BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeazimia kumfungia vikao 15 Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) kwa kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa Shughuli za Bunge. Anaripoti Mwandishi Wetu (endelea.)
Hatua hiyo imekuja baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kupitia kwa Mwenyekiti wake, Ally Juma Makoa kumkuta na hatia Mbunge kwa kitendo cha Mpina kuitisha Mkutano wa Waandishi wa Habari na kutoa ufafanuzi wa ushahidi alioupeleka kwa Spika.
Amesema kitendo hicho kukiuka Kifungu cha 34 (1) (g) vya Sheria ya Kinga, Madaraka na Hadhi ya Bunge, Sura 296 kinachokataza kusambaza kwa umma, Taarifa zinazofanyiwa kazi na Bunge pasipo kupata kibali cha Bunge.
Licha ya Kamati hiyo kupendekeza Bunge linaazimie Mpina apewe adhabu kwa mujibu wa kifungu cha 84 (3a) cha kanuni za Bunge toleo 2023 ya kutohudhuria vikao vya bunge 10 mfululizo kuanzia leo tarehe 24 Juni 2024, Bunge limeazimia afungiwe vikao 15.
Adhabu hiyo imeongezeka baada ya Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson kuwahoji wabunge wanaoafiki afungiwe vikao 190,15 au 20 waseme ndiyo, lakini wabunge waliosema ndio kwa vikao 15 ndio waliokuwa wengi.
Spika Tulia pia amewahoji wabunge hao kuhusu maoni ya kamati kuhusu ushahidi wa Mpina kuthibitisha tuhuma dhidi ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kusema uongo bungeni na kulipotosha Bunge.
Wabunge hao wamekubali maoni hayo ya kamati ambayo kwa sehemu kubwa yamekubaliana na hoja za Bashe kuwa hakusema uongo bungeni bali alichukua hatua za dharura kuhusu sakata hilo la sukari.
Akifafanua kuhusu adhabu hiyo, Spika Tulia amesema Mpina ameanza kutumia adhabu hiyo leo tarehe 24 Juni 2024, kisha ataendelea kukosa vikao vya bunge hilo la bajeti ambalo linaisha Ijumaa wiki hii.
Ameendelea kufafanua kuwa Mpina atakosa kuhudhuria vikao tisa vya Bunge la Septemba kisha kikao kimoja cha Bunge la Novemba ambapo Mpina atakuwa ametimiza adhabu ya kutohudhuria vikao 15.
“Mheshimiwa Mpina hataruhusiwa kuwa maeneo ya Bunge wala kufanya kazi za Bunge kwa muda wote ambao atakaotumikia adhabu,” amesema Spika Tulia.
Awali wakichangia azimio la kamati hiyo, asilimia kubwa ya wabunge wakimowa, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma, Josephat Gwajima (Kawe) na wabunge wengine zaidi ya 15 waliunga mkono hoja ya kupewa adhabu na kupendekeza iongezwe kufikia 15 au 20.
Adhabu hiyo imekuja baada ya Kamati hiyo kudai imejiridhisha kwamba kitendo alichofanya Mpina ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Bunge kwa sababu ya kudharau Mamlaka ya Spika, kuingilia mwenendo wa shughuli za Bunge na vilevile ni kitendo kinachofedhehesha, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.