KILA mwanadamu huzaliwa mara moja, huishi mara moja na kufariki mara moja. Iko hivyo. Ila katika kila eneo kuna mwanadamu wa kipekee.
Leo nimzungumzie John Bocco ‘Adebayor’. Straika halisi wa mpira. Straika Bora wa muda wote wa Ligi yetu.
Nyakati zimekwenda wapi? Majuzi Simba imetangaza kuwa Bocco hatakuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao. Inasikitisha sana.
Habari mbaya zaidi ni kwamba huenda tusimuone tena Bocco uwanjani kama mchezaji. Kwa sasa amegeukia ukocha. Amepewa timu ya Vijana ya Simba U17.
Baada ya miaka 16 ya mapambano na kufunga mabao ya kusisimua, Bocco anatundika daluga rasmi.
Hajaonekana uwanjani tangu Desemba mwaka jana alipoamua kwenda kusomea ukocha. Baada ya mabao 154 katika Ligi Kuu, Bocco amekubali yaishe.
Huyu ndiye Mfungaji Bora wa muda wote wa Bara. Amevunja rekodi iliyodumu muda mrefu ya Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ya mabao 153 katika Ligi. Ndiye fundi Bocco.
Ni nadra sana katika soka letu kupata mchezaji mzawa anayecheza kwa ubora ule ule kwa miaka zaidi ya 10. Wengi huwa wanalewa sifa na kupotea mapema.
Wako wapi kina Jerry Tegete, Hussein Javu, Elius Maguli, Said Bahanuzi na wengineo? Walipotea mapema lakini Bocco akaendelea kuwepo.
Alifanya makubwa akiwa na Azam FC. Akafanya makubwa zaidi akiwa na Simba. Nani anajutia kumtazama Bocco katika ubora wake?
Alikuwa na nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja. Hii ndio sababu Azam ilimpenda kwa wakati wote na sasa Simba ikampenda zaidi.
Ni vigumu kukutana na mchezaji mwenye haiba ya Bocco. Kiongozi wa wachezaji wenzake uwanjani. Mchezaji mwenye juhudi kwa dakika zote. Hana skendo yoyote ya nje ya uwanja. Ni nadra sana.
Tumezoea kuona wachezaji wengi wa nafasi za ulinzi na kiungo wakicheza kwa ubora wa juu kwa miaka mingi, lakini Bocco ametuonyesha hata washambuliaji wanaweza kufanya hivyo. Amesumbua kwa misimu 16 mfululizo tangu alipoipandisha Azam daraja pale Dodoma 2007.
Bahati mbaya ni kwamba Bocco anastaafu wakati ambao hakuna mbadala wake. Nani atavaa viatu vyake? Sijaona.
Waziri Junior amekua na vipindi vya kupwa na kujaa. Ameshindwa kufanya vizuri kwenye timu kubwa mara mbili. Alishindwa Yanga na kisha Azam FC. Ataweza kuvaa viatu vya Bocco? Hapana!
Vipi kuhusu Clement Mzize. Ni mchezaji mzuri. Ana juhudi kubwa. Ana kasi nzuri. Ila shabaha yake katika kufunga sio nzuri. Ndio sababu namba zake Ligi Kuu hazijawahi kuvutia sana.
Bado Mzize ana safari ndefu kufikia ubora wa Bocco. Ana kazi kubwa ya kufanya katika umaliziaji wake.
Bocco kwenye msimu wa pili tu katika Ligi alifunga magoli 14. Miaka miwili baadaye akawa mfungaji Bora. Akifunga 19. Mzize ataweza?
Ukweli ni kwamba tushukuru kwa kuwa na straika aina ya Bocco katika kizazi chetu. Tunashukuru kwa ubora wake wa kuzifumania nyavu.