Katika mechi iliyochezwa mjini Duesseldorf, Uhispania iliifunga Albania 1-0 na kukamilisha hatua ya makundi ya Euro 2024 kwa kushikilia nafasi ya kwanza ya kundi B, baada ya kushinda mechi zote tatu na kujikusanyia jumla ya alama 9.
Bao la Uhispania lilipachikwa nyavuni na winga wa timu ya Barcelona Ferran Torres katika dakika ya 13, na hivyo kuzima shauku ya mashabiki wa Albania waliokuwa wengi uwanjani hapo. Hata hivyo, mchezo huu haukuwa rahisi kwa timu ya Uhispania ambayo ilifanya mabadiliko makubwa ya wachezaji wake ukilinganisha na mechi yao dhidi ya Italia siku nne zilizopita na ambapo walijipatia pia ushindi wa 1-0.
Uhispania walikuwa tayari wamejihakikishia nafasi ya kwanza katika Kundi B, lakini Albania walijua wazi kwamba walihitaji ushindi ili kusonga mbele, jambo iliyoifanya mechi hiyo kuwa na mikikimiki haswa katika kipindi cha pili. Lakini licha ya juhudi zao, Albania wanarejea nyumbani baada ya kuambulia pointi moja tu na kumaliza mkiani mwa kundi hilo gumu.
Soma pia: Ujerumani yawa ya kwanza kufuzu duru ya mtoano
Ni mara ya kwanza tangu mwaka 2008 kwa Uhispania kushinda mechi zote tatu katika hatua ya makundi iwe kwenye Kombe la Dunia au michuano ya Euro. Kocha Luis de la Fuente sasa anajipanga kuelekeza nguvu zake zote kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora utakachezwa mjini Cologne siku ya Jumapili dhidi ya mshindi wa tatu ambaye bado hajafahamika.
Italia yailazimisha Croatia sare ya 1-1
Katika mechi nyengine ya kusisimua, Italia waliilazimisha katika dakika za mwisho Croatia sare ya 1-1 baada ya bao maridadi la Mattia Zaccagni. Italia wanasonga mbele katika hatua ya mtoano ya Euro wakishikilia nafasi ya pili na itamenyana na Uswisi katika hatua ya 16 bora, huku Croatia ikiwa katika hatihati ya kuondolewa lakini bado ina matumaini ya kusonga mbele na hii itategemea na matokeo katika mechi zingine baadaye wiki hii.
Wakiwa na pointi mbili pekee uwezekano ni mdogo kwa kikosi hicho cha Zlatko Dalic kufuzu kama moja ya timu nne bora zilizo nafasi ya tatu lakini bado inawezekana.
Luka Modric ambaye ana umri wa miaka 38, na siku 289, alipachika bao hilo dhidi ya Italia katika dakika ya 55, muda mchache tu baada ya kipa wa Italia Gianluigi Donnarumma kuzuia mkwaju wa penati.
Modric sasa anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye michuano ya Euro. Awali rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Ivica Vastic, ambaye alikuwa na miaka 38, na siku 257 alipoifungia Austria dhidi ya Poland kwenye michuano ya Euro mwaka 2008.
Soma pia: Shirika la reli la Ujerumani linanufaika kwa ongezeka la abiria katika kipindi hiki cha Euro 2024
Kufuatia matokeo ya jana, tayari England, Ufaransa na Uholanzi zimefanikiwa kufuzu katika hatua ya mtoano. Uingereza imefuzu kutoka Kundi C huku Ufaransa na Uholanzi wakisonga mbele kwenye Kundi D.
Lakini timu zote tatu zitacheza mechi zao za mwisho za hatua ya makundi siku ya Jumanne, ambapo zitajaribu kuwa miongoni mwa timu mbili bora ili kuziwezesha kukutana na timu ambazo wanadhani si tishio sana katika hatua ya 16 bora.
Leo Jumanne, Ufaransa watashuka dimbani na Poland huku Uholanzi wakipambana na Austria. Baadaye usiku, Denmark watachuana na Serbia huku England wakimenyana na Slovania. Mtanange wa kwanza kufahamika katika hatua ya 16 bora ni kati ya Uswisi ambao watachuana na Italia Jumamosi ya Juni 29.
(Vyanzo: Mashirika)