Unguja. Uamuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kutangaza dhamira ya kumuongezea muda Rais Hussein Ali Mwinyi wa kuongoza kutoka miaka mitano hadi saba, umewaibua wadau wakipinga hatua hiyo, huku wakiihusisha hatua hiyo na kile walichokiita nia ovu ya kuvunja Katiba na kukiuka misingi ya demokrasia.
Wadau hao wakiwemo wanazuoni wa sayansi ya siasa, wamekwenda mbali zaidi na kuonyesha ugumu wa uwezekano wa jambo hilo kutokea, kwa hoja kuwa Zanzibar haina nguvu ya ushawishi wa kufanya mabadiliko makubwa hasa ya Katiba.
Vuguvugu la nyongeza ya muda wa Rais Mwinyi kukaa madarakani, limeibuliwa leo Jumapili, Juni 24, 2023 na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Dimwa wakati akifunga mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Wilaya ya kichama ya Dimani uliofanyika ofisi za wilaya hiyo iliyopo Kiembesamaki.
Katika maelezo yake, Dk Dimwa amesema wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya CCM, Zanzibar wamepitisha pendekezo la kuishauri Kamati Maalum kuridhia kuongeza muda wa Rais Mwinyi, kuongoza nchi katika muhula wake wa kwanza kwa kipindi cha miaka saba badala ya mitano.
Pendekezo hilo limeibua mjadala mkali mitandaoni kutoka kwa wadau wa siasa na wanasiasa wa vyama vya upinzani.
Hata hivyo, CCM Zanzibar si wa kwanza kuibua hoja kama hiyo; imesikika mara kadhaa katika majukwaa ya viongozi wa chama hicho bara, tangu enzi za uongozi wa hayati John Magufuli.
Kauli hizo zimeendelea kusikika kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho na jumuiya zake, hata wakati huu Tanzania ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kikatiba atamaliza awamu yake ya kwanza ya urais mwaka 2025.
Iwapo atagombea kwa muhula mwingine na kushinda, atamaliza urais wake mwaka 2030, lakini kumekuwepo na baadhi ya viongozi wanaodai anapaswa aachwe aongoze hadi mwaka 2035.
Msingi wa kauli ya Dk Dimwa ni kile alichodai Rais Dk Mwinyi ametekeleza Ilani ya chama hicho kwa zaidi ya asilimia 100 kwa miaka mitatu.
Chama hicho, alisema kimeona hakuna haja kwa Serikali kuingia gharama na hasara kufanya uchaguzi, aliodai ni matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.
“Wajumbe wa sektetarieti tumejadili na kutathmini kwa kina juu ya utendaji wa Rais Mwinyi, tukajiridhisha kuwa hakuna mbadala wake na anastahili aongoze nchi kwa kipindi cha miaka saba ili apate muda mzuri wa kufanya mapinduzi ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii,” alisema.
Alisema maamuzi yao yatafuata taratibu za kikatiba na kikanuni kwa kuyawasilisha katika vikao vya ngazi za juu ili vitoe baraka zake.
Baada ya baraka za vikao vya juu, alisema litapitishwa kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar kufanyika mabadiliko ya baadhi ya vipengele vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ili uchaguzi mkuu ufanyike kila baada ya miaka saba.
Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu kauli hiyo, mwanazuoni wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mohamed Bakari amesema kuna chembechembe za misingi ya kiimla, yaani ukiukwaji wa matakwa demokrasia.
Shinikizo hilo halimaanishi washinikizaji wamependezwa na utendaji wa kiongozi husika, bali wanasema wakilenga kwenda kinyume na demokrasia.
“Watu hadi wameweka miaka mitano kuna kazi kubwa ilifanyika, mara nyingi kwa Tanzania ukisikia Rais anatakiwa kuongezewa muda ni misingi ya kiimla ambayo inakwenda kinyume na demokrasia,” alisema.
Kwa mtazamo wake, Profesa Bakari alisema vipindi viwili vinavyojumuisha miaka 10 ni muda unaotosha kwa kiongozi kutekeleza ahadi zake, akishindwa anayemfuata ataendeleza.
Kwa upande mwingine, mwanazuoni huyo alionyesha ugumu katika uwezekano wa jambo hilo kutokea, akisema katika mabadiliko ya Katiba, aghalabu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo yenye nguvu zaidi.
Sambamba na hilo, ugumu mwingine alieleza unatokana na kukosekana uwiano yaani Zanzibar kiongozi aongoze kwa miaka saba, wakati bara kwa miaka mitano.
“Ni kazi kubwa kupitisha hilo kwa sababu Jamhuri ya Muungano ni miaka mitano, hakutakuwa na uwiano eneo moja miaka saba na lingine mitano, haiwezekani,” alisema.
Mtazamo mwingine wa profesa huyo, alisema kauli hiyo ni propaganda hasa katika kipindi ambacho uchaguzi unakaribia.
“Nadhani ni siasa za propaganda za kuwaaminisha wananchi kwamba Rais aliyepo madarakani ni mzuri na anapaswa kuongezewa muda,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Bakari, kauli kama hizo ziliwahi kutolewa katika vipindi mbalimbali vya viongozi tofauti, lakini hazikufikia popote, zilibaki kuwa propaganda.
