Simba yavunja ukimya hatma ya Chama

Wakati taarifa zikizidi kuenea kwamba kiungo mkongwe wa Simba, Clatous Chama amesaini Yanga, uongozi wa Simba umetoa kauli juu ya Mzambia huyo.

Msemaji wa Simba, Ahmed Ally amesema Chama amemaliza mkataba na klabu hiyo na kwamba kinachoendelea sasa ni mazungumzo ya kutafuta namna ya kumuongezea mpya.

Ahmed amesema, kama haitafanikiwa kumuongezea Simba itatafuta namna ya kuagana na kiungo huyo fundi.

“Hadi sasa mimi kama Msemaji bado sijapata uhalisia wa kipi kinaendelea kama ameongezewa mkataba au viongozi wameamua aondoke ama mazungumzo bado yanaendelea,” amesema Ahmed wakati akiwa mubashara akijibu maswali ya mashabiki kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

“Likishamalizika kwa ngazi ya juu, uongozi unanipa taarifa au watatoa taarifa na Wanasimba wapate kufahamu kipi kinaendelea juu ya Mwamba wa Lusaka. Tuwe wapole ndugu zangu hadi Jumatatu tutajua kinachoendelea,” amesema Ahmed, mtangazaji wa zamani wa RFA na Azam Media.

Aidha Ahmed amesema kuwa, endapo Simba itafanikiwa kumuongezea mkataba kiungo huyo, itakuwa ni kwa maslahi ya klabu hiyo na kama itaamua kutomuongezea mpya pia itakuwa kwa maslahi ya Wekundu hao.

Mashabiki wa Simba wako katika presha kubwa, kiu yao ni kujua hatma ya kiungo huyo mchezeshaji  anayedaiwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga.

Related Posts