Mpanda. Kutokana na malalamiko ya wafanyabiashara wa zao la mahindi katika Manispaa ya Mpanda kuhusu mahitaji ya soko la kisasa, Serikali imeanza mchakato wa ujenzi wa soko kupitia mradi wa Tactic.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Juni 24, 2024, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Sophia Kumbuli amesema tayari andiko la mradi wa soko hilo limeandikwa na kuwasilisha Wizara ya Kilimo, ili kupata fedha za ujenzi wa soko la kisasa.
Imeelezwa soko hilo litawasaidia wafanyabiashara wa mahindi na mazao mengine yanayozalishwa mkoani Katavi.
Kumbuli amesema kutokana na umuhimu wa wafanyabiashara katika halmashauri hiyo na kwa kuzingatia fedha ambazo Serikali imewekeza katika kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa mazao umeongezeka na masoko yaliyopo sasa hayawezi kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Aidha, Kumbuli amesema halmashauri hiyo inatarajia kupata fedha kupitia mradi wa Tactic ambazo zitajenga soko kubwa la kisasa litakaloweza kuwaweka wafanyabiashara mbalimbali na kuondoa malalamiko hayo.
“Ni kweli kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wetu kuhusu masoko tuliyonayo hivi sasa kuwa madogo na kutokidhi mahitaji ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla,” amesema.
Amesema walichokifanya sasa ni kuomba fedha Wizara ya Kilimo na kupitia miradi ya Tactic inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na halmashauri hiyo imepata mradi huo wa soko la kisasa litakalojengwa eneo la Kwa Wajenzi.
Hivyo, Kumbuka amesema wanaamini wakimaliza ujenzi wa soko hilo watakuwa wamemaliza malalamiko ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Katibu wa soko la mahindi Manispaa ya Mpanda, Lucas Mchina, amesema kama Serikali itajenga soko jipya la kisasa, itakuwa imewasaidia kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, ameomba maeneo hayo yasitumike kwa malengo ya kisiasa, kwani ahadi nyingi zimekuwa zikitolewa bila utekelezaji.
Mchina amesema viongozi wa Serikali katika halmashauri hiyo wamekuwa wakiahidi, lakini hawatekelezi ahadi zao.
“Tunashukuru kama Serikali itatujengea soko la kisasa hapa Mpanda, tutakuza biashara zetu na kuvutia watu wengine kuja kununua mahindi hapa kwetu. Lakini kwa sasa viongozi wa Serikali hatuwaamini sana, maana wanatoa ahadi lakini hawazitekelezi. Tutawaamini tu pale tutakapoona ujenzi wa soko umeanza na kukamilika,” amesema Mchina.
Halima Hussein, mkazi wa Manispaa ya Mpanda, amesema kuwa masoko yaliyopo katika mkoa wa Katavi hayana mazingira mazuri.
Amesema kujengwa kwa soko la kisasa kutasaidia wananchi kupata huduma kwenye mazingira bora na kuepukana na magonjwa mbalimbali, hasa katika kipindi cha masika kama kipindupindu na magonjwa mengine.