Rufaa yamnasua hukumu ya kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama ya Rufani imemwachia huru mkazi wa Kahama, Richard Jacobo aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua dereva teksi, Patrick James.

Jacobo na mwenzake Raphael Pius walihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Juni 29, 2021.

Walidaiwa wakiwa kama abiria kwenye taksi hiyo waliyoikodi, walimuua Patrick na kutelekeza mwili wake, kisha kwenda kuliuza gari lake.

Jopo la majaji wa tatu wakiongozwa na Jaji Shabani Lila, Ignas Kitusi na Lilian Mashaka waliosikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 377/2021, walitoa uamuzi huo Juni 21, 2024 katika vikao vyake vilivyoketi Iringa.

Majaji hao walifikia uamuzi huo wa kumuachia huru mrufani huyo wa pili baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa dhidi yake kutothibitisha kosa dhidi yake.

Aidha, majaji hao walisema wameridhika kwamba kesi dhidi ya mrufani wa kwanza ilithibitishwa bila shaka yoyote, hivyo rufaa ya mrufani wa kwanza kutupiliwa mbali.

Warufani wawili waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji, ilidaiwa kuwa Septemba 13, 2016 katika Mji wa Mafinga, wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa, dereva teksi alikufa kifo kisicho cha kawaida na mwili wake ulipatikana siku chache baadaye.

Ilidaiwa warufani walikuwa abiria wa mwisho katika gari la marehemu na walionekana nalo alipokuwa hai.

Ilidaiwa gari hilo lilikuwa na namba za usajili T 351 CWA, Toyota Carina baada ya upelelezi lilikutwa Kahama mkoani Shinyanga na aliyekutwa nalo aliwataja warufani hao ndiyo walimuuzia.

Kwa mujibu wa shahidi wa nne wa Jamhuri ambaye ni kaka wa marehemu, Simon James alidai mahakamani hapo kuwa alisambaza kwenye mitandao ya kijamii picha ya gari hilo kuomba yeyote kama ameliona atoe taarifa.

Alidai mmoja wa wafanyabiashara na mkazi wa Mafinga aliyekuwa akisafiri kutoka Mafinga kuelekea Mwanza kupitia Kahama, aliliona gari hilo limeegeshwa Kituo cha Polisi Kahama.

Alidai alichukua hatua ya kumpigia simu shemeji wa marehemu aliyetangaza kwenye mitandao kumjulisha.

Shemeji yake huyo alifunga safari hadi Kahama akiambatana na askari wakafanikiwa kumkamata Samwel Ntumami ambaye ni shahidi wa nane.

Ntumai alipohojiwa alidai gari hilo aliuziwa na watu wawili aliodai walikuwa wanafahamiana na mrufani wa pili aliyekuwa akiishi Kahama, aliyemtambulisha mrufani wa kwanza kuwa ni shemeji yake na ni muuzaji wa injini za magari.

Shahidi huyo alidai kuwa washtakiwa hao hawakuwa na kadi halisi ya gari licha ya kwamba aliwalipa fedha (hakuja kiasi) na akabakisha  Sh700,000 na walikubaliana wakimpa kadi ya usajili wa gari atamalizia kiasi kilichobakia.

Alidai baada ya kusubiri bila mafanikio, aliingia shaka na kutoa taarifa polisi ambao walimkamata na mrufani huyo kumtaja mrufani wa kwanza kuwa ndiye muuzaji halisi wa gari hilo.

Baadaye shahidi wa nne (kaka wa marehemu) alipofika Kituo cha Polisi Kahama kutoa taarifa mmiliki wa gari hilo ameuawa, walimkamata tena mrufani wa pili na shahidi wa nne alijitwika jukumu la kwenda kumtafuta mrufani wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Shahidi huyo alidai kuwa mrufani wa kwanza alikuwa akiishi Manzese jijini humo, walimsaka kwa zaidi ya wiki moja kabla ya kumkamata.

