Dar City inavyorejea BDL | Mwanaspoti

WAKATI baadhi ya timu za kikapu za Mkoa wa Dar es Salaam zikiwa kwenye mapumziko ya Ligi ya Kikapu mkoani humo (BDL) ili kupisha mashindano ya Kombe la taifa, timu ya Dar City inaendelea na mazoezi katika uwanja  wa Osterbay kujifua kwa ajili ya mzunguko wa pili.

Dar City ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) hadi mzunguko wa kwanza unamalizika  ilikuwa inaongoza kwa pointi 29.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Mohammed Mbwana ameliambia Mwanaspoti kuwa wamejipanga kutumia nafasi ya mapumziko hayo kurekebisha makosa ya wachezaji.

“Kwa kweli ingekuwa ni jambo la ajabu kwangu kutoa mapumziko kwa mchezaji ikizingatiwa tuna mashindano magumu  ya mzunguko wa pili,” alisema Mbwana.

Akizungumzia mzunguko huo  wa pili alisema katika   michezo yote watakayocheza wataichukulia kama fainali.

“Najua katika mzunguko wa pili timu zote zitaingia uwanjani na nguvu mpya. Kwa upande wetu tumejipanga kukabiliana na hilo.”

Mzunguko wa pili wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam unatarajia kuanza Julai 6, mwaka huu.

Related Posts