Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Sarah Katanga amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan atoe tamko la kutunga sheria ya dharura itakayowalinda watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye ualbino, ili waondokane na mauaji dhidi yao.
Katanga ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 24, 2024, siku chache baada ya tukio la mtoto Asimwe Novath (2) mwenye ualbino, kuporwa mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana nyumbani kwao Kijiji cha Mulamula, wilayani ya Muleba, mkoani Kagera Mei 30, 2024 na siku 19 baadaye kupatikana mwili wake, huku
baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa. Tayari mwili huo umeshazikwa.
Sarah amesema Rais Samia akitoa tamko la kupeleka muswada wa sheria bungeni kwa dharura ili upitishwe, watu wenye ualbino watapata amani ya kuishi kwenye nchi yao.
Amesema watu wenye ualbino wamekuwa wakiishi katika nchi yao kama wakimbizi, hasa vijijini, kwani kinamama wanashindwa hata kwenda kukata kuni, kisimani kuchota maji na watoto wameathiriwa kisaikolojia kutokana na matukio ya iana hiyo.
“Rais Samia akisema mara moja sisi wenye ualbino tunapona tunamuomba atoe tamko, ili vitendo hivi viishe na upelekwe muswada bungeni wapitishe kwa ajili ya ulinzi wetu,” amesema Sarah.
Amesema matukio ya mauaji au kutolewa viungo vya wenye ualbino yamekuwa yakitokea wakati wa kuelekea katika uchaguzi mbalimbali, jambo ambalo Serikali imekuwa ikitoa matamko ya kulaani bila ya kuweka mikakati.
Amesema hakuna sheria yeyote iliyotungwa kwa dharura, ili kukomesha vitendo hivyo huku akitolea mfano wa mnyama Faru aliyeitwa John alikuwa amekufa Serikali ilitunga sheria kali ya kuwalinda wanyama.
Kutokana na hilo, chama hicho kimesisitiza kuwepo kwa Katiba mpya, ili watu wenye ualbino wapate haki ya kuishi na kulindwa.
Naye mwanachama wa chama hicho, Luku Kitele amesema suala wenye ualbino kukatwa viungo na kuuliwa limeanza tangu mwaka 2006, hivyo wamekuwa wakiishi wa hofu yangu wakati huo.
Amesema pia ni muhanga, kwani alinusurika mara mbili kukamatwa na watu wasiojulikana na kwamba alitoa taarifa polisi.