Shahidi wa tatu ambaye alikuwa shemeji wa marehemu, alidai siku moja kabla ya kifo cha shemeji yake, alimuona akiwa na abiria wawili kwenye teksi yake baada ya kupita karibu na makazi yake, akiulizia upatikanaji wa mbao ambazo abiria hao walikuwa wanazitaka.

Alidai kumtambua mrufani wa kwanza ambaye alikuwa anafahamika kwa jina la Musoma, ushahidi  ulioonekana kuwa msingi wa Mahakama kuhitimisha kuwa warufani walikuwa watu wa mwisho kuonekana wakiwa na marehemu akiwa hai.

Mrufani wa kwanza anadaiwa kutambuliwa na shahidi wa tatu na wa nane katika gwaride la utambuzi na upande wa mashtaka kuegemea kwenye ushahidi huo kuwa warufani ndiyo walihusika na mauaji hayo na pia walitoa nakala ya makubaliano ya uuzaji wa gari hilo.

Wakijitetea mahakamani, warufani hao walikanusha na kushangazwa kukamatwa kwa mauaji hayo pamoja na uuzaji wa gari hilo huku mrufani wa pili akieleza kuwa hajawahi kufika Mafinga, hivyo asingeweza kutekeleza mauaji hayo.

Mrufani wa kwanza alidai kuteswa na kulazimishwa kukiri kosa hilo wakati akiandika maelezo ya onyo akiwa kituo cha polisi.

Baada ya wazee wa baraza kutoa maoni, Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alikubaliana nao na kuwatia hatiani warufani kwa madai  walikuwa watu wa mwisho kuonekana wakiwa na marehemu.

Baada ya hukumu hiyo warufani hao wawili walikata rufaa wakitaja sababu sita zinazofanana ikiwamo ushiriki wa wazee wa baraza na kesi dhidi yao kutothibitishwa.

Walidai kuwa Jaji alikosea kisheria kutoa taarifa ya majumuisho na kuwaeleza wazee hao wajibu wao kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi.

Warufani hao waliowakilishwa na mawakili Jally Mongo na Jassey Mwamgiga, waliiomba Mahakama ya rufani kubatilisha mwenendo mzima wa kesi kwa sababu vifungu vya Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai kuhusu wazee hao vilikiukwa.

Wakili Mongo alidai kutokuwaeleza wazee wa baraza wajibu wao si sahihi huku akinukuu kesi ya Betram Nkwera dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini, katika rufaa ya jinai namba 567/2019 (haijaripotiwa).

Pili, alimkosoa Jaji kutojumlisha kiini cha ushahidi uliotolewa na mrufani wa kwanza na kuwa  kuna muhtasari wa kina kuhusu ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka.

Alieleza hakuna muhtasari wa kina unaoonyesha ushahidi uliotolewa na warufani na kutokuwepo, kuliathiri maoni ya wazee hao wa baraza.

Sababu ya tatu anasema Jaji hakuwaeleza wazee wa baraza mambo muhimu ya kisheria yaliyopaswa kutumika katika kesi hiyo yaliyotegemewa na Jaji katika kufikia uamuzi wake, lakini hayakuelezwa na Jaji katika muhtasari.

Wakili Mwamgiga aliyekuwa akimwakilisha mrufani wa pili, aliunga mkono hoja iliyowasilishwa na wakili mwenzake kuhusu kubatilishwa kwa shauri hilo kutokana na dosari za ushiriki wa wazee wa baraza.

Wakili huyo aliunga mkono msingi wa kukata rufaa na kuomba majaji hao kubatilisha mwenendo, hukumu na isiamuru kusikilizwa upya kwa shauri hilo kwa sababu kesi hiyo ina mashaka mengi.

