Huko City kumekucha, wenye vipaji waitwa

SIKU chache baada ya kufunguliwa dirisha la usajili, Mbeya City imewaita vijana na wachezaji wenye kipaji na nia ya kitumikia timu hiyo kujitokeza kwenye majaribio ‘trial’ kwa ajili ya msimu ujao.

Mbeya City iliyoshuka daraja msimu wa 2022/23 kupitia play off ilipofungwa kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya Mashujaa, inajiandaa na Championship msimu ujao baada ya kushindwa kurejea Ligi Kuu.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Newton Mwatijobe alisema kuwa majaribio yanatarajia kuanza mapema mwezi Julai badala ya Juni kama ilivyokuwa imepangwa kutokana changamoto zilizojitokeza.

Alisema tayari wameanza usajili japokuwa hawajaanza kutangaza walioingia na kwamba majaribio hayo yatawasaidia kupata vijana wenye uwezo kwa ajili ya msimu ujao.

“Usajili tumeanza japokuwa bado kuwatangaza, tunasubiri na majaribio ili kupata kikosi bora kama tulivyowahi kufanya msimu wa 2013/14 wakati tunapanda Ligi Kuu” alisema Mwatijobe.

Kuhusu benchi la ufundi, Mwenyekiti huyo hakuweza kufafanua hatma ya kocha Mkuu, Salum Mayanga na wenzake huku habari za ndani zikidokeza kuwa watafumua kila kitu.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa matarajio yao ni kuona City yenye ubora na ushindani kuhakikisha wanapoanza msimu wanafanya vizuri na kurejea Ligi Kuu.

“Suala la kocha tunaendelea kulifanyia kazi, lakini niwatoe hofu mashabiki kuwa City itarudi Ligi Kuu kwa kishindo kutokana na mipango tunayoiweka, kimsingi tunaomba ushirikiano” alisema.

Related Posts