RC Mtambi aagiza wenye ulemavu watambuliwe, wapewe mikopo

Rorya. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kuwatambua na kuwezesha uanzishwaji wa vikundi vya watu wenye ulemavu katika wilaya zao.

Pia amewataka kusimamia usajili wa vikundi hivyo, ili viwezeshwe kiuchumi.

Mtambi ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Juni 23, 2024, alipofunga mafunzo ya ujasiriamali kwa kikundi cha watu wenye ulemavu cha Demoche kilichopo wilayani Rorya.

Amesema atagharamia mafunzo ya awamu ya pili ya kuwajengea uwezo wanakikundi hicho, ili wafanye shughuli zao kwa weledi na tija.

Mtambi amesema dirisha la utoaji mikopo kwenye halmashauri kwa makundi maalumu litafunguliwa mwezi ujao, hivyo, ametoa rai watu wenye ulemavu watambuliwe na kusajiliwa na kuagiza kundi hilo lipewe kipaumbele kwenye mikopo.

“Wiki iliyopita viongozi wa kikundi hiki walikuja ofisini kwangu, nilipatwa na mshangao mkubwa na hata sasa bado nashangaa, kwa sababu ombi walilokuja nalo ni kutaka niwasaidie wapate mafunzo, ili wapate ujuzi na hatimaye waanze kujishughulisha na kuwa na njia ya uhakika ya kujiingizia kipato.

“Hii ilinishangaza, wengi wetu tunaamini watu wenye ulemavu huwa wanaomba tu misaada,” amesema Mtambi.

Anasema kutokana na hilo, ndiyo maana ameagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) kutoa mafunzo kwa watu hao kulingana na miongozo yao.

“Ingawa kwa mujibu wa taratibu, walitakiwa kwenda ofisi za Sido kwa ajili ya mafunzo, lakini niliagiza watu wa Sido wawafuate huku, ili kuwaondolea usumbufu kulingana na hali zao,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Amesema watu wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya ya kiuchumi katika jamii.

“Sina takwimu, lakini ukweli ni kuwa kundi hili bado halijanufaika na fursa zilizopo, ikiwepo hii ya mikopo ya halmashauri. Kwa kutambua umuhimu wao katika ujenzi wa uchumi wa nchi, niwaagize wakurugenzi na wakuu wa wilaya tutoe kipaumbele kwao,” amesema.

Akitoa taarifa ya kikundi hicho, mwenyekiti Magreth Owesi amesema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mtaji, hali iliyosababisha kushindwa kuendeleza mradi wao wa ushonaji na utengenezaji wa viatu.

“Tulianzisha mradi wa kushona na kutengeneza viatu, lakini kutokana na ukosefu wa mtaji tumeshindwa kuendeleza mradi wetu. Tunaomba tusaidiwe mtaji, ili tuiendeleze mradi wetu kwani mradi huo utatusaidia kukua kiuchumi na kuweza kumudu mahitaji yetu na familia zetu,” amesema Owesi.

Amesema watu wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kujitegemea na hivyo kuondokana na hali ya kuomba misaada kwa watu, ili kujikimu kimaisha.

Katibu wa kikundi hicho, Robert Dismas amesema waliamua kwenda kwa mkuu wa mkoa kuomba kupatiwa mafunzo, ili wapate ujuzi hatimaye wajitegemee.

“Sisi watu wenye ulemavu tumesahaulika hata kwenye suala la elimu, hivyo tuliona tukipata mafunzo ya ujuzi tunaweza kujikwamua kiuchumi,” amesema Dismas.

Amesema jumla ya watu wenye ulemavu 10 kutoka katika kikundi hicho wamepata elimu juu ya utengenezaji wa sabuni za maji na miche pamoja na elimu ya uendeshaji wa biashara kwa siku nne kutoka Sido.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka, amesema zaidi ya Sh200 milioni zinatarajiwa kukopeshwa kwa makundi maalumu wilayani humo baada ya Serikali itakaporuhusu mikopo hiyo isiyokuwa na riba ianze kutolewa.

“Tuna Sh200 milioni ambazo zinasubiri dirisha lifunguliwe na ninakuahidi kuwa watu wenye ulemavu watapewa kipaumbele na tutahakikisha tunawaibua na kuwaongoza namna ya kuomba mikopo hiyo na namna nzuri ya kutumia mikopo watakayopewa, ili ilete tija,” amesema Chikoka.

Chikoka pia ameahidi kuwa mlezi wa kikundi cha Demoche ambapo pamoja na mambo mengine atahakikisha anawatafutia soko la bidhaa zao kwenye taasisi za umma na binafsi, ili kufanya miradi yao kuwa endelevu.

Related Posts