya namna wanavyotakiwa kulipa kupitia mitandao.
“Kipindi hiki cha wiki mbili wadau watoe ushirikiano deni tunalodaiwa ni kubwa la Sh7.5 bilioni na wasilete migomo na watumishi wasiwanyanyase wanaotakiwa kutoa ushuru,” amesema.
Amesema fedha hizo zinahitaji ili kujenga miundombinu mbalimbali ya kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo barabara na kuwaletea maendeleo.