KLABU ya Simba imeachana rasmi na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Msumbiji, Luis Jose Miquissone baada ya kutoridhishwa na kiwango chake tangu aliporejea ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi akitokea Al Ahly ya Misri.
Kwa mara ya kwanza Luis alijiunga na Simba Januari mwaka 2020 akitokea UD Songo ya Msumbiji kwa mkopo kutokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ambako alionyesha kiwango bora timu hizo zilipokutana katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hizo zilikutana katika raundi ya kwanza ambapo mechi ya awali iliyopigwa Msumbiji Agosti 10, 2019 zilitoka suluhu na Simba iliporejea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 25, 2019, zilitoka sare ya 1-1 na kutolewa kwa faida ya bao la ugenini.
Katika mchezo huo, Luis alifunga bao katika dakika ya 12 kisha Simba kuchomoa kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Erasto Nyoni katika dakika ya 87 na ndipo viongozi wa kikosi hicho cha Msimbazi wakavutiwa na huduma yake na kuamua kumbakisha hapa nchini.
Nyota huyu aliendelea kujitengenezea soko kwani katika mechi ya Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi iliyopigwa Februari 23, 2021, alifunga bao katika ushindi wa 1-0, dhidi ya Al Ahly kisha Simba kuchapwa 1-0 katika marudiano Misri, Aprili 9, 2021.
Kiwango hicho kiliwavutia mabosi wa Al Ahly waliomsajili Agosti 2021 kwa mkataba wa miaka minne ingawa mambo yalikwenda tofauti na kujikuta akitolewa kwa mkopo kwenda Abha Club inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia na kufeli pia.
Tangu arejee Simba Julai 22, 2023, kwa mara nyingine amefunga bao moja tu katika michuano ya Kombe la Shirikisho la FA hatua ya pili wakati Simba ikishinda mabao 4-0, dhidi ya Tembo FC ya Tabora, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Luis alifunga bao hilo katika dakika ya 11 huku mengine yakifungwa na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ katika dakika ya 31, Saleh Karabaka (dk81) na Pa Omar Jobe (dk83) na baada ya hapo nyota huyo hajafunga tena hadi anaondoka rasmi kikosini humo.
Katika Ligi Kuu Bara iliyomalizika, Luis amecheza jumla ya michezo 19, akiwa na kikosi hicho sawa na dakika 585 ambapo pia hajafunga bao lolote huku akipoteza imani hata kwa benchi la ufundi hivyo kurahisisha uamuzi wa viongozi kumtupia virago.
Rekodi hizo ni mbovu kwake tofauti na ilivyokuwa mwanzo kwani kabla ya kutimkia Misri, aliicheza Simba kwa misimu miwili jumla ya michezo 37 ya Ligi Kuu Bara na kuhusika katika mabao 25 ndani ya kikosi hicho baada ya kufunga mabao 12 na kuchangia mengine (asisti) 13.
Kwa upande wa Clatous Chama ambaye pia inaelezwa amejiunga na Yanga, amemaliza mkataba ndani ya timu hiyo baada ya kuitumikia kwa vipindi tofauti ambapo kwa mara ya kwanza alijiunga mwaka 2018, akitokea klabu ya Lusaka Dynamos ya kwao Zambia.
Kiwango kizuri alichokionyesha kilimuondoa Simba mwaka 2021 aliponasa dili la kujiunga na RS Berkane ya Morocco ingawa pia mambo yalikuwa magumu kwake na kurejea 2022 na kukikutumikia kikosi hicho kwa misimu miwili hadi anapohusishwa na Yanga.
Msimu wa kwanza kwake katika Ligi Kuu Bara baada ya kurejea alifunga mabao manne na msimu uliopita alifunga saba nyuma ya kiungo Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyemaliza kinara ndani ya kikosi hicho na mabao 11 japo ameachwa pia.
Rekodi ya kipekee kwa Chama katika Ligi ya Mabingwa Afrika, yupo katika wachezaji 10 bora wa michuano hiyo akifunga mabao 19 tangu ilipoanza mwaka 1964, akishika nafasi ya tisa sawa na nyota wa zamani wa Sudan na Klabu za Al Hilal na Al Merrikh, Bakri Almadin na Emmanuel Osei Kuffour.
Kati ya mabao hayo 19 aliyofunga, mabao 15 ameyafunga akiwa na Simba katika nyakati tofauti ambazo ameitumikia timu hiyo huku mengine manne akiyapachika wakati alipokuwa akichezea Zesco United ya Zambia.
Kuondoka kwa wachezaji hao, kunachangiwa na mambo mawili makubwa ambapo mojawapo ni kupunguza gharama za matumizi ndani ya timu hiyo.
Luis ni mchezaji aliyekuwa analipwa kiasi kikubwa ndani ya Simba ambapo inadaiwa alikuwa analipwa Dola 25,000 kwa mwezi takriban Sh65 milioni, huku Chama akilipwa Dola 20,000 ambayo ni Sh52 milioni zilizowafanya mabosi wa Simba kuwaondoa.
Mbali na mishahara mikubwa ila hata viwango vyao vimeshuka kwa kiasi kikubwa kwani moja ya malengo ya timu hiyo kwa sasa ni kutengeneza kikosi chenye vijana wenye uchu na mafanikio, baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo.
Mchezaji anayewafuatia kwa kulipwa kiasi kikubwa ni Fabrice Ngoma anayedaiwa kuvuta Sh18 milioni jambo linalowafanya mabosi wa Simba kupunguza gharama kubwa kwa nyota hao wawili kwanza ili kutengeneza uwiano wa kikosi cha msimu ujao.
Ukiachana na mishahara hiyo mikubwa pia katika klabu hiyo kuna wachezaji wanaolipwa hadi Sh2 milioni kikiwa ni kima cha chini zaidi.
Mbali na Luis aliyepewa mkono wa kwaheri, wachezaji wengine ni aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, John Bocco, Said Ntibazonkiza ‘Saido’, Shaaban Chilunda na Kennedy Juma huku Chama akidaiwa kuwa njiani kuondoka na kujiunga na watani zao wa jadi, Yanga.