Pangani. Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mussa Kilakala ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani humo kufuatilia mashine za kukusanya ushuru maarufu kama ‘Pos’ ambazo zimezimwa wakati zinaonekana zimekusanya fedha za halmashauri, ili wahusika wachukuliwe hatua.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya Serikali juu ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa miezi sita wilayani Pangani, leo Jumatatu Juni 24,2024 mkuu huyo wa wilaya amesema kuna Pos za kukusanyia ushuru inaonekana zimezimwa kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, huku zikionyesha zimekusanya fedha, hivyo Takukuru wafuatilie na kupata taarifa za Pos hizo.
Ameagiza kuwa kwa watumishi wote watakaobainika wamefanya hivyo kwa makusudi, sheria zichukuliwe na hatua kali dhidi yao, kwani bado mapato ya halmashauri si ya kuridhisha hivyo lazima kulindwa ili kwenda kutimiza malengo.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa Serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, huku wananchi wakitoa kodi zao, hivyo lazima fedha hizo kulindwa na kupelekwa sehemu zote husika na malengo kutimia.
“Mtu wetu wa Takukuru utusaidie hao wanaofanya hivyo hatua kali za kisheria zichukuliwe, tunahitaji mapato katika Pangani yetu, hatuhitaji watu watuchezee, fedha kweli tunazo kidogo, lakini tusidokoe ili tufanye miradi ya maendeleo,” amesema DC Kilakala.
Akijibu hoja hiyo, mweka hazina wa halmashauri ya wilaya Pangani, Salimu Lugalo amesema ni kweli kuna Pos zinaonekana zimezimwa, ila tayari wameandaa kikao kwa ajili ya kuwaita wote waliopewa Pos hizo kuja kujieleza.
Amesema licha ya agizo hilo la mkuu wa wilaya, ila zipo sababu zinasababisha kuzima kwa Pos hizo, ikiwemo kuzima chaji, kuwa nje ya mtandao na changamoto nyingine, lakini wanafanyia kazi taarifa hiyo na watatoa mrejesho.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilaya ya Pangani, Zozima Shayo amekiri kuwepo kwa taarifa hizo na wamekuwa wakizifanyia kazi na wao pia wamebaini uwepo wa Pos zilizozimwa na wameanza kuchukua hatua.
Amesema tayari baadhi ya watumishi wamefikishwa mahakamani kutokana na Pos zao kutofanya kazi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Selemani Sankwa amesema katika ziara zao za kichama wamebaini kuna baadhi ya mapungufu ya kiutendaji, hasa kwenye matumizi ya pesa na kuwaomba watumishi wa Serikali kuzingatia miongozo na kanuni za matumizi ya fedha.
Halmashauri ya wilaya ya Pangani katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 imefanikiwa kupata hati safi ambayo inakuwa ni mwaka wa sita mfululizo kupata hati hiyo safi.