USHAWAHI kusikia ule mkasa wa wanandoa kupeana talaka na kuachana huku wakiwa bado wanapendana.
Kila mmoja humfuatilia mwenzake kimyakimya katika maisha mapya ya useja. KIu kubwa ni kutaka kujua anafanya nini na yupo na nani?
Wale wanaume wenye mioyo midogo, akisikia zilipendwa wake ametua kwa jamaa kwingine, wakati mwingine huleta za kuleta na kujizima data, kwa kumfanyia fujo mtalaka wake na hata kuleta maafa.
Hizi sio habari za kufikirika. Hutokea ndani ya jamii na mitaani tunakoishi.
Sasa stori kama hizi zimehamia kwenye soka la Tanzania baada ya Coastal Union, kuamua kumkomalia beki iliyomuuza Simba, Lameck Lawi.
Saa chache baada ya Simba kumtambulisha beki huyo chipukizi kuwa ni mali yao, Wagosi wa Kaya nao wakaibuka na kudai dili lilishakufa na Lawi ni mali halali ya Wana Mangushi.
Sababu za kuichomolea Simba kumbeba Lawi ni kitendo cha mabosi wa Simba kushindwa kutekeleza kwa usahihi makubaliano yao ya kuwaingizia fedha za malipo ya ununuzi wa mchezaji huu. Fasta ikaamua kurejesha fedha zilizoingizwa nje ya muda waliokubaliana kutaka kuthibitisha kwamba dili limekufa.
Hata hivyo, Simba nayo imejibu mapigo kwamba Wagosi ni kama wamevurugwa kwa ilichokifanya cha kudai walicheleweshewa fedha zao, wakati sitisho lao limekuja wakiwa wamemaliziwa fedha zote, hata kama walicheleweshewa kwani, hata Coastal ilikiuka kumpeleka kwa wakati Lawi akafanyiwe vipimo vya afya.
Ukisikilia pande zote zinavyozungumza na kutetea suala hilo la beki Lawi anayekipiga pia timu ya taifa, Taifa Stars, unagundua Coastal Union ni kama wamezingua.
Hata kama Simba ilicheleweshwa kuingiza fedha za malipo, lakini hiyo haiwezi kuvunja mkataba baina ya mchezaji na klabu iliyomnunulia na pia kuna taratibu za kutangaza kuvunja dili ililolikubali hapo awali.
Kinachoonekana wazi ni kwamba Coastal ilikubali kumuachia Lawi wakati bado inamhitaji na ilipotokea mwanya huo uliosababishwa na Simba wanaona wamepata pa kutokea.
Kitendo cha timu hiyo kutinga michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, Coastal waliona kama wamejizingua kumuacha Lawi kwenda Msimbazi, wakati wanahitaji huduma ya kuwabeba kimataifa.
Inawezekana kabisa, Coastal imetingisha kiberiti ili kuona kama kimejaa kwa kuukana usajili wa Lawi kwenda Simba, lakini inajua wazi beki huyo ni lazima atavaa uzi Mwekundu na Mweupe kama aliokuwa akiuvaa kwa Wagosi, ila safari hii ikiwa ni ule wa Msimbazi.
Kutaka kuonyesha kweli wao ni wakongwe wa soka nchini, wangempotezea Lawi na kumkolia Kennedy Juma aliyeachwa na Simba.
Na kama inaona vipi bado in nafasi ya kumrejesha kikosini, aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto anayekipiga Yanga ambaye ameshamaliza mkataba na klabu hiyo na bado hajasaini kokote.
Kennedy ni beki mzoefu wa michuano ya kimataifa kama ilivyo kwa Mwamnyeto, kwani amekuwa na Simba kwa misimu kadhaa sasa akiitumikia tangu 2019.
Licha ya mara kadhaa kuanzishwa benchi mbele ya nyota wengine waliokuwa wakikipiga Simba kuanzia enzi za Pascal Wawa, Joash Onyango na baadae Henock Inonga na Che Fondoh Malone, bado Kennedy alikuwa kiraka kinachofukia mashimo ya nyota tegemeo wanaokosekana uwanjani katika kikosi cha Simba.
Bahati nzuri anamudu kucheza na yeyote na wala usiona tofauti. Wakati Wawa alipokuwa ana dharura alikuwa akisimama na Onyango na ngome ya Simba ilikuwa freshi. Hata ilipotokea Onyango ana majanga alipangwa na Wawa na kumudu vizuri tu kuilinda Simba.
