HATIMAYE na mchezaji anayeitwa Sadio Ntibazokinza naye amepewa ‘Thank You’ katika ukurasa wa Instagram wa Simba. Mashabiki wa Simba walisubiri kwa hamu habari hii. Na kweli, mkataba wake ulipomalizika Simba wakafanya hivyo kwa haraka.
Safari ya Saido katika soka la Tanzania imetatanisha kidogo. Wakati anatua nchini kucheza Yanga kuna mashabiki hasa wa watani wa Yanga, Simba walisikika wakidai alikuwa mzee. Sijui ulikuwa ni ukweli kiasi gani.
Akacheza soka safi lakini wakati huo Yanga walikuwa wanapanda juu chini ya utawala wa GSM. Baadaye wakaamua kuachana na Saido pindi mkataba wake ulipomalizika. Ilizua maswali kidogo kutokana na kiwango cha Saido. Alikuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu klabuni.
Kiburi chao kilitoka wapi? kuna waliodai kwamba Saido alikuwa kiburi. Kuna wengine waliochungulia na kuona kwamba huenda kweli Saido umri ukawa umemkamata. Bahati nzuri maamuzi mabovu ambayo Injinia Hersi na watu wake huwa wanayafanya huwa yanazibwa na matokeo mazuri ya Yanga uwanjani.
Ilikuwa ni rahisi kusahau kama Yanga walikuwa wamefanya maamuzi mabovu kwa Saido kwa sababu ndio kwanza wakaendelea kufanya vyema katika michuano mbalimbali. Saido alienda zake Geita na kuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu.
Baadaye Simba wakamtupia jicho na kuona kwamba angeweza kuwasaidia. Usiwaamini sana mashabiki na viongozi wa klabu hizi. Rafiki zangu walewale ambao walidai Saido ni mzee wakati ule anakwenda Yanga ndio walewale ambao niliwaona wamesimama nyuma ya picha ya Saido akisaini mkataba wa Simba. Maisha bila ya unafiki hayaendi.
Kwa misimu miwili Saido alikuwa anafukuzana na mbio za ufungaji bora. Msimu ule ambao alichota mabao ya Geita na kuhamia nayo Simba alikuwa anafukuzana na Fiston Mayele. Msimu huu alikuwa ameachwa mbali kidogo na Aziz Ki pamoja na Feisal Salum ‘Fei Toto’. Hata hivyo alikuwa na idadi nzuri ya mabao wakati ligi ikiendelea ukingoni.
Katika hii misimu miwili mingine Saido ameibuka kuwa mfungaji bora katika Klabu ya Simba. Amepewa ‘Thank You’ ambao ina utata kidogo. Ni kama ile Thank You aliyopewa na Yanga ambayo kwa kiasi chake ilitetewa na kile kilichotajwa kwamba eti ana nidhamu mbovu.
Safari hii Simba wamedai kwamba Saido amechoka. Kwanini hawakuliona hili wakati Yanga walipokuwa wanamchukua na wao ndio walikuwa wanasema hili? Kwanini hawakuliona hili wakati baadhi ya watu wa Yanga walipolisema hili wakati wanaachana naye?
Labda kwa kudharau kile ambacho Yanga walikuwa wanakisema kisha wao wakambeba huenda ndio ilikuwa ni miongoni mwa anguko la Simba na kupanda kwa Yanga katika miaka ya karibuni? Kwamba kwa miaka ya karibuni Yanga huwa wanaona mbali kuliko wao?
Pamoja na yote hayo Saido anaondoka akiwa mfungaji bora mara mbili mfululizo katika Klabu ya Simba. Inatajwa hana nguvu tena kwa sasa na mabao mengi amefunga kwa penalti. Hata hivyo ukitaka kujua umuhimu wa penalti basi ni pale zinapokoswa. Msimu huu umetuonyesha umuhimu wa penalti baada ya Fei na Aziz Ki kukosa penalti muhimu katika mechi muhimu.
Lakini hii pia inafungua mjadala kuhusu suala la namba na kile ambacho tunakiona uwanjani. Simba hawafurahishwi kabisa na walichokuwa wanakiona uwanjani kutoka kwa Saido lakini namba zake zinatusuta. Ni kama ilivyo kwa Fredy Michael. Ukiangalia uwezo wake na namba zake tangu afike ni vitu tofauti.
Simba wameamua kumla jongoo kwa meno. Wameachana na habari za namba na kuamua kushughulika na kile ambacho walikuwa wanakiona uwanjani. Muda ni hakimu sahihi. Wanachopaswa kwa sasa ni kutafuta wachezaji wa mbele ambao namba na uwezo wao vitaongea zaidi kuliko ilivyo kwa Saido.
Kama Saido alitajwa kuwa hana nguvu ingawa alikuwa anafunga basi ni wakati mwafaka kwao kutafuta damu changa ambayo inafanya mambo yote kwa usahihi. Bahati mbaya hii imekuwa changamoto kwa Simba katika miaka hii anatoka afadhali anaingia potelea mbali.
Mfano mzuri wa kuzima habari ya Saido ilikuwa ni katika dirisha la Januari wakati Simba walipopata fursa ya kuleta wachezaji takriban saba katika dirisha dogo. Miongoni mwa waliokuja ni kina Pa Omary Jobe, Edwin Balua, Ladack Chasambi na Fredy. Jaribu kulinganisha mchango wa wote hao wengine na Saido kuelekea mwishoni mwa msimu.
Ukiachana na vijana wetu wachanga Chasambi na Balua, angalia mchango wa Jobe dhidi ya Saido. Bado Saido alikuwa na mchango mzuri katika timu kulinganisha na Jobe. Na sasa Saido ameondoka kabisa. Ni muda muhimu kuleta wachezaji ambao watahalalisha kuondoka kwake.
Bahati nzuri labda tuseme kwamba suala la uhamisho wa wachezaji limepelekwa kwa watu wengine kina Crescentius Magori. Labda huenda wakairudisha Simba katika mstari sahihi zaidi. kama wakiletwa kina Jobe wengine sidhani kama mashabiki watawaelewa.
Mwisho wa siku pengine ni wakati pia wa kumshukuru Saido mwenyewe na pia kumpa pole. Anabakia kuwa mchezaji mwenye wasifu mkubwa zaidi kuwahi kucheza soka la Tanzania. Amecheza Ulaya katika nchi za Ufaransa na Uholanzi.
Bahati mbaya amekuja kumalizia mpira wake katika nchi ambayo ina mihemko mingi na mashabiki huwa wanadharau wachezaji wenye wasifu mkubwa. Kama Watanzania wanamzomea Mbwana Samatta, alama yao ya soka, itakuwa Saido?
Labda wakati umefika kwa Saido kwenda kujaribu malisho mema nje ya mipaka yetu. Sidhani kama ana nafasi nyingine ya kwenda katika klabu kama Geita na kisha aibukie tena Simba, Yanga au Azam. sidhani.