YANGA sasa iko mezani na menejimenti ya kipa Djigui Diarra, ili kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja ili aendelee kuitumikia, licha ya kuwa amebakiza msimu mmoja kabla ya mkataba wa sasa kumalizika.
Kipa huyo raia wa Mali alisaini mkataba wa miaka mitatu na Yanga unaomalizika mwishoni mwa msimu ujao akiwa na rekodi ya kufanya vizuri katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa akiiwezesha Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na msimu uliomalizika ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kupita zaidi ya miaka 20.
Mabosi wa Yanga wamekaa mezani na kipa huyo aliyeng’ara katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 iliyofanyika mapema mwaka huu huko Ivory Coast, ili kumuongezea mkataba huo mpya kupunguza presha ya alionao utakapomalizika mwakani.
Hata hivyo, pande hizo mbili kati ya Yanga na uongozi wa mchezaji huyo unaonekana bado haujafikia makubuliano kwani bado Diarra hajasaini mkataba huo ikielezwa anataka kuongezewa masilahi apewayo kwa sasa.
Meneja wa kipa huyo, Djally Tchumbi aliliambia Mwanaspoti kuwa, Yanga bado inataka kubaki kwa muda mrefu na kipa huyo na sasa wako katika mazungumzo yanayoelekea mwisho na mambo yakijiseti Diarra atasaini kwani bado hata yeye anapenda kuendelea kuitumikia.
“Unajua Djigui Diaraa amekuwa na miaka mitatu bora ya mafanikio, uongozi wa klabu yake nao umeyaona hayo ndio maana sasa tuko mezani wakitaka kumuongeza mkataba zaidi,” alisema Thumbi na kuongeza;
“Hatujafika mwisho, japo tunaelekea mwishoni kama tukikubaliana kabisa atakavyorudi kutoka mapumziko atasaini mkataba wa mwaka mmoja, mchezaji wangu ana furaha na klabu hiyo ingawa kuna mahitaji ya klabu zingine, lakini tumeona tuitangulize Yanga kwa sasa kwa kuwa bado ana mkataba wa mwaka zaidi.”
Katika hatua nyingine usajili wa beki wa kati, Bakari Mwamnyeto bado inaendelea kuchakatwa mezani kwa meneja wa nahodha huyo wa Yanga, Carlos Sylivester kusema wazi anataka mteja wake anufaike na maslahi mazuri kwa timu yoyote inayohitaji huduma yake muhimu kwake apate nafsi ya kucheza.
Mwamnyeto alijiunga na Yanga 2020/21 akitokea Coastal Union na mkataba alionao umeisha msimu uliomalizika hivi karibuni, hivyo amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali ndani na nje, japo inaelezwa Yanga imepewa kipaumbele kwanza iwapo itatekeleza masharti aliyotoa kubaki kikosini.
Timu zinazotajwa kumpa ofa Mwamnyeto, imo Yanga, Simba na Far Rabat ya Morocco na yoyote kati ya hizo ikifikia muafaka naye atajiunga nayo kwa ajili ujao wa mashindano.
Ili kujua ukweli juu ya Mwamnyeto atacheza wapi msimu ujao, Mwanaspoti lilimtafuta Meneja anayemsimamia, Carlos Sylivester aliyekiri jamaa bado hajasaini na mambo yakienda sawa anaweza akajiunga na mojawapo kati ya timu anazohusishwa nazo.
“Soka ni kazi ya mchezaji, ndio maana tumepata muda wa kuzichambua tuone ni ipi itamfaa, kama unavyojua usajili ulivyo lolote linaweza likatokea,” alisema Carlos.
Mwamnyeto akiwa nahodha Yanga, alifanikiwa kunyakua mataji ya Ligi Kuu mara tatu mfululizo, yakiwemo na makombe ya FA.
Kiwango alichokionyesha akiwa na Yanga, kimemuibua aliyekuwa beki wa timu hiyo na Simba, Amir Maftah aliyemuona bado ana uwezo wa kucheza ndani na nje kwa mafanikio makubwa.
“Kiwango cha Mwamnyeto bado ni kizuri, anaweza akacheza Simba, Yanga, Azam na akapata timu za nje na kama anaweza akaenda kujaribu nje kwanza,”alisema Maftah.