Dodoma. Wakati uongozi mpya wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), ukitarajiwa kupatikana kesho, kazi kubwa inayowasubiri ni kupigania marekebisho ya sheria, sera, kanuni ili kuondoa mianya iliyokuwa ikiwafanya wasitimize wajibu wao vizuri.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 24, 2024, Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Tanzania Bara, Beatrice Mayao amesema yapo mengi yaliyofanywa na uongozi uliopita, lakini yapo mengi ambayo yalikuwa ni matarajio ya Serikali hayakufanyika kwa wakati.
Hata hivyo, amesema ni matarajio ya Serikali kuwa mambo hayo yataweza kufanywa na uongozi huo mpya ambao hukaa madarakani kwa miaka mitatu.
“Kama unavyofahamu sheria na baadhi ya kanuni zao (mashirika yasiyo ya kiserikali) zimepitwa na wakati, lakini uongozi uliopita haukuweza kufanyia kazi hiyo. Matarajio yetu na viongozi watakaochaguliwa hivi sasa wataona umuhimu wa kurekebisha na kuishauri Serikali namna bora ya kuweza kuendesha misingi ya uwazi na uwajibikaji hasa kwenye mashirika haya,”amesema.
Amesema wanatarajia kwa mashirika hayo hasa kwenye uongozi wa juu wa NaCoNGO kuweka uwazi na uwajibikaji.
Beatrice amesema Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni mwaka 2002, Sera ya Mwaka 2001 na kanuni zipo za mwaka 2006.
“Hakuna changamoto kubwa katika utekelezaji wa sheria, lakini zipo katika kanuni kuna gaps (mianya), mbalimbali ambazo wao wenyewe wameziibu, hivyo watafikisha katika hatua nzuri ya kuhakikisha wanazifanyia kazi. Serikali ni sikivu itapokea maoni ya wadau na kuyafanyia kazi,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya NaCoNGO, Christina Ruhinda, amesema mchakato wa kupokea maombi ya wagombea kwenye uchaguzi huo yaliyoanza Juni 17 hadi Juni 19, 2024 umekamilika.
“Baada ya hapo ni kuangalia fomu zilizokuja kama zimekidhi vigezo ama la. Sasa kinachofanyika ni kuandaa orodha ya waombaji waliokidhi vigezo kwa ajili ya uchaguzi kesho,”amesema.
Amesema baada ya kukutana kwa siku tatu kwenye mafunzo hayo, wamefahamiana, kuzungumza pamoja na hivyo wataweza kufanya uamuzi sahihi kwenye uchaguzi huo.
Naye Mratibu wa wa mafunzo hayo, Ntimi Charles amesema wajumbe wa baraza hilo wana wajibu wa kuunganisha NGOs na Serikali pamoja na wadau wengine na kuhimiza NGOs kutimiza sheria.
Wajumbe hao waliochaguliwa Juni 11, 2024, kesho watawachagua viongozi mbalimbali wakiwemo mwenyekiti, katibu mkuu, mweka hazina wa baraza hilo.