Matumizi makubwa ya mbolea, viuatilifu tishio jipya Tanzania

Arusha. Matumizi makubwa ya mbolea za kisasa na viuatilifu yametajwa kutishia usalama na uhakika wa chakula nchini Tanzania.

 Inaelezwa hali hiyo inasababishwa na kuibuka kwa wadudu waharibifu, magonjwa mapya ya mimea na viumbe vamizi.

Watafiti wa Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA) wameiomba Serikali na wadau wa kilimo kuunganisha nguvu kukabiliana na changamoto hiyo. Hiyo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za asili na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na hali hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya TPHPA, Profesa Andrew Temu amesema hayo leo Jumapili Juni 23, 2024 katika mkutano mkuu wa wadau wa afya ya mimea na viuatilifu unaofanyika jijini Arusha.

Amesema matumizi makubwa ya mbolea za kisasa na viuatilifu yamesababisha kuibuka kwa wadudu waharibifu na magonjwa mapya ya mimea na mazao.

Profesa Temu amesema pia viumbe vamizi vimekuwa vikiingilia mifumo ya ekolojia ya asili na kushindana na viumbe vingine, jambo linalotishia ustawi wa mimea na mazao.

Profesa huyo ametaja changamoto nyingine ni usugu wa visumbufu dhidi ya viuatilifu na ukosefu wa mbadala wa viuatilifu vilivyopigwa marufuku baada ya kutumika kwa muda mrefu. Hivyo, ametoa shime kwa wadau kuchangamka na kufanya utafiti katika kusaka mbadala wa viuatilifu hivyo sambamba na kutafuta njia za kuangamiza visumbufu vipya vinavyoibuka kila siku.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Profesa Temu amesema wanatoa elimu kwa wadau, hususan wakulima kuhusu madhara ya matumizi makubwa ya mbolea za kisasa na viuatilifu.

Pia wanahamasisha uhifadhi wa bioanuai na kushirikiana na taasisi za kitafiti nchini na mashirika ya kimataifa ya kilimo na chakula.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema lengo la mkutano huo ni kuwajulisha wadau kuhusu kazi za mamlaka, sheria na taratibu zake ili kupunguza ukiukwaji wa sheria, hasa uuzaji na ununuzi wa viuatilifu feki.

Amesema tayari wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima ya udhibiti wa visumbufu mimea, wakiwemo wadudu kama kantangaze, ndege aina ya kweleakwelea, panya, na magonjwa kama mnyauko.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuella Kaganda akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amewataka wadau hao kuwasilisha mapendekezo yao kwa Serikali kuhusu nini kifanyike kukabiliana na changamoto hizo.

Amesisisitiza kuwa mahitaji ya chakula ifikapo mwaka 2030 yatakuwa tani milioni 20 kutoka tani milioni 16 za sasa, hivyo changamoto yoyote kwa sekta ya kilimo ni hatari kwa nchi.

Related Posts