Waratibu maandamano kupinga biashara ya ‘makahaba’ Dar

Dar es Salaam. Uongozi wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) umesema hatua ya kukamatwa wanawake wanaodaiwa kuuza miili yao ‘makahaba’ katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, ni njia mojawapo ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini.

Ili kuunga mkono oparesheni hiyo, SMAUJATA imesema inaratibu maandamano ya kupinga biashara hiyo, huku ikiwataka viongozi wa wilaya na mkoa katika maeneo mbalimbali nchini kukomesha biashara hiyo.

Imesema oparesheni ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko ya kuwasaka na kuwatia ndani wote wanaodaiwa kufanya biashara hiyo haikuwadhalilisha au kunyanganya haki za watu kama baadhi ya wanaharakati na wanasheria wanavyodai, upo ukiukwaji wa sheria unaotendeka.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, alianza kampeni ya kukamata kundi la wanawake na wanaume wanaojihuhisha na biashara ya ngono hivi karibuni na video mbalimbali zilisambaa zikimuonyesha kiongozi huyo usiku akiingia nyumba za kulala wageni na kuwaondoa watu waliomo ndani na kuwapeleka mahabusu, kitendo kilichoibua tafsiri ni uingiliaji wa faragha za watu.

Jana Jumamosi, Juni 22, 2024 akizungumza na waandishi wa habari jijini  Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Maadili wa SMAUJATA, Fredrick Rwegasira amesema badala ya watu kupinga hatua zinazofanywa na mkuu huyo wa wilaya, ni muhimu kumuunga mkono kwa mustakabali wa maadili ya jamii.

“Haiwezekani kubariki vitendo viovu kwenye jamii, Bomboko anapambana na chanzo cha tatizo, ni muhimu viongozi wengine waige haya kwa mustakabali wa kizazi chetu, tuache ushabiki unaoambatana na fikra finyu,” amesema.

Kwa upande wake, Wakili Aristarko Msongela ambaye ni Katibu wa Idara ya Sheria Taifa SMAUJATA, amesema ukamataji wa makundi hayo ni kuilinda jamii dhidi ya maradhi.

Kwa sheria zilizopo sasa, wakili huyo amesema wapo tayari kuwasilisha maoni yao juu ya mambo yanayopaswa kufanyiwa mabadiliko kwenye sheria, ili ibainike ni mtu wa namna gani anapaswa kuwajibishwa kwenye mazingira gani na wakati gani hasa anapojihusisha na biashara ya ngono.

Wakili Msogela amesema sheria ya kanuni ya adhabu ya 145(2) inabainisha pale mwanaume anapodhihirika kuishi au kuwa na uhusiano na kahaba au ikidhihirika kuwa anaamuru, anatoa maelekezo au ana ushawishi ya mienendo ya kahaba kwa namna inavyoonyesha anasaidia, anashawishi au anamlazimisha mwanamke huyo kufanya ukahaba au mtu mwingine yeyote.

Kifungu hicho kinafafanua asipoiridhisha mahakama vinginevyo atachukuliwa anajua anaishi kwa kutegemea kipato kutokana na ukahaba.

Msongela mbali na masuala ya maboresho ya sheria amesema SMAUJATA wanaandaa maandamano kupinga biashara ya ngono nchini, ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono viongozi wanaokabiliana na biashara hiyo.

Naye Ridhiwani Salumu kutoka SMAUJATA, amesema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupinga biashara ya ngono kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Vijana tuwaunge mkono watu au taasisi zinazojitokeza kupinga au kutokomeza biashara hii haramu, tuisaidie Serikali hasa kuibua maeneo biashara hii inapofanyika na kuwaibua na wadau wanaowezesha biashara hii kufanyika,” amesema.

Aipozungumza na Mwananchi Digital Jumanne iliyopita, Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko alifafanua jambo hilo huku akieleza haki zote zilifuatwa katika ukamataji, ikiwemo kuwekwa huru kwa dhamana kwa waliokuwa wakihitaji.

“Wote waliokamatwa, dhamana ziliachwa wazi, wengine walipelekwa mahakamani wakakiri makosa wakamrishwa kifungo au kulipa faini, wengine walilipa faini wakaachiwa hakuna aliyekaa zaidi ya siku moja.

“Zile kelele za kusema wengine wamelala chini, tumekamata watu 60 ni uongo kwa sababu idadi kubwa tuliyowahi kukamata ni 30 kule Sinza ambapo wanawake walikuwa 23 na wanaume,” amesema.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo madai ya kutakiwa kuwalipa fidia ya Sh36 bilioni watuhumiwa hao wakidai walidhalilishwa wakati wa ukamatwaji wao.

Related Posts