Madina yupo tayari kwa vita Zambia

NYOTA wa timu ya taifa ya Gofu ya Wanawake ya Tanzania kutoka Arusha, Madina Idd amekuwa ni Mtanzania wa pili kuthibitisha ushiriki wa mashindano ya wazi ya ubingwa wa gofu yanayotarajiwa kupigwa mwisho wa mwezi huu kwenye viwanja vya Lusaka, Zambia.

Madina amethibitisha jana kutoka klabu ya Gymkhana ya Arusha kuwa atakuwa miongoni mwa Watanzania wachache watakaoipeperusha bendera ya nchi katika mashindano hayo ya siku tatu.

“Naenda kushindana na kufanya vizuri kwa sababu Watanzania, hasa  timu ya wanawake, tumekuwa tukifanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya ngazi ya kimabara,” alisisitiza na kudai tayari amefanya mazoezi ya kutosha kwa ajili ya safari ya Zambia.

Madina anakuwa mchezaji wa pili kutoka Tanzania kuthibitisha ushiriki wake ikiwa ni siku chache baada ya Vicky Elias  wa TPDF Lugalo pia kutangaza azma yake ya kuliwakilisha taifa, huko Zambia.

Kwa mujibu wa rekodi za gofu, Madina Iddi ni mmoja wa wacheza gofu wakubwa wa kike kutoka Tanzania walio na hadhi ya kimataifa.

Licha ya kushinda mashindano kadhaa ya kimataifa nchini Uganda, Kenya na Zambia muongo uliopita aliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili kitimu barani Afrika katika mashindano ya bara la Afrika yaliyofanyika nchini Ghana na katika mashidano hayo pia Madina alichukua nafasi ya kwanza kwa wachezaji binafsi baada ya kumtoa bingwa kutoka Afrika Kusini.

Madina, akiwa pamoja na Angel Eaton pia waliiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika mashindano ya dunia yaliyofanyika nchini Argentina mwaka 2014.

“Nina ukomavu wa kutosha kupambana na yoyote na niko tayari kabisa kwa mashindano ya Zambia,” alisisitiza.

Madina anakwenda Zambia akiwa na rekodi nzuri ya mashindano ya wazi na bado anabebwa na matokeo mazuri ya mashindano ya gofu ya wanawake yaliyofanyika hivi karibuni nchini Ghana.

Madina aliibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya ridhaa ya wanawake yaliyofanyika katika viwanja vya klabu ya Celebrity, Sakumono, Ghana baada kushinda raundi ya mwisho kwa kutumia fimbo 71 tu kujaza vishimo 18 na kumzidi mpinzani wake wa karibu kwa mikwaju 18 katika mashindano hayo ya nchi 7.

Madina aliwapiga wacjezaji wote kutoka nchi kama Ghana, Uganda, Togo, na Nigeria.

Katika mashindano hayo, Madina alianza kwa mikwaju 77 na baadaye kucheza mikwaju 76  kabla ya kumaliza ubishi na mikwaju 71 katika siku ya tatu ya michuano hiyo akitengeneza jumla ya mikwaju 224 katika kujaza mashimo 54 ya mchezo mzima.

Related Posts