Mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo kung’oa vigogo TRA

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikipambana kuzima tishio la mgomo wa wafanyabiashara kwenye Soko la Kimataifa la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, taarifa zinadai sakata hilo linaweza kugharimu nafasi za baadhi ya watendaji ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Habari za ndani kutoka chanzo chetu zinadai, licha ya maelekezo ya mara kwa mara yanayotolewa na viongozi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kufuatwa kwa utaratibu wa kutoza na kudai kodi, bado wapo baadhi ya watumishi ndani ya mamlaka hiyo wanaokwenda kinyume na maelekezo hayo.

Miongoni mwa malalamiko ya wafanyabiashara hao ni kurudishwa kimyakimya kwa kikosi kazi cha kudai kodi ambacho kimetajwa kuwabughudhi. Jambo hili pia lilizungumzwa na baadhi ya wabunge walipokuwa wakichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali bungeni jijini Dodoma.

Hata hivyo, inaelezwa huenda hayo si maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa watendaji wa juu ndani ya mamlaka hiyo inayoongozwa na Kamishna Mkuu, Alphayo Kidata, lakini kwa kuwa ni jambo lililokemewa mara kadhaa na viongozi wakuu wa nchi, akiwemo Rais Samia halikupaswa kuachwa lifanyike.

“Kwa sasa Serikali imechukua hatua mbalimbali kutuliza hali ya hewa. Ni kweli kuna wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia vitendo vinavyokwenda kinyume katika kudai kodi. Wanaona ni kama manyanyaso na kubambikiwa kodi kubwa ama kulipishwa kodi mara mbili kinyume cha taratibu.

“Wapo wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kujaribu kukwepa kodi. Hata kwenye hili kundi linalotaka kufanya mgomo, wapo wafanyabiashara wakubwa wenye nia ovu ya kukwepa kodi,” kimeeleza chanzo chetu na kuongeza;

“Sasa kwa hali ilivyo, kuna shughuli inakuja na huenda ikawakumba baadhi ya vigogo na wakapoteza nafasi.”

Mwananchi Digital inafahamu kutokana na mvutano wa mara kwa mara kati ya TRA na wafanyabiashara, panga pangua inatarajiwa kufanyika muda wowote kuanzia sasa, ili kupata sura mpya za watumishi ndani ya mamlaka hiyo watakaorejesha imani kwa wafanyabiashara.

Mei 15, 2023, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wafanyabiashara waliokuwa kwenye mgomo kupinga kero mbalimbali walizodai zinatokana na TRA, alisema hakuna mtumishi wa umma mwenye mamlaka ya kudharau maagizo yanayotolewa na viongozi wake.

Baadhi ya kero za kipindi kile ambazo ndizo zanalalamikiwa na sasa ni kamatakamata ya TRA dhidi ya wafanyabiashara, wateja kutoka nchi jirani na ulazima wa kusajili maghala yanayohifadhi bidhaa.

Taarifa za mgomo huo zilianza kusambaa jana Jumamosi, Juni 22, 2024 kwa vipeperushi vikieleza uwepo kwa mgomo kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kuanzia kesho Jumatatu Juni 24, huku maeneo mengine kama Mbeya, Iringa, Mwanza, Arusha, Ruvuma, Kagera na Rukwa wakitakiwa kuanza mgomo Jumanne ya Juni 25.

Aidha, Juni 26, 2024 kipeperushi hicho ambacho hakijajulikana kimetolewa na nani kinaeleza itakuwa mgomo kwa wafanyabiashara nchi nzima.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabisahara Tanzania (JWT), Hamis Livembe amesema leo Jumapili Juni 24, 2024 kuwa mgomo huo hauna baraka za viongozi, kwa kuwa hata alipowasiliana na wasimamizi wa wafanyabiashara sokoni hapo hawakuwa na taarifa.

“Mgomo hauna baraka za viongozi, sisi pia tumesikia uwepo wake kama ninyi mlivyosikia, tumeona katika mitandao ya kijamii vipeperushi na katika baadhi ya makundi yetu mitandaoni, lakini tulipojaribu kuwasiliana na viongozi wa wafanyabiashara mikoa, wilaya na hapo Kariakoo nao walikuwa hawajui,” amesema Livembe.