Hata hivi karibuni, wakati Inonga au Malone wakiwa na changamoto zilizowafanya wakosekane kikosini, bado jamaa alisimama imara ya yeyote kati ya hao na kukiwasha kama kawaida hadi juzi kati alipopewa mkono wa kwaheri, kitu kinachoweza kuwafanya Wagosi wamuwahi haraka kabla hatajua kokote.
Kama inaona Kennedy sio mapigo yao, bado kuna Mwamnyeto. Mtoto wa nyumbani kabisa ambaye licha ya kuwa nahodha wa Yanga kwa misimu mitatu mfululizo sasa, lakini mara kadhaa amekuwa akianzia benchi ili kuwapisha Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kulisongeza pale Jangwani.
Bahati nzuri, kwa sasa mkataba wake umemalizika na hivyo yupo huru kunaswa na klabu yoyote ikiwamo Coastal aliyowahi kuitumikia kwa uaminifu mkubwa kabla ya kusajiliwa na Yanga mwaka 2020.
Miaka miwili akiitumikia timu hiyo na ukichanganya na mingine minne akiwa na Yanga aliyofika nayo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 na kuifikisha Yanga makundi na kuishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25 ilipocheza mara ya kwanza na mwisho 1998 ni sababu tosha ya Coastal kuachana na Lawi kiroho safi na kuwekeza nguvu kumvuta ili kumrejesha Mwamnyeto.
Kama inawaona Kennedy na Mwamnyeto sio taipu yao na hawana uwezo wa kuwamudu kuwalipa, kuna nyota kadhaa wengine wazoefu wa michuano ya kimataifa wanaoweza kuwasajili na kuwabeba katika Kombe la Shirikisho Afrika itakalocheza kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipobadilishwa mwaka 2004.
Wagosi wanajua ni kweli mara ya mwisho kucheza mechi za kimataifa ilikuwa 1989 iliposhiriki Kombe la Washindi, lakini wakimpata mtu kama Daniel Amoah au Malickou Ndoye waliotemwa Azam watawafaa.
Pia Wagosi lazima watambue kuwa, sio nafasi moja tu ya Lawi inayoweza kuwapa heshima CAF, italazimika kuijenga timu katika kila eneo.
Kwa upande wa kipa, hapo haina tatizo, kwani Ley Matampi ameonyesha uzoefu wake ulivyo muhimu kwa kuibeba Coastal hadi kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara akiwa na clean sheet 19 akimzidi hadi Kipa Bora wa misimu miwili iliyopita, Diarra Djigui wa Yanga.
Tayari inadaiwa imemnasa Djuma Shaban aliyekuwa hana timu tangu atemwe na Yanga na kukimbilia Azam ambapo dili lilikuwa kimyakimya. Huyu atawafaa kwa uzoefu alionao. Amefanya makubwa akiwa na AS Vita na hata akiwa Yanga ndiye aliyefunga bao pekee lililoipa timu hiyo ushindi katika mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita mbele ya USM Alger ya Algelia. Kama Yanga ingekuwa imetoka sare nyumbani badala ya kulazwa 2-1, ingetangaza ubingwa Uarabani na kuandika historia kubwa.
Mabosi wa Coastal waharakishe kusajili mashine nyingine kali kwa eneo la kiungo, kwani licha ya kuwa na vifaa vilivyoibeba katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho msimu uliomalizika hivi karibuni kwa kufika nusu fainali, bado inahitaji mashine za maana zenye uzoefu ili kuwabeba mbele ya wapinzani watakaokutana CAF.
Hata eneo la ushambuliaji, Coastal inahitaji watu wa maana na sio kina Ibrahim Ajibu au Hija Ugando, kwani basi yao inaweza isiwe na faida mbele ya majabari watakaokutana nao kwenye mechi nne za awali za Kombe la Shirikisho kabla ya kuifukizia makundi itakayokuwa na mechi sita ndipo iingie katika mechi za mtoano za hatua za robo fainali, nusu fainali na hata fainali yenyewe kuwania taji inayolishikilia Zamalek ya Misri.
Coastal ikiamua kufanya maamuzi ya kufunga ukurasa wa Lameck Lawi na kuanza kujipanga kwa maisha mapya bila ya beki huyo ni wazi kila kitu kitakuwa sawa na sio ajabu watakuja kujisifia kwa uamuzi iliyofanya kwa kumuuza na kuingia Sh 100 milioni.
Vinginevyo itafanya zile stori za kuachana mke huku bado unampenda ikaja ikawagharimu kwa Lawi, kwani tayari akili na mwili ulishajiandaa kutumika Msimbazi. Kazi kwenu Wanamangushi!