Gharama tiba za saratani, umaskini vinavyochangia vifo-2

Dar es Salaam. Wakati Sera ya Afya ya mwaka 2007 ikielekeza matibabu ya saratani ni bure, wagonjwa wanaofika Taasisi ya Saratani Ocean Road (Orci), hukumbana na bili kubwa za tiba.

Si hayo pekee, pia wagonjwa na wasaidizi wao wanaokosa mahali pa kukaa wakiendelea na matibabu hali inayowaongezea gharama za maisha kwa kuwa wapo wanaoandikiwa tiba-mionzi na wataalamu wanalazimika kusubiri muda mrefu kupata tiba kutokana na upungufu wa mashine.

Gharama huongezeka zaidi kutokana na kukosekana makazi ‘hosteli’ ya wagonjwa wanaosubiri tiba-mionzi na ndugu wanaowauguza.

Kukosekana hosteli ni changamoto kwa wenye kipato na wasionacho, wenye bima za afya na wasionazo ambao hulazimika kusubiri kwa zaidi ya wiki sita na hata miezi mitatu kwa wengine ili kupata huduma.

Hali ya kusubiri huwalazimu madaktari kuwaanzishia tiba za awali wagonjwa, ambao baadhi wameieleza Mwananchi walianzishiwa tiba-kemikali ‘chemotherapy’ hali inayowaingiza katika gharama mara mbili zaidi.

Tiba-kemikali inaanzia Sh40,000 hadi Sh10 milioni kwa mzunguko mmoja, mgonjwa akihitaji mizunguko kuanzia 12 na kuendelea ikitegemea aina ya saratani na dozi aliyoandikiwa mgonjwa. Gharama hizo huambatana na za vipimo kila wiki.

Gharama hizo kwa wagonjwa ni kinyume cha Sera ya Afya ya mwaka 2007 kifungu cha msamaha wa uchangiaji gharama huduma za afya kwa makundi maalumu 1.1.1.3.

Kifungu hicho kinaeleza Serikali inatambua kuwepo kwa wananchi wasio na uwezo wa kuchangia gharama za huduma za afya, ikiwa ni pamoja na wenye magonjwa sugu kama saratani.

“Serikali itaboresha, itaandaa na kusimamia sheria, kanuni na miongozo ya uchangiaji gharama za huduma za afya ikiwamo msamaha kwa makundi maalumu. Serikali itahakikisha kuna uwiano katika kutoa huduma za afya kwa makundi yote. Serikali kwa kushirikiana na wadau itaandaa utaratibu mzuri wa namna ya kuyahudumia makundi maalumu yanayostahili msamaha,” linaeleza tamko la sera hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaelekeza baadhi ya huduma zitatolewa kwa msamaha kwa wagonjwa ambao hawana uwezo.

“Hakuna kipengele kwamba huduma zitatolewa bila malipo (bure). Sera imeanisha misamaha kwa magonjwa na makundi mbalimbali maalumu kwa ambao hawana uwezo ikiwamo wanaougua kisukari, moyo, saratani n.k. Kwenye upande wa saratani, wagonjwa wanapata msamaha kwa wale ambao hawana uwezo,” amesema Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Afya, Englibert Kayombo.

“Hivyo sera inatekelezwa ipasavyo kwa wagonjwa kuchangia gharama kidogo na wasiokuwa na uwezo hupata msamaha wa matibabu kupitia ofisi ya ustawi wa jamii.” Kayombo amesema Taasisi ya Saratani Ocean Road imeweka kiwango kidogo cha uchangiaji ikieleza wagonjwa huchangia Sh5,000 kwa siku kwa kulazwa wodini na kupata milo yote mitatu ikiwa ni asilimia 12.5 ya gharama halisi.

“Gharama nyingi ambazo Taasisi ya Saratani Ocean Road wameziweka ni pungufu kuliko hata gharama za kumwona daktari, vipimo maabara na radiolojia katika hospitali za mikoa. Hivyo, kwa wagonjwa ambao hawana uwezo wanapatiwa msamaha kwa utaratibu wa kiserikali kupitia ofisi za ustawi wa jamii,” amesema.