Kutokana na taarifa hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekutana na waandishi wa habari leo na kueleza tayari baadhi ya changamoto za wafanyabiashara katika soko hilo zimeanza kufanyiwa kazi na Wizara ya Fedha, Viwanda na Biashara, halmashauli za jiji hilo na sekta nyingine muhimu zilizokuwa zinalalamikiwa.

“Yawezekana wafanyabiashara wana malalamiko ya dhati kabisa kuhusu biashara zao,” amesema Chalamila na kusisitiza wamekuwa wakikaa mara kwa mara kujadili na kuzungumzia changamoto zao.

Wakati hayo yakiendelea, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime limewahakikishia ulinzi wafanyabiashara wa soko hilo watakaotaka kuendelea na shughuli zao pamoja na wanunuzi watakaofika sokoni, huku likiwatafuta waliosambaza tangazo hilo.

Wakati wengine wakieleza hawa taarifa, baadhi ya wafanyabiashara wamesema wana taarifa za mgomo huo na Lameck Mbilinyi, anayefanya biashara ya vyombo sokoni hapo anamethibitisha hilo.

Amesema vipeperushi vya mgomo huo vimepitishwa, isipokuwa sababu haijawekwa wazi, huku akiwashari wateja kufika sokoni kuanzia saa nne asubuhi pengine hali itakuwa shwari.

“Jana kila duka lilikuwa linapewa karatasi la tangazo la mgomo kwa sababu watu wanalia kamatakamata imerudi, faini ya wasiotoa risiti imeongezeka, hivyo sisi tutafika ofisini kama kawaida, ila tutakuwa tunasikilizia kile ambacho kitasemwa na wenzetu,” amesema.

Hata Lilian Kimaro naye amesema ana taarifa za mgomo, akisisitiza wanafanya hivyo kushinikiza kurahisishwa kwa mazingira ya ufanyaji biashara.

“Wanaosema hawajui ni waongo na wanaogopa kusema ukweli, taarifa zipo kila sehemu,” amesema Lilian.

Alipoulizwa kuhusu viongozi wao kwenda jijini Dodoma katika vikao na viongozi wa Serikali, ili kutafuta suluhisho, amesema hayupo na wafanyabiashara kwa sasa, akituhumu kwa kile alichokiita ‘uchawa.’

“Hakuna anachosaidia kwa sasa zaidi ya kuwa chawa kwa viongozi wakati sisi huku tunahangaika na hali ngumu ya biashara,” amesema na kuongeza; “Si kugoma tu hadi kuandamana.”

Chanzo kingine cha kugoma kwao ni kile kilichoelezwa na Lauren Massawe, anayefanya biashara ya vitenge sokoni hapo kuwa kumekuwa na kukamatwa kwa madai ya kutotoa risiti, hivyo wanagoma kufikisha malalamiko yao.

Hata hivyo, ameeleza kugoma huko pia kunalenga kushinikiza kupata mrejesho wa malalamiko yao ya mwaka jana.

“Kumekuwa na ukamataji kwa wateja kupitia TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na malalamiko yetu ya mwaka jana hayajafanyiwa kazi kwa sababu hatujapata mrejesho hadi leo na hatujui maamuzi yaliyotolewa ni yapi,” amesema.

Mwinyimkuu Yusuph, ni mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, amesema hakusikia taarifa yoyote kuhusu mgomo wa wafanyabiashara sokoni hapo.

“Kungekuwa na huo mgomo mwenyekiti angeshatuambia nini tunapaswa kufanya hiyo kesho, ila hadi sasa hakuna kitu,” amesema.

Kama ilivyo kwa Mwinyimkuu, Zaida Athuman naye amesema hana taarifa rasmi kuhusu mgomo huo, zaidi ya kuona kipeperushi hicho mitandaoni.

Kwa sababu hiyo, amesema amebaki kusikiliza na atatekeleza kile kitakachoamriwa kesho.

Baraka Manyanya, naye ni miongoni mwa wale wale wasio na taarifa, lakini amesema malalamiko ya kukamatwa mara kwa mara na watu wanaodai ni kutoka TRA, ingawa hawana utambulisho wowote.

Related Posts