Dodoma. Serikali imesitisha kazi ya ukaguzi wa risiti za kielektroniki (EFD) na ritani za kodi iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia mkoa wa kikodi wa Kariakoo, Jijini Dar es Salaam, wakati ukiandaliwa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo.
Uamuzi huo umekuja baada ya kikao kilichowashirikisha wafanyabiashara nchini wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Khamis Livembe na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martine Mbwana.
Kwa upande wa Serikali kikao hicho kiliwashirikisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima.
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sajini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi.
Akitoa maazimio ya kikao hicho, Profesa Kitila amesema walikutana na wafanyabiashara hao, ili kujadili changamoto zilizochangia kufunga maduka yao.
Amesema katika kikao hicho walionyesha changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa nyaraka, hususani bandarini ambako kunasababisha makadirio ya kodi yasiyo sahihi na ukokotoaji wa kiwango cha kodi ambacho wanalipa.
Ametaja changamoto nyingine ni uwepo wa wafanyabiashara ndogo ndogo ‘machinga’ katika maduka wanayouza, suala la kamatakamata ambalo limekuwa likiendeshwa na TRA.
Profesa Kitilia amesema pia wafanyabiashara hao waliainisha changamoto katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024.
Amesema baada ya majadiliano ya kina wamekubaliana kuanzia Julai mosi mwaka 2024, TRA itakuwa na mfumo mpya wa nyaraka ambao utatumika vizuri zaidi katika kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanapata makadirio sahihi kwa maana ya mfumo stakabadhi pamoja na risiti yake.
“TRA inasitisha operesheni zake maarufu kamata mpaka ikamilishe utaratibu huu, baada ya kuweka mfumo mzuri zaidi wa kukusanya mapato, hususan katika suala zima la upatikanaji wa nyaraka kwa hiyo linasitishwa wakati wanatengeneza mfumo wao huo wa nyaraka,” amesema.
Aidha, amesema suala la ukokotoaji wa kodi ni la kisheria na kwamba wamelichukua na wataendelea kuliangalia, ili kuboresha zaidi mfumo wa ukokotoaji, hususan katika makadirio pale bandarini.
“Suala lingine ni kuendelea kuwapanga machinga kama ambavyo Serikali iliagiza, ili wakae katika maeneo sahihi ambayo haingilii biashara za wenye maduka, ili kila mtu aweze kunufaika. Wenye maduka wafanye biashara, pia machinga wafanye biashara,” amesema.
Amesema cha muhimu ni kila mtu anayefanya biashara eneo la Kariakoo aweze kulipa kodi na uwiano ambao unakubalika.
Kuhusu changamoto ya muswada, Profesa Kitila amesema wamewataarifu wafanyabiashara hao kuwa Muswada wa Sheria ya Fedha kwa Mwaka 2024 haujapitishwa, kwani sasa uko katika majadiliano bungeni.
Amesema pia wamewataarifu wafanyabiashara hao kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeita wananchi wote kutoa maoni yao, hivyo wanawaalika kupeleka maoni yao katika kamati hiyo na wabunge watazingatia maoni yao kabla ya sheria hiyo kupitishwa.
“Kamati ya Waziri Mkuu na mikutano iliyofanyika iliibua changamoto 41 ambazo zinawakabili wafanyabiashara wa Kariakoo na maeneo mengine na katika hizi changamoto 35 zinahusu mambo ya utendaji, hayahusu mambo ya sheria wala sera. Changamoto sita zinahusu sheria pamoja na sera mbalimbali,” amesema.
Amesema changamoto zote zinaendelea kufanyiwa kazi na kwamba wafanyabiashara pamoja na viongozi wao watapata nafasi ya kupitishwa kwenye changamoto moja hadi nyingine.
“Mfano wake ni ile walitaka tuanze kutambua bidhaa nane kama mfano wa kuweza kukokotoa kodi ambayo Serikali imekubali na bidhaa zimeshatambuliwa na wenzetu wa TRA wataanza kuzitekeleza,” amesema.
Amesema Serikali inafanyia kazi changamoto hizo zote za kisheria na kiutendaji.
Profesa Kitila amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara Tanzania na kuwa nafasi ya Kariakoo katika biashara za nchini wanaendelea kuitambua.
“TRA wameelekezwa waendelee kuwa karibu na wafanyabiashara na TRA waendelee kulinda hadhi ya Kariakoo kama kitovu muhimu cha biashara hapa Tanzania. Na sisi kama Serikali tutaendelea katika muktadha huo,” amesema.
Amesema Serikali wamekubaliana kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu na kuboresha mawasiliano, hususani kati viongozi wa TRA na wafanyabiashara.
Amesema kwa upande wa Serikali panapokuwa na changamoto ya sheria na sera watakuwa wepesi kushughulikia, ili kuhakikisha kunakuwa na mahusiano mazuri, ili wafanyabiashara walipe kodi wakiwa na furaha na wao wahudumie wananchi kupitia kodi zao wakiwa na furaha.