Dereva wa aliyekuwa RAS K’manjaro azikwa, viongozi wa dini wakemea mauaji ya albino

Moshi. Wakati dereva wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa kilimanjaro, Alphonce Edson (54) akizikwa katika makaburi ya familia, Mchungaji Thobias Msekwa ametumia nafasi hiyo kukemea vitendo vya kikatili katika jamii, ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino na kuitaka Serikali kutowafumbia macho wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Mchungaji huyo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Lowiri, Dayosisi ya Kaskazini, amesema hakuna utajiri unaopatikana kwenye viungo vya binadamu na badala yake watu wafanye kazi zinazowaingizia kipato kwa njia halali bila kukatisha uhai wa maisha ya wengine.

Ameyasema hayo leo Jumatatu, Juni 24, 2024, wakati wa ibada ya maziko ya dereva huyo yaliyofanyika katika makaburi ya familia nyumbani kwake, Kahe, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Edson na Katibu Tawala huyo (RAS), Tixon Nzunda aliyezikwa Juni 22, 2024 mkoani Songwe, walifariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Juni 18, saa 8:30 mchana, eneo la Njia panda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.

Akihubri katika ibada hiyo, Mchungaji Msekwa amesema dunia ya leo watu wameweka imani kuwa, wakiwa na viungo vya binadamu watapata utajiri, jambo ambalo wamedanganywa.

“Diniani leo ukatili umezidi ndani ya jamii zetu, wengine wamediriki kuamini kwamba wanapokuwa wamepata viungo vya binadamu wanakwenda kuwa matajiri, juzi tumesikia habari ya yule mtoto mwenye ualbino Kagera (Asimwe) amefanyiwa ukatili mbaya sana na baba yake akihusishwa, wakidai wanahitaji utajiri, ndugu zangu tunadanganywa, utajiri hauwezi kuja kama haufanyi kazi.”

Ameongeza kuwa; “Utajiri unakuja kwa mtu kufanya kazi kwa bidii na si katika hali ya kutafuta watu na kuua, hapana. Ninaona Serikali yetu inapiga kelele katika hilo na naomba mkuu wa mkoa, Mungu akusaidie kupambana nalo mkoani kwetu na hata nje ya mkoa wetu.”

Amesema mauaji kwa watu wenye ualbino yamekuwa tishio na kuwafanya kuishi kwa wasiwasi bila kujua hatima yao ya kesho.

“Jambo hili limekuwa tishio kwa hawa ndugu zetu wenye ualbino, hawajui kama kesho kutakucha, wanawindwa kama wanyama, huruma haipo, tunaenda mbingu ipi?” amehoji.

Aidha, mchungaji huyo ameonya wananchi kuacha kuishi maisha ya kiburi na kunyanyua mabega na badala yake wote kuishi maisha ya upendo na unyenyekevu wakitambua maisha ya hapa duniani ni mafupi.

“Leo watu wengi wanaishi kwa kiburi, kimabavu, wanatembea wamepandisha mabega utadhani wanapaa, kama dunia hii ni yao,  hata akionywa kwa jambo fulani hasikii, ndugu zangu wapendwa, dunia hii ya leo tunapaswa kuishi katika hali ya unyenyekevu na tukimuomba Mungu atusaidie tukijua muda wowote tunaweza kuondoka duniani hapa,” amesema mchungaji huo.

Akisoma historia ya marehemu, mtoto  wa marehemu, Aswile Alphonce amesema wamepoteza kiungo muhimu katika familia na kuishukuru Serikali kwa jinsi ilivyobeba msiba huo.

“Tumeumia kwa kumpoteza baba ambaye alikuwa kiungo muhimu kwa familia, lakini tunaishukuru Serikali chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na mkuu wa wilaya hiyo  kwa jinsi ilivyotukimbilia tangu tukio la msiba lilipotokea, tunajua familia tumepoteza na ninyi mmepoteza mtumishi, hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuwaombea kwa Mungu.”

Marehemu Alphonce ameacha mke, watoto sita na wajukuu wanne.

Related Posts