Wanamgambo waua polisi 15, raia kadhaa huko Dagestan – DW – 24.06.2024

Taarifa hiyo imethibitishwa na Gavana wa mkoa huo Sergei Melikov alieeleza kuwa watu wenye silaha walishambulia kwa risasi makanisa mawili ya Kiorthodox, sinagogi na vituo vya polisi katika miji miwili ya Derbent na Makhachkala.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya  Dagestan  imesema kundi la watu wenye silaha walifanya mashambulizi hayo karibu wakati mmoja na kwamba kanisa na sinagogi vyoote viliteketea kwa moto.

Mashambulizi ya kigaidi huko Dagestan, Urusi
Moshi ukifuka huko Derbent (mkoa wa Dagstan nchini Urusi) baada ya shambulio la wanamgambo wenye silaha: 23.06.2024Picha: via REUTERS

Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi nchini Urusi imeyahusisha mashambulizi hayo kuwa vitendo vya kigaidi na kutangaza siku tatu za maombolezo katika mkoa huo wa Dagestan wenye Waislamu wengi.

Soma pia: DAGESTAN : Polisi watatu wauwawa katika mripuko

Mamlaka imetangaza operesheni ya kukabiliana na ugaidi katika eneo hilo na kubainisha kuwa watu watano wenye silaha “walitokomezwa.” Haikuwa wazi ni jinsi gani wala wapiganaji wangapi walihusika katika mashambulizi hayo.

Hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulizi hayo licha ya mamlaka kuanzisha uchunguzi wa makosa ya jinai kwa shtaka la vitendo vya kigaidi.

Watu wanne wauawa na wengine 124 wajeruhiwa katika rasi ya Crimea

Ukraine imefanya mashambulizi kadhaa huko Sevastopol katika rasi ya Crimea
Picha hii iliyochapishwa na kampuni ya Maxar Technologies inaonyesha ndege ya kivita ya MiG 31 iliyoharibiwa katika kituo cha anga cha Belbek, karibu na Sevastopol katika rasi ya CrimeaPicha: Maxar Technologies/AP Photo/picture alliance

Katika tukio jingine, Urusi imesema Marekani imehusika moja kwa moja katika mashambulizi yaliyofanywa na Ukraine katika rasi ya Crimea na kusababisha vifo vya watu 4 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 124. Moscow imeilaumu Washington kwa kuipatia Kyiv makombora ya kisasa yaliyotumiwa katika shambulio hilo.

Soma pia: Ukraine yasema imeshambulia mifumo ya kujilinda angani iliyoko Crimea

Mamlaka za Urusi zimesema watoto wawili ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio la roketi huko Sevastopol katika rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi mnamo mwaka 2014.

Rais wa Ukraine  Volodymyr Zelensky  amewatolea wito washirika wake wa Magharibi kuipatia Kyiv silaha zaidi za kimkakati na kutoa idhini ya kushambulia ndani ya Urusi.

(Vyanzo: APE, DPAE)

 

Related Posts