LEICESTER City, Ipswich Town na Leeds United zimerejea Ligi Kuu ya soka ya England baada ya kufanya vizuri katika Ligi ya Championship na mechi za mtoano (play-off).
Leicester City imerejea Ligi Kuu baada ya kutwaa ubingwa wa Championship, ambayo ni ligi ya pili kwa ukubwa huko England, wakati Ipswich Town imerejea Ligi Kuu baada ya kushika nafasi ya pili katika Ligi hiyo ya Championship, huku Southmpton, iliyoshika nafasi ya nne Championship, imerejea Ligi Kuu baada ya kushinda mechi za mtoano (play offs) dhidi ya West Bromwich Albion na Leeds United.
Timu hizo tatu zinachukua nafasi za Burnley, Sheffield United na Luton Town zilizoshuka daraja msimu mmoja baada ya kupanda.
Kwa England, timu mbili zinazoshika nafasi ya juu katika Ligi ya Championship, hupata tiketi ya moja kwa moja kupanda daraja kwenda Ligi Kuu, wakati zinazoshika nafasi ya tatu, nne, tano na sita huwa na nafasi ya kuungana na timu hizo mbili, lakini hulazimika kucheza mechi za nyumbani na ugenini baina yao na mshindi hufuzu Ligi Kuu.
Nafasi ya pili inayotolewa kwa timu zilizokosa nafasi ya moja kwa moja, haihusishi timu ambazo zimeshuka daraja kutoka Ligi Kuu. Yaani zile timu nne zilizoshika nafasi ya kuanzia ya tatu hadi sita hukutanishwa katika mechi za kuanzia nusu fainali na baadaye fainali kupata mshindi ikiwa na maana kila timu hucheza mechi nne.
Hii ni kanuni bora ya kupata timu zinazopanda daraja tofauti na ile tunayotumia huku Tanzania.
Timu kama Tabora United – kwa kuangalia msimu huu—ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu, lakini ikapewa nafasi mbili za kujiuliza kabla ya kujihakikishia tiketi ya kubaki katika ligi hiyo.
Maana yake ni kwamba nafasi moja kati ya zile tatu zilizotengwa kwa ajili ya timu kupanda daraja, imeporwa na timu ya Ligi Kuu kwa kucheza mechi mbili tu dhidi ya timu inayotaka kupanda daraja.
Huu si utaratibu mzuri. Si busara timu iliyokuwa Ligi Kuu kupambana na timu iliyocheza Ligi ya Championship kuwania tiketi ya kucheza daraja ambalo ilifanya vibaya. Labda ingekuwa busara kama timu inayotakiwa kuwa ya tatu kushuka, ipambane na timu nyingine iliyokuwa katika hatari ya kushuka kuamua ipi ishuke.
Yaani kama nilivyotolea mfano Tabora United, uliyoshika nafasi ya 14 katika Ligi Kuu na JKT Tanzania, zilizocheza play-off ya Ligi Kuu ili kuamua ya kubaki, ingeishia hivyo na sio aliyeshindwa kwenda kucheza tena na ile ya Ligi ya Championship kwa nia ya kubakiza zile nafasi tatu za kupanda daraja kwa Championship tu.
Timu inayoshika nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu haitakiwi ijiulize kwa timu kutoka chini, bali kwa timu ambazo ilipambana nazo katika Ligi Kuu. Huko ndiko kujiuliza na huko ndiko kupewa nafasi ya pili kama utamaduni wa mpira wa miguu ulivyo.
Kwa kanuni hii inaweza kuwa vigumu sana kwa msimu mmoja kushuhudia timu tatu kutoka Championship zikipanda daraja kwa kuwa ni ngumu sana kwa timu ya Ligi Kuu iliyokumbana na ugumu mkubwa kwenye Ligi Kuu, kuondolewa na timu ambayo haikukumbana na ugumu mkubwa kwenye Championship.
Ni kweli msimu ul;iopita Mashujaa iliing’oa Mbeya City katika hatua hiyo, lakini hutokea kwa nadra kutokana na tofauti za timu za madaraja hayo na hata maandalizi yao ya ushiriki kwa msimu mzima.
Pamoja na hayo, Championship imekuwa ikimalizika mapema sana na kusubiri Ligi Kuu ambayo imekuwa ikichelewa kumalizika. Maana yake ni kwamba timu ya Ligi Kuu ambayo inatakiwa ishuke, inakuwa bado iko katika hali ya kimchezo kulinganisha na timu iliyokaa muda mrefu bila ya mechi na inawezekana kabisa wachezaji wake wengi wameshaingia mikataba ya kuchezea timu nyingine.
Kuwarejesha kambini kujiandaa kwa mechi za play off kwa timu ya Championship ni kibarua kigumu na kinachohitaji fedha za ziada kulinganisha na timu ambayo ndio kwanza imetoka kumaliza mechi zake za msimu.
Ni muhimu kwa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kuangalia vizuri kanuni hii na kuirekebisha ili kuwe na ushindani stahiki wa kupanda daraja na wa kupigania kubakia Ligi Kuu.
Ni muhimu zile nafasi tatu zilizotengwa kwa ajili ya timu za Championship kupanda Ligi Kuu zibakie kuwa za Championship tu na si kuachia moja iviziwe na timu za Ligi Kuu. Ushindani wa haki ni pale timu za Ligi Kuu zinapopambana kutafuta timu inayotakiwa kubaki daraja hilo, na timu za Championship zipambane kuwania tiketi ya tatu ya kupanda.
Yaani ikiwezekana timu zilizoshika nafasi ya tatu hadi ya sita ya Ligi ya Championship zicheze tena play-off ya kuwania nafasi moja iliyosalia ya kupanda Ligi Kuu kama ilivyo kule England.
Ni kawaida na utamaduni wetu kutotaka kulinganisha mafanikio ya Ligi za nchi za Ulaya eti kwa madai kuwa “wale wameendelea, si wa kujilinganisha nao”, lakini siku zote tunatakiwa tumfikie mafanikio ya waliofanya vizuri. Hata kwa kufanya hivyo kwa hatua na si kwa usiku mmoja.
Tuige kanuni hii ya Ligi Kuu ya England ambayo ni moja ya Ligi Bora kabisa duniani.