Hata hivyo, kumeonekana kuna njia nyembamba ya jambo hilo kutekelezeka, kwa mujibu wa Mwenyekiti mstaafu wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji.
Kushindikana kwa jambo hilo, kunatokana na kile alichosema CCM Zanzibar haina nguvu, labda kama kuna mkono wa chama hicho upande wa Bara, akifananisha na lilivyowahi kuibuka enzi za Salmin Amour na baadaye likapotea.
“CCM kuu haiwezi kukubali kwa sababu, kwanza Katiba hairuhusu, katiba inasema vipindi vya rais ni miaka mitano mitano sasa jambo hili liwezekane lazima wabadilishe Katiba.
“Sawa wanaweza kwenda baraza la wawakilishi wakasema wabadilishe sheria, lakini lazima kupigwe kura ya maoni na kura ipigwe, lazima wananchi wakubali na sidhani kama wanaweza kwenda huko labda walazimishe kama wanavyolazimisha uchaguzi,” alisema.
Aliihusisha kauli hiyo na kile alichokiita uchawa, akifafanua wanaosema wana dhamira ya kunyoosha mambo yao kadhaa.
Katika maelezo yake, alisema Kamati maalumu ya Zanzibar haina nguvu kwani iliwahi kutaka Dk Ghalib Bilal (Makamu wa Rais awamu ya nne) awe Rais na Amani Karume akapata kura tisa lakini Halmashauri Kuu, ilirudisha jina la Amani na akawa Rais wa awamu ya sita.
“Haijawahi kamati maalumu ya Zanzibar kujitutumua kutaka jambo libadilike likakubalika na ukiona limekubalika limetakiwa na CCM Tanzania Bara,” alisema
Pendekezo hilo la CCM Zanzibar, lilipingwa pia na mchambuzi wa siasa visiwani humo, Ali Makame aliyesema iwapo litatekelezwa ni kosa na litatoa mwanya kwa kila anayeingia madarakani kutaka kubadili Katiba ili aongeze muda wa kuongoza.
“CCM wanaweza kupitisha chochote kutokana na wingi wao lakini ingekuwa jambo la busara nafasi hiyo wakaitumia kukuza demokrasia kuliko kudumaza demokrasia,” alisema.
Alisema kwa sasa Watazania wanapigana kubadilisha katiba kumpunguzia madaraka Rais na kukuza demokrasia, kwa kilichozungumzwa na CCM kinashangaza.
Hata hivyo, alieleza pamoja na wingi wa wafuasi wa CCM jambo hilo linaonyesha wanaogopa.
“Anayependekeza hili ni kutaka kujipendekeza kwa Rais, lakini angeweza kumsaidia Rais kwa njia nyingine chama kipendwe kwa kutatua changamoto za wananchi sio kwa ujanja huu,” alisema.
Katibu wa Itikadi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT -Wazalendo, Salim Biman alisema CCM imeshaona mambo yameikalia kooni sasa imeanza kutapatapa.
“Huu ni uoga wa CCM wanajua hawana tena lao uchaguzi ujao kutokana na mambo ya ovyo waliyofanya. Pia kufanya hivi ni kuvunja katiba na sheria za nchi na hili wafanikiwe wanatakiwa wapige kura ya maoni sio kupeleka baraza la wawakilishi,” alisema.
Mmoja wa vigogo ndani ya Serikali akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amesema suala hilo linaangaliwa kwa jicho la uchaguzi wa mwaka 2030.
“Unajua mwaka 2030 kama hali itakwenda hivi tutakuwa hali ngumu, inaweza kutingisha utulivu wetu kwa maana, wagombea urais Bara na Zanzibar watakuwa wapya, kwa miaka ya karibuni viongozi wamekuwa wanapishana.
“Kwa hiyo kwa kuliona hilo na ili kupishanisha, nafikiri ndio mikakati imeanza sasa la sivyo hali haitakuwa rahisi, yaani una mgombea mpya Bara, halafu una mgombea mpya Zanzibar na labda siasa ziwe moto moto kama za mwaka 2015 hali itakuwa ngumu,” alisema.
Pamoja na kukiri kwamba kitendo hicho ni kosa kikatiba, Mtaalamu wa sheria, Wakili Abdalla Mohamed, alisema iwapo CCM itataka kutekeleza hilo haitashindwa kwa sababu ya nguvu.
Hata hivyo, alisema hafikirii kama RaisMwinyi atakubali kusigina Katiba kiasi hicho katika uongozi wake isipokuwa yanaweza kuwa maneno ya kisiasa.
Alisema kubadilisha Katiba wakati kiongozi yuko madarakani kwa ajili ya kumlinda, ni hatari na iwapo wakitaka kufanya hivyo ni bora wakabadilisha kwa utaratibu.
“Kubadilisha Katiba wakitaka hawashindwi kwa sababu wataenda barazani hilo ni jambo jepesi, ila shida inakuja kwa nini Katiba ibadilishwe kwa ajili ya mtu mmoja? sidhani kama hili linaweza kutokea na likitokea ni hatari sana.”
Wakili huyo aliongeza:“Leo unabadilisha Katiba kisa mtu mmoja amefanya vizuri, je ikitokea akaja mwingine naye akafanya vizuri au vibaya je mtabadilisha pia Katiba? au itakuwaje huu sio utawala bora.”