Mikumi. Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka amemuagiza mkandarasi anayejenga uwanja wa ndege kwenye hifadhi ya Taifa ya Mikumi kufanya ujenzi usiku na mchana, ili ukamilike kwa wakati na kuanza kutumika kuingiza watalii ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumzia ujenzi huo leo Jumapili Juni 23, 2024, Shaka amesema kamati ya ulinzi na usalama ilitembelea na kubaini mwenendo wa ujenzi kutoridhisha.
“Tumekagua ujenzi wa uwanja huu wa ndege hapa hifadhi ya Taifa ya Mikumi wenye uwezo wa kupokea ndege kubwa, umefikia asilimia 60 na tulitegemea kukabidhiwa Julai 2, mwaka huu, lakini kwa mazingira yalivyo, uwanja hautakamilika ndani ya wakati na hatujaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wake,” amesema Shaka.
Amesema Serikali imetenga zaidi ya Sh20 bilioni kwa ajili ya ujenzi wake, hivyo amemtaka mkandarasi aujenge usiku na mchana, ili ukamilike kama ilivyokusudiwa.
“Hatujaridhishwa na ujenzi unavyoendelea kwa kuwa hitajio letu ni kuongeza watalii wanaokuja hapa kwa ndege na uwanja usipokamilika kwa wakati tutapata hasara kama Taifa,” amesema Shaka.
Amesema awali uwanja huo ulikuwa na uwezo wa kupokea ndege moja kwa siku, lakini baada ya kampeni ya Royal Tour ilifika wakati ndege zaidi ya 10 zikawa zinatua kwa siku, hivyo ukikamilika ndege za kimataifa zitakuwa na uwezo wa kutua na kuongeza watalii wanaoitembelea hifadhi hiyo.
Ofisa mhifadhi mwandamizi wa Hifadhi ya Mikumi, Alfred Mwakusye amesema mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa asilimia 38 ya malipo yake na ujenzi umefikia asilimia 60.
“Tumeshamlipa mkandarasi asilimia 38 kama mkataba unavyosema, tumepokea maelekezo ya Serikali kupitia kwa mkuu wa wilaya tutahakikisha tunafanya kazi bega kwa bega na mkandarasi kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati,” amesema Mwakusye.
Amesema ujenzi wa uwanja huo ulianza Mei, 2023 na unapaswa kukamilika Julai 2, 2024.
“Lakini changamoto ya mvua pia imesababisha ujenzi kukushindwa kuendelea katika vipindi tofauti,” amesema.
Moses Dotto, mkazi wa Mikumi amesema uwanja huo ukikamilika, watalii wataongezeka na wakazi wa wilaya hiyo watanufaika na ajira za upagazi na nyinginezo.
Naye Edna Marai, amesema wanawake wengi wa eneo la Mikumi ni wajasiriamali wa bidhaa za asili, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo, utatoa fursa kwao za biashara.
“Tutapata wateja wengi wa nje, kwa hiyo maisha pia labda yatabadilika kwa sababu tutaongeza kipato,” amesema Marai.