Dodoma. Bunge limeelezwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinaendelea na majadiliano kufikia uamuzi wa pamoja kuhusu utaratibu wa kudumu wa kuchangia matumizi na kugawana mapato ya Muungano.
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande leo Jumatatu Juni 26, 2024 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa.
Mbunge huyo amehoji ni lini akaunti ya pamoja ya fedha ya Zanzibar na Tanzania Bara itafunguliwa.
Akijibu swali hilo, Chande amesema utaratibu tayari umependekezwa na Tume ya Pamoja ya Fedha na kuwasilishwa katika Serikali mbili kupitia ripoti ya mapendekezo ya vigezo vya kugawana mapato na kuchangia matumizi ya uendeshaji wa shughuli za Muungano.
“Hadi sasa Serikali mbili zimeendelea na mashauriano na majadiliano kuhusu kufikia uamuzi wa pamoja kuhusu utaratibu wa kudumu wa kuchangia matumizi na kugawana mapato ya Muungano. Maamuzi ya pamoja yatakapofikiwa ndiyo yatakayowezesha kufunguliwa kwa akaunti ya fedha ya pamoja,” amesema.
Katika swali la nyongeza, Issa amesema Katiba inaelekeza kufunguliwa kwa akaunti hiyo na kuhoji nini kilichokwamisha hadi leo haijafunguliwa.
“Kwa kuwa Serikali ya muungano ina kofia mbili– Serikali ya Muungano na Tanzania Bara, je ikitokea upande moja umelalamikia mapato hatuoni kwamba tutakuwa tumeutia doa muungano huu?” amehoji.
Akijibu maswali hayo, Chande amemtoa hofu mbunge huyo kuwa Serikali haijakwama na kwamba utaratibu unaendelea na mapendekezo yakikamilika, akaunti ya pamoja itafunguliwa.
Kuhusu malalamiko, Chande amesema hawawezi kusema kuwa wanalalamika, ila wanasema wanashauriana na kwamba mashauriano hayakatazwi katika kujenga nchi kwa pamoja.