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanyika kwa takribani miezi mitatu umebaini gharama za matibabu ya saratani mgonjwa analipia, huku matibabu ya mionzi pekee ndiyo yanatolewa bure, hata hivyo huambatana na gharama kadhaa za vipimo vya awali kabla ya kuanza tiba na vipimo vya kabla ya kila mzunguko wa tiba-mionzi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Lucas Kiyeji amesema katika utaratibu wa matibabu, gharama hazifanani lakini hutegemea pia aina ya saratani.

Amesema mgonjwa mwingine hupata tiba-kemikali mara moja na kulipa Sh40,000 na mwingine mzunguko mmoja analipa takribani Sh10 milioni.

“Kama ana saratani ya shingo ya kizazi anapata mionzi na kemikali, kuna wakati kila wiki anachoma kemikali Sh40,000, lakini kwa mfano mtu ana saratani ya titi ipo hatua ya nne ina baadhi ya vitu vya kuhakikisha vinaondolewa anachoma mpaka dawa za Sh10 milioni kwa mzunguko mmoja,” amesema.

Dk Kiyeji amesema mojawapo ya vipimo vya msingi vinavyofanyika ni CT-Scan.

“Hii ni muhimu, inafikia Sh200,000 hadi Sh300,000 inategemea na saratani aliyonayo kama ni shingoni, kifuani au tumboni itapima kulingana na ugonjwa ulipo na kuwekwa saratani iko wapi ili mnapotoa mionzi iende pale. Mionzi inagharimu Sh50,000 kisha ndipo anaenda kupata tiba,” amesema.

Imebainiki baadhi ya ndugu wanaouguza wagonjwa au wagonjwa wanaosubiri dozi hutembea kwa miguu kila siku kutoka hospitalini hapo hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili jengo la nje kwenda kulala.

Kutokana na gharama kubwa za matibabu, Hellen Chamafwa (36), amesema alikimbiwa na mchumba wake, hivyo aliuza kila kitu kufanikisha tiba ya saratani ya matiti.

Hellen amesema familia haina uwezo naye ndiye alikuwa tegemeo, hivyo aliuza samani za ndani na viwanja vyake viwili jijini Arusha mwaka 2018 na kuja kupata tiba Ocean Road.

“Nilianza kuona ishara, nilihisi kifua kizito, hali hii ilinitokea kwa muda mrefu karibu miaka sita. Sijawahi kuzaa wala kunyonyesha, hivyo nilivyoanza kuumwa mchumba niliyekuwa naye alinikimbia,” amesema.

Ingawa amepona, Hellen aliyekuwa akifanya kazi katika moja ya hoteli za kitalii jijini Arusha amesema ametumia zaidi ya Sh14.8 milioni kujitibu kwa tiba-kemikali na dawa, ikiwamo mionzi hivyo amebaki hana mali.

Ametoa wito kwa Serikali kuangalia namna ya kupunguza gharama kwa wagonjwa.

Amesema gharama huchangia vifo vinavyoweza kuepukika, kwa kuwa ndugu wa wagonjwa huwaondoa hospitalini kwa kukosa fedha za matibabu na za kujikimu wanapouguza.

“Mama yangu mkubwa alipelekwa Ocean Road baada ya kugundulika ana saratani ya shingo ya kizazi, tulipofika walisema ugonjwa upo hatua ya juu, aliandikiwa mionzi. Hata hivyo, aliambiwa angeanza kupewa miezi miwili mbele, ilibidi turudi nyumbani kwanza,” anasema Frank Mbwilo, mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya.

“Hali iliendelea kubadilika tukimtibu hospitali za kawaida baadaye alifariki dunia wiki tatu kabla ya tarehe ya kuanza tiba-mionzi,” amesema Mbwilo.

Mbwilo ni miongoni mwa wananchi kadhaa waliopoteza ndugu zao kutokana na changamoto ya upungufu wa vifaatiba kutibu saratani, zikiwamo mashine za mionzi, kama anavyosimulia Alfred Lyimo, mkazi wa Kilimanjaro.

