Idadi ya wanaojua kusoma yaongezeka Tanzania

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amebainisha maeneo manne yaliyoonyesha matokeo chanya katika ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ikiwemo ongezeko la idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika kufikia asilimia 83.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka asilimia 78 ya mwaka 2012 kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya sensa ya mwaka 2022 ikiangazia vijana kuanzia miaka 15 na kuendelea.

Majaliwa amebainisha hayo jana Jumamosi Juni 22, 2024 wakati akizundua Ripoti za Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na Mazingira zilizotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 chapisho namba nne pamoja na ripoti ya kina iliyotokana na taarifa zilizokusanywa katika Sensa ya Majengo Nchini mwaka 2022.

Waziri Mkuu amesema matarajio ya Serikali ni kuona mipango yake katika ngazi zote za utawala, ikiwemo ya kibajeti inazingatia uhalisia unaotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022.

Maeneo mengine yaliyoonyesha matokeo chanya ni matumizi ya nishati safi ambapo hadi  2022, kaya asilimia 4.3 zilikuwa zinatumia umeme tofauti na mwaka 2012 kulikokuwa na asilimia 1.6 waliokuwa wanatumia nishati hiyo.

Hata hivyo, kwa upande wa kaya zinazotumia kuni zimepungua kutoka asilimia 68.5 ya mwaka 2012 hadi asilimia 55.5 ya mwaka 2022, huku nishati ya gesi matumizi yakipanda kutoka asilimia 0.9 hadi kufikia asilimia 9.4 kwa kipindi cha 2022.

Kwa upande wa maji, asilimia 70.1 ya kaya zinatumia maji kutoka vyanzo vilivyoboreshwa, huku asilimia 60.2 ya Watanzania wakitumia vyoo vilivyoboreshwa.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema takwimu za sensa ziliwezesha Serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti katika kubainisha kiwango cha madhara yaliyotokana na majanga ya maporomoko ya udongo yaliyotokea katika wilaya ya Hanang, mkoa wa Manyara na mafuriko katika wiilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani.

“Taarifa ziliwezesha kuandaa mikakati ya kuwafariji wananchi walioathirika? mafanikio hayo yote yametokana na uwepo wa matokeo ya takwimu za Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambazo zimeunganishwa na takwimu za Sensa ya majengo na anwani za makazi”amesema.

Akizungumzia takwimu za majengo nchini, Majaliwa amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo Tanzania ina majengo milioni 14.3. kati ya hayo, majengo milioni 13.9 yapo Tanzania bara na takribani majengo laki nne yapo Zanzibar.

“Asilimia   94.4 ya majengo yote siyo ya ghorofa, isitoshe, majengo tisa kati ya kumi ni kwa ajili ya makazi na asilimia 3.4 ya majengo ni ya makazi na biashara,”amesema Majaliwa.

Ili kuwa na matunda juu ya matumizi ya takwimu za sensa, Majaliwa amewaagiza watendaji wote wanaohusika na sera na mipango katika Serikali kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wahakikishe kuwa mipango na maamuzi yote yanayohusu maendeleo, ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi yanazingatia matokeo hayo ya sensa.

“Pia Serikali ingependa kuona matokeo ya sensa yanatumika kikamilifu katika kubaini na kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu kwa namna ambayo ni endelevu, matumizi ya matokeo haya ni ya kila Mtanzania kwa kuwa ni mali ya umma, hivyo mkakati wa uelimishaji umma katika maeneo mbalimbali uendelezwe,” amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Makamu wapili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hemed  Suleiman Abdullah amesema uwepo wa takwimu hizo ni jambo moja na matumizi yake na tafsiri ni jambo lingine, hivyo ni muhimu kutumia takwimu hizo kwa uweledi mkubwa.

“Hatuna sababu za kukosea kupanga,uchambuzi wa takwimu unakwenda kujibu maswali ya eneo lolote la Tanzania, kila eneo linajulikana lina huduma gani, takwimu zitatusaidia kuonyesha maslahi ya wananchi na kusaidia Serikali juu ya upotevu wa vitu mbalimbali,” amesema.

Kuhusu ripoti hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, amesema takwimu zilizopatikana zitaisaidia Serikali kupanga mipango ya nchi.

“Kodi ya majengo Serikali itakusanya bila kuwasumbua watu kwa sababu kanzidata ya majengo nchini imekamilika,” amesema.

Related Posts