Dorothy alivyoweka rekodi kuikwaa PhD akiwa na miaka 17

Akiwa na umri wa miaka 14 tayari alifanikiwa kuhitimu shahada ya kwanza pamoja na ile ya uzamili.

Pamoja na kufikia hatua hiyo kubwa ya kielimu ambayo kwa umri wake ni nadra sana kufikiwa, bado hakuridhika nayo alitazama mbele na kuweka lengo jingine la kupata shahada ya uzamivu.

Huyu ni Dorothy Jean Tillman, binti mdogo ambaye sasa ana umri wa miaka 18 mkazi wa mji wa Chicago nchini Marekani aliyefanikiwa kuzifikia ndoto zake akiwa katika umri mdogo na kuweka historia ya kipekee baada ya kupata shahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya tabia katika afya (Doctorate degree in Integrated Behavioral health) akiwa na umri wa miaka 17.

Desemba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 17, Dorothy alifanikiwa kutetea tasnifu yake iliyojikita katika kuangalia vikwazo wanavyopitia wanafunzi wa vyuo vikuu, katika kupata matibabu ya afya ya akili iliyomwezesha kuhitimu daraja hilo la juu la elimu.

Shahada hiyo ya uzamivu ameipata katika Chuo Kikuu cha Arizona na kufanikiwa kuweka historia ya chuo hicho na hata duniani kwa ujumla, kuwa mmoja wa watu waliofikia hatua hiyo wakiwa katika umri mdogo.

Akiwa na umri mdogo, Dorothy alionekana kuwa mwenye malengo na mwamko wa kusoma, kwani alianza masomo yake akiwa na miaka saba akiwa anasomea katika mazingira ya nyumbani kwa njia ya mtandao, alianza elimu ya sekondari na baadaye masomo ya ngazi ya chuo.

Kwa mujibu wa tovuti ya NBC News, Dorothy akiwa na miaka 14 alipata shahada ya ‘Bachelor in Humanities’ kutoka Chuo cha Excelsior kilichopo jijini New York mwaka 2018.

Miaka miwili baadaye alifanikiwa kuhitimu shahada yake ya uzamili ya sayansi ( Master’s of Science) kutoka Chuo Kikuu cha Unity na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Arizona kuanza masomo yake ya uzamivu.

Inaelezwa kuwa asilimia kubwa ya masomo yake aliyasoma kwa njia ya mtandao.

Katika mahojiano yake na shirika la habari la The Associated Press Tillman, anasema haikuwa rahisi kufika hapo alipo lakini kilichokuwa kinampa ari na nguvu ya kutimiza lengo lake, ni kuaminiwa pamoja na ushirikiano aliokuwa akiupata kutoka katika familia yake hasa mama yake, ambaye alikuwa akimhimiza kufanya jitihada kwa kile anachokiofanya.

“Ninaweza kusema nisingeweza kufika hapa bila ya jitihada zake na kunipa moyo, alikuwa akifanya kazi kwa bidii kwa ajili ya familia, kwangu familia yangu naweza kuielezea kama timu yangu bora ya ushindi, ”anasema.

Pia anasema ujasiri wa kuyafanya hayo aliupata kutoka kwa bibi yake anayejulikana kama Dorothy Tillman, ambaye alifanya kazi pamoja na Dk Martin Luther King Jr. wakati wa harakati za kudai haki za watu weusi nchini Marekani.

Vile vile alipofanya mahojiano na kituo cha televisheni cha CNN, alibainisha kuwa sababu nyingine iliyompa msukumo wa kusoma shahada hiyo, ni baada ya kuchunguza vikwazo vinavyowazuia wanafunzi wa chuo kikuu kupata matibabu ya afya ya akili hivyo akataka akasome ili awasaidie.

Dorothy ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya uongozi ya Dorothyjeanius Steam, anasema kwa sasa baada ya kuhitimu moja kati ya malengo yake, ni kuhakikisha anaiendeleza taasisi yake hiyo iliyoundwa kwa ajili ya kusaidia vijana katika masuala ya elimu pamoja na sanaa. Anasisitiza kuwa katika kulifanya hilo, pia atatumia maarifa aliyoyapata wakati akisoma shahada yake ya uzamivu.

Anaeleza kuwa katika harakati zake za kuhakikisha taasisi hiyo inakua, anatamani pia kuifikia Afrika na kuwasaidia watoto waliopo katika nchi za bara hilo.

Pia katika mahojiano hayo alisema anatamani kuona kupitia historia yake, iwape moyo vijana kuwa wanaweza kutimiza malengo yao.

Akifanya mahojiano na shirika la ABC Profesa Lesley Manson ambaye ni mmoja wa wahadhiri waliomfundisha, anasema Dorothy ameingia katika historia ya chuo hicho, kwa kuwa mhitimu wa kwanza kupata shahada ya uzamivu akiwa na umri wa miaka 17.

Pia anamuelezea kama mfano bora wa kuigwa kwa wasichana wengine.

Anasema Dorothy ni binti hodari, mchapakazi mwenye mawazo ya kibunifu ambaye anaweza kusimama kama maana halisi ya kiongozi bora.

Naye mama wa binti huyo, Jimalita Tillman alipofanya mahojiano na shirika la CNN, anasema anajiskia furaha isiyo na kifani kuona binti yake amefikia hatua hiyo.

Ukiachana na Dorothy, katika historia ya academia duniani, wapo baadhi ya watu waliowahi kupata shahada ya uzamivu katika umri mdogo na kuwashangaza watu wengi, kama ilivyotokea kwa Dorothy aliyekuzwa katika mji wa Chicago.

Kwa mujibu wa tovuti ya Online phd Program baadhi ya watu hao ni pamoja na Karl Witte mtoto wa mchungaji aliyezaliwa mwaka 1800, ambaye alifanikiwa kupata shahada yake ya uzamivu katika chuo cha Giessen nchini Ujerumani akiwa na umri wa miaka 13 na kuvunja rekodi ya dunia ambayo anaendelea kuishikilia hadi sasa.

Mwingine ni pamoja na Kim Ung-Yong ambaye anatajwa kuwa moja kati ya watu walio na akili nyingi.

Alivunja rekodi ya dunia kwa kuwa mtu aliyewahi kuanza kuzungumza vizuri akiwa na umri mdogo wa miezi sita.

Alipofika miezi nane aliweza kukokotoa hesabu za algebra jambo ambalo liliwashangaza wengi.

Alipofika umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada yake ya uzamivu katika chuo cha Colorado State.

Wengine waliopata shahada ya uzamivu katika umri mdogo ni pamoja na Balamurali Ambati, Ruth Lawrence, Norbert Wiener katika umri wa miaka 17.

Pia yuko Sho Yano (18), Juliet Beni, Charles Homer Haskins (19), Erik Demaine pamoja na Akshay Venkatesh katika umri wa miaka 20.

Kwa Tanzania msichana Mwasi Mboya anatajwa kuwa miongoni mwa watu waliowahi kuhitimu ngazi hiyo wakiwa na umri chini ya miaka 30.

Akiwa na umri wa miaka 28 tu, Mwasi akawa daktari wa falsafa katika fedha na takwimu (PhD in Financial Econometrics and Statistics) kutoka Chuo Kikuu cha Leibniz Hanover cha Ujerumani, alichokuwa akifundisha alipohojiwa na Mwananchi Oktoba 2022.

Related Posts