CCM, Ikulu Zanzibar waikana kauli ya Dk Dimwa

Dar es Salaam. Hapana. Ndivyo unavyoweza kutafsiri karibu kila mchango wa mdau wa siasa aliyezungumza na Mwananchi kuhusu  kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Dimwa, aliyetaka Rais Hussein Mwinyi aongezewe muda wa kukaa madarakani kutoka miaka mitano hadi saba.

Msingi wa kauli hiyo ya Dimwa ni kile alichoeleza kuwa  sekretarieti ya kamati maalum ya chama hicho,  imetathmini na kujiridhisha na utendaji wa kiongozi huyo aliyetekeleza kwa zaidi ya asilimia 100 Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa miaka mitatu pekee, hivyo kupendekeza aongezewe miaka ya kutawala hadi kufikia saba.

Ukiacha mijadala ya mitandaoni kupinga kauli hiyo, kilichozungumzwa na Dk Dimwa kimepingwa hadi na viongozi waliowahi kukitumikia chama hicho katika nafasi nyeti.

Upinzani wa viongozi hao unatokana na hoja walizoziibua kuwa, kilichozungumzwa na kiongozi huyo kinakwenda kinyume na Katiba ya nchi, ambayo inapaswa kuheshimiwa.

Ikulu ya Zanzibar nayo imeikana kauli hiyo kwa kusema, Rais Mwinyi ataongoza kwa kufuata utaratibu uliowekwa wa miaka mitano na si vinginevyo.

Wakati wengine wakiibua upinzani huo, Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, Yusuph Makamba amehoji kwa nini watu wanashangazwa na kauli ya Dimwa,  ilhali kabla yake wapo waliowahi kuzungumza kama hivyo na hakuna aliyeshangaa.

Alichokisema Dimwa kinaakisi kauli mbalimbali za baadhi ya viongozi wa CCM na hata wabunge wakitaka Rais Samia Suluhu Hassan aongezewe muda.

Aidha, kauli kama hizo, zilikuwepo pia hata wakati wa utawala wa hayati John Magufuli.

Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Pius Msekwa alisema kauli iliyotolewa kuhusu kumwongezea muda rais huyo, inasikitisha na kuhuzunisha kwa kuwa inachezea Katiba ya nchi.

Kwa mujibu wa Msekwa, Katiba ya nchi si kitu cha kuchezea kama kundi la watu fulani linavyotaka, akisisitiza inapaswa kuheshimiwa.

“Katiba ya nchi si kitu cha kuchezea kama kundi la watu fulani linavyotaka, ni vitu vya kuheshimiwa hadi inapotokea haja ya kuirekebisha kupitia taratibu  zinazopaswa,” alisema.

Alikwenda mbali zaidi na kueleza jaribio kama hilo limewahi kutokea enzi za uongozi wa Salmin Amour, lakini lilizimwa katika vikao vya ndani vya CCM.

Msekwa ambaye pia amewahi kuwa mtendaji mkuu wa chama cha TANU kilichozaa CCM na Spika mstaafu wa Bunge, , alisisitiza ni huzuni kauli kama hizo kuendelea kuwepo hata baada ya jaribio la enzi hizo kuzimwa.

“Mimi inanihuzunisha kuona kwamba bado kuna madai ya kuchezea Katiba yetu badala ya kuiheshimu,” alieleza.

Hata hivyo, alisema ni imani yake wenye mitazamo kama hiyo, watarejea historia na kuona namna ya kujirekebisha.

Kauli ya Dk Dimwa ilipata upinzani hata kutoka Ofisi ya Rais Ikulu ya Zanzibar, ikieleza kiongozi huyo ataheshimu utaratibu uliopo wa kuongoza kwa miaka mitano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Charles Hilary, wale wote wenye mawazo tofauti na hayo wanapaswa kufunga mjadala huo.

Katika taarifa hiyo, Ikulu ya Zanzibar ilisisitiza kauli hiyo haina tija wala faida kwa Zanzibar na Chama cha Mapinduzi kinachofuata misingi ya demokrasia.

Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuph Makamba, alisema watu hawapaswi kumshangaa Dk Dimwa, kwa kuwa kauli kama hizo zimewahi kutolewa na viongozi wengi katika awamu mbalimbali za Serikali.

Katika maelezo yake, alimtolea mfano Rais wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi katika moja ya mikutano ya CCM enzi za utawala wa John Magufuli, alitaka aongezewe muda.