“Kaka yangu alipata saratani ya njia ya chakula. Ilikuwa Mei 2023, iligundulika katika hatua ya juu. Baada ya kufika Ocean Road aliandikiwa mionzi lakini tuliambiwa tusubiri,” amesema Mbwilo.

Ameeleza daktari alishauri aanze tiba-kemikali wakati akisubiri foleni ya mionzi, alianza na baadaye walishindwa kutokana na mgonjwa kupata athari hasi ya tiba hiyo na ongezeko la gharama, hivyo walirudi Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Tulifanya uamuzi wa kurudi bila kumshirikisha daktari kwa sababu hatukuwa na fedha hata za chakula. Alikaa wiki moja na nusu akafariki dunia, lakini tunaamini kama mashine zingekuwepo za kutosha huenda ndugu yetu angalikua hai,” amesema Mbwilo.

Mtaalamu wa utambuzi na matibabu ya saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Beda Likonda amesema changamoto ya gharama imewafanya Watanzania wengi kuondoka bila kushauriana na daktari na kwenda kwenye tiba mbadala au kuishia nyumbani.

Amesema wamekuwa wakiwafuatilia, baadhi wakishindwa kuwapata.

“Gharama ndiyo chanzo, pia Watanzania wengi hawaji kwenye mionzi, wengi wana hofu. Wakisikia neno mionzi wapo wanaokwenda kujifungia nyumbani,” amesema.

Msemaji wa Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro, Gabriel Chiseo amesema wagonjwa wengi hawawezi kukaa muda mrefu hospitalini kwa sababu ya gharama, hivyo akipata tiba-kemikali mbili au tatu anaondoka kwenda nyumbani.

“Ili kupambana na hali hiyo, KCMC tumejenga hosteli wagonjwa watakuwa wanakaa hapa na tutaanzisha shule kwa watoto wanaougua saratani. Matibabu yao yanahitaji muda mrefu pia kutakuwa na sehemu ya kuishi ndugu wa wagonjwa,” amesema.

Chiseo amesema wamegundua kutokana na kukosa mashine ya mionzi, wanapotoa rufaa kwa wagonjwa kwenda Ocean Road wengi hawaendi kutokana na gharama, hivyo wameanza maandalizi ya kufunga mashine hiyo.

Amesema wagonjwa wengi hawana uwezo wa kulipia matibabu, akitoa mfano mwaka 2023 KCMC ilitumia Sh9 bilioni kutibu wagonjwa wa msamaha wa saratani.

“Hata kama utampa matibabu bure, ataishi au atakaa wapi na mwingine hajui atakula nini na anahitaji chakula kizuri chenye afya kulingana na dozi anazotumia. Tanzania bado umasikini ni changamoto na matibabu ya saratani yanagharimu fedha nyingi,” amesema Chiseo.

Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Hospitali ya Ocean Road, Islam Mposso amesema ni kweli sera inaelekeza matibabu yatolewe bure, lakini Serikali kupitia hospitali haiwezi kubeba mzigo wote moja kwa moja, ndiyo maana kuna utaratibu wa kuchangia huduma.

“Mgonjwa anatoa kidogo, Serikali inachangia. Utaratibu kama wananchi wanashindwa kupata huduma hapa kwetu tunawasaidia na wanatibiwa kupitia mfumo wa msamaha kwa kupunguziwa gharama, lakini wapo wanaolipia asilimia 20 au 50 na wale wasiolipa chochote,” amesema.

Mposso amesema kwa mwaka Ocean Road inatumia Sh40 bilioni kwa ajili ya msamaha kwa wagonjwa wasio na uwezo kwa kutumia vigezo maalumu vilivyowekwa na kitengo cha Ustawi wa Jamii.

Amesema gharama za dawa za saratani ni kubwa, zipo dawa za Sh5 milioni mpaka Sh10 milioni na kwamba wagonjwa wote wanauziwa kwa gharama ya chini.

Related Posts