‘Nguvu zielekezwe kuzuia ajali za majini’

Bagamoyo. Wakati vyombo vya dola nchini Tanzania vikiweka mikakati kupunguza ajali za barabarani, jitihada kama hizo zimeshauriwa zielekezwe kwenye usafiri wa majini.

Hali hiyo inatokana na ajali mathalani za Mv Bukoba, Mv Nyerere, Spice Islander zilizosababisha vifo na majeruhi, chanzo kikielezwa ni matatizo binafsi ya mabaharia na huenda zingeepukika kama hatua zingechukuliwa.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Juni 24, 2024, Bagamoyo, Mkoa wa Pwani na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mabaharia Dar es Salaam (DMI), Dk Wilfred Kileo na Ofisa Mwandamizi wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (Tasac), Kepteni Gadafi Chambo katika warsha ya mabaharia na watumiaji wa majini.

Warsha hiyo inafanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Dunia yaliyoanza Juni 22 na kuhitimishwa kesho Jumanne, Juni 25, 2024 katika Uwanja wa Nianjema, Bagamoyo.

“Kumekuwa na utaratibu wa mambo ya usalama katika nchi kavu kama ambavyo tumekuwa tunaona vyombo vingi vya dola, kampeni nyingi lakini tunaona kwa mwaka huu ni vizuri sana kukumbushana usalama baharini ni jambo la muhimu.

“Sababu maisha ya mengi yanapotea kwa sababu fursa ni nyingi majini, kwani mambo mengine (yanatokea/ yanasababishwa) ni mambo binafsi, watu wanapaswa kufundishwa kuzingatia usalama,” amesema Dk Kileo.

Amesema kwa kuliona hilo DMI wameandaa kongamano Julai 4 -5, 2024 litakaloangazia fursa za uchumi zilizopo majini na uzingatiaji wa usalama wa watu, vyombo na mali zao.

Dk Kileo amesema kwa sasa wanaendelea na tafiti mbalimbali na mpaka sasa wameona suala la mwendokasi, mambo binafsi na kutokuzingatia taratibu za majini ndio chanzo cha baadhi ya ajali.

“Huko nyuma tulikuwa tunaweka msisitizo zaidi kwenye vyombo, sasa tunaangalia mambo binafsi yanayoweza kuepukika,” amesema Dk Kileo.

Kwa upande wake, Kepteni Chambo amesema usalama wa wanaotumia chombo, mizigo iliyoko ndani, usalama wa maji ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa, kwani  meli inapozama inapoteza watu, mizigo na chombo chenyewe.

Amesema meli inapozama kuna sababu mbalimbali na nyingine za kibinadamu, mathalani mmiliki wa chombo kuwa na sauti zaidi kuliko mabaharia, jambo linalomfanya baharia kufuata anachokisema, ikiwemo kujaza abiria ama mizigo, kwani akikata anaweza kupoteza kazi.

Mbali na hilo, Kepteni Chambo amesema sababu nyingine ni hali mbaya ya hewa, matatizo binafsi ya mabaharia: “Kujiamini kupita kiasi na kumfanya kupuuza kuchukua hatua kwa baadhi ya mambo majini.”

“Tunapataga majanga makubwa sana kama Mv Nyerere, Spice Islander zote hizi ni ‘human errors’. Tunataka kuepukana na haya, kwani madhara yake ni makubwa. Tunapoteza watu wengi. Usalama wa majini ni muhimu mno,” amesema Kepteni Chambo.

Naye Kaimu Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia wa Tasac, Lameck Sondo amesema waendeshaji wa vyombo ndani ya maji wanapaswa kuzingatia usalama kwanza.

“Wanapozingatia usalama majini na usalama wa vyombo, tunazuia ajali zinazoweza kujitokeza na kugharimu maisha ya watu na mali zao,” amesema Sondo.

Amesema kwa sasa Tasac wanatoa vyeti vya kielektroniki pamoja na vitambulisho vitakavyowawezesha kutambulika maeneo mbalimbali wanapopita.

Sondo amesema kwa sasa mabaharia waliosajiliwa ni 8,000 kati yao maofisa ndani ya meli wanakaribia 2,300 na wanawake wanakaribia 200, huku jitihada mbalimbali zikiendelea kuongeza idadi yao.

Related Posts