“Kwa nini hamjamshangaa Mzee Mwinyi akisema Magufuli aongezewe muda na alisimama kwenye mkutano wa CCM na akasema anafanya kazi vizuri kuliko sisi, hata Ndugai (Job) amewahi kusema,” alihoji.

Hata hivyo, Makamba alieleza hata Dk Dimwa hakusema kama kauli yake ni uamuzi, bali aliweka wazi ni maoni anayotarajia kuyapeleka katika vikao vya juu.

“Itakuwa hoja kama vikao vya juu alikosema atalipeleka vitalipitisha, lakini kwa sasa yanabaki kuwa maono yake binafsi na Dimwa si wa kwanza kutoa maoni hayo,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu usahihi wa kauli kama hizo, alijibu si ajabu huku akifafanua, “Chanda chema huvikwa pete.”

CCM Zanzibar, bara zakana

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Zanzibar, Khamis Mbetto alisema kilichozungumzwa na Dk Dimwa ni maoni yake binafsi, haukuwa msimamo wa chama kama ilivyoaminiwa na wengi.

Maoni hayo ya Dk Dimwa, alisema yametokana na ziara ya sekretarieti ya Kamati Maalum ya chama hicho iliyohusisha kupokea taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Baada ya kupokea taarifa hizo, alisema Dk Dimwa ametoa maoni hayo na si msimamo wa wajumbe wa sekretarieti na hata hivyo anayo nafasi ya kuyawasilisha maoni hayo katika vikao vya juu.

“Yalikuwa maoni yake lakini msimamo wa CCM ni kwamba Rais Mwinyi ameapa kutumikia kwa miaka mitano na Katiba ya nchi na chama inasema hivyo,” alisema.

Kuhusu kauli ya Dk Dimwa, alisema ni kama aliteleza isipokuwa bado ana nafasi ya kupeleka pendekezo lake hilo katika vikao vya juu ambavyo yeye ni mjumbe.

Kwa sababu suala la kumuongezea kiongozi muda linahusisha mabadiliko ya Katiba ya nchi na chama, alisema kuna michakato mingi kufanikisha hayo.

Kwa mujibu wa Mbetto, kauli ya Dk Dimwa  isichukuliwe kuwa ndiyo msimamo wa sekretarieti na chama kwa ujumla.

Alisema ni kweli utaratibu wa CCM hufanya maamuzi yake kwa vikao na jambo hilo halikupitia mchakato huo, hivyo ni maoni tu bado haujawa msimamo.

Kwa upande wake,  Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala,  alisema hakuna jambo hilo, huku akidokeza tayari bajeti ya kugharimia chaguzi zote imeshapangwa, hivyo chaguzi zitafanyika kama kawaida.

Katika mahojiano yake katika kipindi cha Power Breakfast kinachoendeshwa na Kituo cha Redio cha Clouds  cha jijini Dar es Salaam, Makala alisisitiza kilichozungumzwa ni wazo bado si uamuzi.

“Kwa ufupi sana niseme, hilo jambo halipo,” alisema huku akisisitiza CCM inaendeshwa na vikao na kwamba kikao kilichotoa msimamo huo si kile kinachoongozwa na viongozi wa juu.

Alieleza vikao vya chama hicho vinavyofanya maamuzi ni Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu, Kamati Kuu inayoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa na Kamati Maalum ya Zanzibar inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

Katika vikao vyote hivyo, alisema yeye ni mmoja wa wajumbe na taarifa zote zinazotokana na vikao hivyo zinapaswa kutolewa na yeye, lakini kuhusu suala hilo hakusikia na halipo kwenye utaratibu wake.

“Nimelisoma kwenye mitandao kama ninyi mlivyosoma. Mimi ndiye Katibu Mwenezi wa CCM, ndiyo msemaji wa CCM, kwa hiyo vikao vyote vya CCM vikimaliza mimi ndiye napaswa kusema, kwa hiyo hilo halipo katika utaratibu wangu,” alisema Makala.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa alichokisema Dk Dimwa) ni wazo ambalo hata hivyo halijafikishwa katika vikao vikubwa na halikupaswa kuwekwa wazi.

Lakini, msisitizo wa maelezo yake umejikita katika hoja kuwa, bajeti ya mwaka ujao wa fedha, pamoja na mambo mengine fedha imetengwa kwa ajili ya kugharimia chaguzi na hivyo uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa.

“Tumeongelea bajeti hapa, tumeweka hela ya uchaguzi wa mitaa, tumeweka hela ya uchaguzi mkuu, uchaguzi upo kama kawaida,” alisisitiza.

Related Posts