MJADALA mkubwa wiki iliyopita ulikuwa ni wa sakata la beki wa kati, Lameck Lawi kutambulishwa rasmi ndani ya kikosi cha Simba ikiwa ni usajili wa kwanza kwa timu hiyo kwa ajili ya kuongeza nguvu wakati wa mashindano mbalimbali msimu ujao.
Nyota huyo aliyeonyesha kiwango bora, amesajiliwa akitokea Coastal Union ya jijini Tanga ingawa baada tu ya utambulisho wake yameibuka mambo mengi ambayo kwa kiasi kikubwa yanazidi kutia dosari soka letu ambalo linazidi kupiga hatua kubwa.
Baada ya Simba kumtambulisha beki huyo, ghafla Coastal Union ikaibuka na kueleza haitambui suala la nyota wao kujiunga na timu hiyo ya Msimbazi, hapo ndipo ikaleta sin’tofahamu kubwa kwa wadau wa soka nchini wakitaka kufahamu kilichokuwa nyuma ya sakata hilo.
Coastal Union kupitia kwa ofisa habari na mawasiliano wake, Abbas Elsabri, alithibitisha mazungumzo ya kumuuza nyota huyo kwenda Simba yalikuwapo ingawa yalifeli baada ya miamba hiyo kushindwa kuzingatia makubaliano waliyoingia awali.
Abbas alisema, walikubaliana na Simba kumlipa Lawi fedha zake hadi kufika Mei 14, 2024 ila hawakufanya hivyo huku jambo la pili, walipaswa kulipa pesa ya manunuzi ya mchezaji hadi kufikia Mei 31, 2024 na hawakuzingatia pia makubaliano hayo.
Hata hivyo, Simba inaelezwa kulipa fedha hizo Juni 10, 2024, ikiwa imelipa sehemu kubwa ya fedha na Coastal Union kuamua kusitisha mauziano hayo kisha kurudisha fedha zote za wekundu hao jambo ambalo limeleta sintofahamu hapa nchini.
Kwa upande wa Simba kupitia kwa Crescentius Magori anayesimamia suala zima la usajili alisema, walichelewa kulipa pesa ila hadi Juni mwaka huu walikuwa wamekamilisha, hivyo walifuata utaratibu kwani hata nyaraka zote za usajili wanazo.
“Tumemsajili Lameck Lawi kwa kufuata utaratibu, tunafanya kazi kwa weledi, hoja zao ni dhaifu kusema mkataba umevunjika kwa sababu pesa haikulipwa yote, nyaraka zote tunazo na hata tukienda FIFA, mpira ni wa FIFA na hauishii hapa,” alisema.
Ukisikia kauli hizi za pande zote mbili, ndipo unagundua kuna shida kwenye soka letu kwani linaendeshwa tofauti na ilivyo duniani kote yaani kwa kiufupi unaweza kulitafsiri kwa msemo wetu tuliouzoea wa ‘Soka letu kivyetu vyetu’.
Kwa nchi zilizoendelea, ni nadra kuona mambo kama haya yakitokea kwani mchezaji anapotoka timu nyingine basi utakuta katika mitandao ya kijamii ya klabu husika ikiweka wazi kufikia makubaliano hayo jambo ambalo ni ngumu kwetu Tanzania.
Kwa mfano mchezaji aliyetoka Manchester United, akitambulishwa Arsenal utaona timu aliyotoka ikithibitisha usajili wake wa kuondoka ingawa kwa nchini kwetu imekuwa ni tofauti na mara nyingi imekuwa kwenye nadharia za kubebana na kukomoana wala sio kwa kufuata weledi.
Sakata la Lawi, linaonyesha bado soka la Bongo lina safari ndefu kufika nchi ya ahadi kwani matukio ya aina hii yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na kuzidi kuweka dosari japo yamekuwa yakichukuliwa kawaida na kuonekana ni utamaduni wetu tuliojijengea.
Kabla la sakata hili la Lawi, iliibuka ishu ya aina hii ya kimkataba ya mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube aliyekuwa anaishtumu timu hiyo kukiuka makubaliano huku viongozi nao wakiona mchezaji hayuko sahihi hali iliyowafanya kupelekana TFF.
Jingine ni suala la Feisal Salum ‘Fei Toto’ akiwa anataka kuondoka Yanga na kwenda kujiunga na Azam ambapo ilisababisha hadi Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kuzitaka pande zote mbili kukaa chini na kumaliza tofauti zao.
Ishu nyingine iliyotikisa ni ya aliyekuwa winga wa Yanga, Mghana Bernard Morrison, ambaye sinema yake ilikuwa kubwa kwani ilibidi kupelekana kwenye Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi ya Michezo (CAS) ili kupata ufumbuzi wa kimkataba.
Sakata jingine lilitokea msimu wa 2020/2021, ambapo Simba ilimsajili winga, Perfect Chikwende kutoka FC Platnum ya kwao Zimbambwe baada ya kuwafunga kwenye michuano ya CAF japo usajili huo uligeuka kaa la moto kwa ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Ujio wa winga huyo uliifanya Simba kumtoa Mkenya, Francis Kahata katika usajili wa wachezaji wa Ligi ya ndani na kubaki kutumika kimataifa kutokana na sheria za wakati huo na kuingia Chikwende japo baada ya kushindwa kuonyesha ubora wakaachana naye.
Kitendo cha Simba kuachana na Chikwende baada ya miezi sita tu, akaanza kuwaletea shida kuhusu mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu uliobakia jambo ambalo linaonyesha wazi muda mwingine viongozi wa hizi timu wanafanya uamuzi kwa mihemko.
Kuonyesha mambo haya hufanywa kwa mazoea, Julai 9, 2022 uongozi wa Yanga ulimtambulisha kiungo Mrundi, Gael Bigirimana ambaye alitua nchini akiwa na wasifu mkubwa (CV) baada ya kuchezea timu mbalimbali hususani Newcastle United ya Ligi Kuu ya England.
Usajili huo ulishtua kutokana na wasifu wa nyota huyo ingawa mambo yalienda tofauti na kujikuta akikosa hadi nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza na viongozi wa Yanga kumtoa kikosini na nafasi yake kuchukuliwa na beki Mmali, Mamadou Doumbia.
Kitendo cha mchezaji huyo kuondolewa kimyakimya, ilibidi kufungua mashtaka ili alipwe fedha zake zote baada ya kuvunjiwa mkataba, hivyo viongozi wa Yanga wakaanza kuhaha japo mwishoni walilipa kwa ajili ya kukwepa rungu la kufungiwa usajili.
Ndio maana unaweza ushishangae sana Yanga kutangaza kuwa ilipata hasara ya Sh1 bilioni katika bajeti yake ya mwaka uliopita. Kulipa mamilioni ya pesa kwa wachezaji walioingia na kuvunjiwa mikataba inaweza kuwa ni mzigo mkubwa sana wa gharama kwa klabu. Klabu inakosaje kupata hasara?
Yapo madudu mengi katika soka letu yanayokiuka taratibu za soka kidunia lakini mwisho wa yote hufunikwa na kuishi kwenye msemo wa ‘soka letu kivyetu vyetu’.