Mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa Salvatory Edward ametangazwa kuwa Kocha Msaidizi wa Pamba Jiji FC, ambapo anatarajiwa kuwa msaidizi wa Kocha Goran Kopunovic ambaye alitangazwa kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo mapema wiki hii.
Kupitia Ukurasa wa Instagramu wa Pamba Jiji wamemtangaza Kocha Salvatory Edward Kuwa Kocha Msaidizi wa timu hiyo, ambapo ni mwendelezo wa timu hiyo kuimarisha benchi lake la ufundi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Meneja wa Timu hiyo Ezekia Ntibikeha amesema mpango wao ni kuwa na benchi la ufundi bora ambalo litaiwezesha timu hiyo kufanya vizuri kwenye Ligi baada ya kupanda daraja msimu huu 2023/24.
“Tumemtangaza Salvatory Edward kuwa Kocha Msaidizi wa Pamba Jiji, wote ni mashahidi Kocha huyu amekuwa na mchango mkubwa kwenye soka la Tanzania ambapo ana leseni A ya CAF na kwa namna alivyocheza soka katika nchi hii kwa mafanikio makubwa tunaamini ataongeza thamani kwenye timu yetu”
“Lengo ni kuwa na benchi la ufundi bora litakalotuwezesha kuwa na timu bora na amepewa mkataba wa Mwaka mmoja, ambapo atakuwa msaidizi wa Kocha Goran Kopunovic “
“Tunaendelea kuimarisha benchi letu la ufundi kwa kuwa tumepanga kuanza kambi yetu mapema iwezekanavyo ili tupate maandalizi ya kutosha kabla ya ligi kuanza maana Mapendekezo ya kocha wetu tunatakiwa kupata wiki 12 za maandalizi kabla ya ligi kuanza hivyo wanapamba wategemee makubwa kwenye timu yao”
Salvatory Eduard amewahi kuwa Kocha wa Pamba FC kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Pamba Jiji FC msimu wa 2020/21, ambapo hata hivyo hakumaliza msimu kwa kuwa nafasi yake ilichukuliwa na Kocha Ulimboka Mwakingwe baada ya timu hiyo kutokuwa na matokeo mazuri.