Wanafunzi elimu ya juu watakiwa kutafuta fursa wakiwa vyuoni

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa amewaasa wanafunzi wa vyuo kutafuta fursa wakiwa bado chuoni ili kuwarahishia njia pale wanapohitimu masomo yao.

Ametoa kauli hiyo Juni 22,2024 katika mkutano mkuu wa Asasi ya Haki za Binadamu Chuo Kikuu cha Dar es Salam ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Amesema mwanafunzi anapoanza kujihusisha katika shughuli ambazo anasomea kunamfanya kutengeneza mahusiano ya karibu na wale wanaofanya shughuli anazosomea na kutambulika haraka katika jamii na soko la ajira.

“Nikiwaambia mambo niliyoyajaribu mimi nikiwa chuo, nimejaribu kuwa padri, nimejaribu kuwa mwanasiasa nilikuwa UVCCM nikaona hii hainifai, nimekuwa kwenye shughuli nyingi mpaka kwenye utamaduni.

“Nilikuwa mwenyekiti wa chama cha wanafunzi wa Kimasai hapa na mwisho wa siku nikaangukia huku kwenye utetezi wa haki za binadamu,” amesema Wakili Olengurumwa.

Mkutano huo uliokuwa na ajenda tatu ambazo ni kufanya mdahalo, kuchagua viongozi wapya na kuwafanyia mahafali wanaomaliza ulihudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Ally Seif kutoka dawati la vijana LHRC na Francis Luziga kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Related Posts