Wakili wa Jamhuri, Yahaya Misango alikiri hoja ya warufani kuwa Jaji hakuwaeleza wazee wa baraza kazi zao, hata hivyo alidai wazee hao walitekeleza majukumu na kuwa kosa hilo la kutokuelezwa linatibika chini ya kifungu cha 388 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Wakili huyo alikubali kesi ya utetezi haikufupishwa maelezo sawa na kesi ya mashtaka huku akikiri Jaji hakuwaelekeza wazee wa baraza mambo kadhaa muhimu ya kisheria na pia mawakili wa warufani hawakueleza makosa hayo yalivyoachwa yalivyowaathiri warufani.

Baada ya kusikiliza hoja za kisheria za pande zote majaji walianza kwa kueleza kuwa inaonekana hakuna ubishi kwamba Jaji aliyekuwa akisikiliza hakuzingatia sheria kuhusu ushiriki wa wazee wa baraza ikiwamo kutowaeleza wajibu wao na baadaye katika majumuisho.

Majaji hao wanaeleza kuwa wanaungana na wakili wa Serikali kuwa kuna ushahidi kwenye kumbukumbu wazee wa baraza walishiriki kikamilifu katika shauri hilo na kutupilia mbali msingi wa kwanza wa kukata rufaa.

Baada ya uchambuzi wa shahidi wa nane aliyetambulishwa kwake na mrufani wa pili, majaji waliridhika na ushahidi wa mdomo wa shahidi huyo kuwa  alipokea gari kutoka kwa mwombaji wa kwanza mbele ya mrufani wa pili.

“Ni lazima tuonyeshe kwamba, jukumu la mrufani wa pili katika shughuli hiyo lilikuwa ni kuwezesha mkutano wa shahidi wa nane na muuzaji wa gari na mwenendo wa mrufani wa pili ambao haukuendana na hatia,” wameeleza majaji.

Wameeleza kuwa, wakati muuzaji wa gari hilo alikuwa amepotea (mrufani wa kwanza), mrufani wa pili alikuwa akiendelea na maisha yake ndani ya Wilaya ya Kahama hata baada ya kuhojiwa na polisi na kupata dhamana.

Majaji wameeleza hiyo ni ishara kwamba mrufani wa pili hakuwa na dhamira kama ya mrufani wa kwanza na kuwa katika kesi za jinai, mshitakiwa kamwe hapatikani na hatia kwa sababu ya udhaifu wa utetezi wake, huku wakinukuu kesi za mahakama ya rufaa.

“Kwa kuzingatia yaliyotangulia, hasa ukweli kwamba shahidi wa tatu  hakumtambua mrufani wa pili kwenye gari la marehemu na baada ya kuhojiwa awali na polisi, tumeridhika kwamba ushahidi dhidi yake ulikuwa wa doa sana kusababisha hatia,” wamesema.

Baada ya kushughulika na ushahidi wa mashahidi hao majaji hao waliangalia maelezo ya onyo ya  mrufani wa kwanza kwamba, katika kesi hiyo wanaona ilifanywa kwa hiari na mrufani wa kwanza na kuwa hakuna ushahidi unaweza kuwa bora kuliko wa mtuhumiwa anayekiri kosa.

Kuhusu msingi wa tatu wa rufaa kwamba mashahidi wa upande wa mashtaka hawakuwa wa kutegemewa, wanatupilia mbali msingi huo kwa sababu shahidi wa nne pekee ndiyo wameutilia shaka kwa kwa ni wa kubahatisha.

Wamesema shahidi wa tatu na nane walimtambua mrufani wa kwanza na katika gwaride la utambuzi hivyo kutupilia mbali sababu kuhusu kutokuwepo kwa upande wa mashtaka kuita mashahidi muhimu, kwani mashahidi hao wasingeongeza thamani yoyote.

“Kwa hiyo tumeridhika kwamba kesi dhidi ya mrufani wa kwanza ilithibitishwa bila shaka yoyote, rufaa ya mrufani wa kwanza inatupiliwa mbali kwa jumla wake,” wameeleza majaji hao

“Kwa sababu ambazo tumeonyesha hapo awali, tunaruhusu rufaa ya mrufani wa pili na kuamuru aachiliwe mara moja kutoka gerezani.”

Related Posts