Moshi. Kesi ya mauaji inayomkabili mkazi wa Katanini, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Beatrice Kwai (36) anayetuhumiwa kumuua mumewe, Evagro Msele (43) imepigwa kalenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi hadi Julai 8, 2024.
Tukio hilo la mauaji ya mfanyabiashara huyo maarufu mjini hapa, lilitokea usiku wa Mei, 25 2024 katika Kitongoji cha Pumuani A, wilayani Moshi baada ya mwanamke huyo kudaiwa kumvizia mumewe akiwa nyumbani kwa mzazi mwenzake kisha kumshambulia kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni kisu.
Kesi hiyo, imefikishwa mahakamani hapo leo, Juni 25, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Hudi Majid huku upande wa Mwendesha Mashitaka wa Serikali ukiongozwa na Ramadan Kajembe.
Kwa mara ya kwanza, mshitakiwa huyo, alifikishwa mahakamani hapo, Juni 10, 2024 mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Herieth Mhenga na kusomewa mashitaka yake na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Henry Daudi.
Leo, mshitakiwa huyo alipofikishwa mahakamani hapo, mwendesha mashitaka huyo wa Serikali, Kajembe aliieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na hivyo kumwomba hakimu kuipangia kesi hiyo tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imekuja leo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake haujakamilika, tunaomba kesi hii ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuitwa,” amesema.
Hata hivyo, Hakimu Hudi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 8, 2024 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa, hivyo mshitakiwa huyo amerudishwa Gereza la Karanga kwa kuwa kesi yake haina dhamana.