STRAIKA wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele ambaye kwa sasa anaichezea Pyramids yupo katika nafasi nzuri ya kuwania kiatu cha dhahabu baada ya kushika namba mbili kwenye msimamo wa wafungaji bora katika Ligi Kuu Masri.
Hii ni baada ya jana Jumapili kufunga mabao mawili dhidi ya Arab Contractors, timu yake ikishinda 3-1, ambapo Mayele amefikisha mabao 11 katika mechi 14 alizocheza.
Pyramids ndiyo inayoongoza ligi ikiwa na pointi 62 ikiwa imecheza mechi 25 na mchezaji anayeongoza kwa ufungaji wa mabao 12 ni Hossam Ashraf wa Baladiyat El Mahalla.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Mayele amesema kwamba haikuwa rahisi kufikisha mabao 11, kwani wakati anajiunga na timu hiyo alikuwa anasumbuliwa na majeraha ya mguu.
“Wakati najiunga na Pryramids nilipitia changamoto ya majeraha. Kitendo cha kufunga mabao 11 sikukitarajia imekuwa faraja kubwa kwangu, hivyo nitaendelea kupambana hadi ligi itakapomalizika,” amesema.
“Kiukweli Ligi Kuu Misri ni ngumu. Ikumbukwe tunacheza na timu kama Al Ahly ambayo imechukua ubingwa wa Afrika mara nyingi, unaweza ukapata picha ya jinsi ambavyo mchezaji anapaswa kukaza buti ili huduma yake iwe muhimu kwenye timu.”
Mayele aliibuka mchezaji bora wa mechi dhidi ya Arab Contractors jambo ambalo amesema: “Ulikuwa mchezo mgumu na wachezaji wote tulifanya vizuri, hivyo nimefurahi nimeisaidia timu yangu.”
Ndani ya misimu miwili aliyoichezea Yanga alifunga mabao 33 katika Ligi Kuu Bara – 2021/22 ikiwa ni mabao 16 na 2022/23 alikuwa mfungaji bora kwa mabao 17 aliyogongana na yale aliyofunga Said Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyekuwa Simba.