Mfahamu Askofu Pisa, Rais mpya wa TEC

Dar es Salaam. Kanisa Katoliki Tanzania kupitia Baraza la Maaskofu (TEC) limetangaza viongozi wake wapya, huku nafasi ya urais ikichukuliwa na Askofu Wolfgang Pisa wa Jimbo la Lindi.

Viongozi  hao waliotangazwa jana Jumamosi Juni 22, 2024, mbali na Askofu Pisa, wengine waliochaguliwa ni Makamu wa Rais, Askofu Eusebius Nzigilwa (Jimbo Katoliki Mpanda), Katibu Mkuu, Padri Dk Charles Kitima na Naibu Katibu Mkuu, Padri Chesco Msaga wa Jimbo Katoliki la Singida kuwa Naibu Katibu Mkuu wa baraza hilo.

Uchaguzi wa kuwaingiza madarakani viongozi hao ulifanyika Ijumaa Juni 21, 2024 kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tatu  usiku jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa tovuti ya Vatcan, Aprili 9, 2022 Askofu Pisa aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi akichukua nafasi ya Askofu mstaafu, Bruno Pius Ngonyani.

Tovuti hiyo imeandika kuwa Askofu Pisa alizaliwa Julai 6, 1965 wilayani Mbulu mkoani Manyara. Baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 1989 alijiunga na shirika la ndugu wadogo wakapuchini (OFM Cap) kwa mafunzo ya upadri.

Aidha, alitumwa seminari ya Mtakatifu Agustino huko Kabwe, Zambia na mwaka 1992 alitunukiwa shahada ya Falsafa (Bachelor Degree in Philosophy).

Baada ya hapo, alijiunga na seminari kuu ya Mtakatifu Dominic, Woodland Lusaka nchini Zambia kwa mafunzo ya biblia.

Tovuti ya Vatcan inasema mwaka 1996 alitunukiwa shahada ya elimu ya biblia (Bachelor degree in Divinity). Baadaye alijiunga na chuo kikuu kishiriki cha Jordan na kutunukiwa Shahada ya utaalimungu (Bachelor degree in Theology).

“Septemba 1, 1999 alipewa daraja takatifu la upadri kisha alipangiwa kuwa mlezi wa wanafunzi katika  Seminari ndogo ya Maua mkoani Kilimanjaro.

Mwaka 2000 alitumwa masomoni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwaka 2002 alitunukiwa Shahada ya Uzamili (Masters of Education – Applied Social Psychology).

Baada ya kuhitimu nafasi hiyo, alirudi seminari ndogo ya maua kama mwalimu na mwaka 2005 aliteuliwa kuwa Gombera wa seminari hiyo.

Mwaka 2008 alitumwa na kanisa kwenda masomoni, Catholic University of America (Washington) na mwaka 2011 alitunukiwa shahada ya uzamili ya maadili (Masters in Social Ethics).

Aliporejea alichaguliwa Mkuu wa Shirika la Wakapuchini Tanzania na kuongoza hadi mwaka 2016, kabla ya kutumwa tena Chuo cha Catholic University of America kusomea shahada ya uzamivu katika maadili (PhD in Social Ethics).

Amewahi kufanya shughuli zake za kichungaji Parokiani Kibaigwa, Jimbo Kuu la Dodoma kati ya mwaka 2019-2020, pia aliwahi kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kwangulelo Jimbo Kuu la Arusha na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (Saut) Tawi la Arusha.

Pisa anaingia katika wadhifa huo akipokea kijiti kutoka kwa Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga ambaye amemaliza muda wake wa miaka sita (vipindi viwili vya miaka mitatu) kama Rais wa TEC, akisaidiwa na Makamu wa Rais Askofu Flavian Kassala na Katibu Mkuu Padri Dk Charles Kitima ambaye amechaguliwa tena katika nafasi hiyo.

Waliowahi kuwa marais TEC

Kwa mujibu wa ukurasa wa Instagram wa Redio Maria Tanzania, ifuatayo ni orodha ya waliowahi kuwa Marais wa TEC;

1. 1969-1970: Askofu Placidus Gervasius Nkalanga, Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba.

2. 1970-1976: Askofu James Dominic Sangu, Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya.

3. 1976-1982: Askofu Mario Epifanio Abdallah Mgulunde, Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa.

4. 1982-1988: Askofu Anthony Mayala, Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma (na Baadaye aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza)

5. 1988-1994: Askofu Josephat Louis Lebulu, (Wakati Huo akiwa Askofu wa Jimbo la Same kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha na sasa ni Askofu Mkuu Mstaafu)

6. 1994-2000: Askofu Justin Tetemu Samba, Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma.

7. 2000-2006: Askofu Severine Niwemugizi, Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara.

8. 2006-2013: Askofu Mkuu Juda Thadaeus Ruwa’ichi, Mwanza na sasa ni Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es salaam.

9. 2013-2018: Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa.

10. 2018 – 2024: Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya.

11. 2024- Askofu Wolfgang Pisa, Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi

Related Posts