Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara kuepuka kushiriki kwenye masuala yanayoweza kuleta uvunjifu wa amani na kurudisha nyuma uchumi ikiwemo uvumi wa mgomo unaodaiwa kuanza kesho Jumatatu. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Amesema Serikali imekwishashughulikia baadhi ya changamoto na inaendelea kushughulikia changamoto za wafanyabiashara hususani zile zinazohusu mabadiliko ya kisheria.
Chalamila ameyasema hayo mapema leo tarehe 23 Juni 2024 jijini Dar esSalaam kutokana na uwepo wa taarifa za uvumi wa mgomo wa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo na mikoa mingine.
Chalamila amewataka wafanyabiashara kutambua kuwa mgomo sio suluhisho pekee la kutatua changamoto bali utaratibu bora wa kutatua changamoto ni kukaa mezani na mamlaka kujadili kwani mgomo huongeza chuki na wakati mwingine kusababisha uvunjifu wa amani
Aidha, Chalamila amesema kuwa Serikali inatambua changamoto za wafanyabiashara na kada zingine za wafanyakazi na watumishi na inaendelea kuzifanyia kazi.
Amewataka wafanyabiashara kushirikiana na Serikali kumaliza changamoto zao na kuepuka mihemko inayoanzishwa na watu wachache wasio kuwa na nia njema na Mkoa wa Dar es salaam na Taifa kwa ujumla.
Sanjari na hilo Chalamila amesema ujenzi wa soko jipya la Kariakoo na ukarabati wa soko liloloungua kuwa soko hilo linalojengwa kwa zaidi ya Sh 28 bilioni lpo katika hatua za mwisho na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa soko hilo.
“Wfanyabiashara waliokuwepo zamani na wapya wataingia kwa utaratibu maalum utakaotolewa na uongozi wa soko hilo,” amesema.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam amezungumzia oparesheini ya kuwaondoa wafanyabiashara za ngono (Dada Poa) inayofanyika Wilayani Ubungo na kusema kuwa mila, desturi na tamaduni za Tanzania hazikubaliani na biashara hiyo ya ngono pamoja na ndoa za jinsia moja hivyo Serikali mkoani humo itaendelea kupinga vitendo.