Kule NBA… Wembanyama ni mrefu, halafu kiatu chake balaa

NEW YORK, MAREKANI : LIGI ya Kikapu Marekani (NBA) ni maarufu na ndiyo mchezo wenye wachezaji wengi mabilionea duniani kuliko yote. Hii ni ligi ya watu wenye pesa zao.

Kipato cha chini kwa mchezaji kwa mwaka ni takriban Dola 10 milioni ambacho anavuta supastaa Victor Wembanyama ‘Wemby’ anayeichezea San Antonio Spurs.

Hata hivyo, Wembanyama ambaye pia ndiye mchezaji mrefu kuliko wote NBA akiwa na urefu wa futi 7 na inchi 4, analipwa kiasi hicho cha fedha kutokana na msimu uliomalizika wiki iliyopita ndiyo ulikuwa msimu wake wa kwanza akicheza katika ligi hiyo katika nafasi za Center na Power Forward.

Nyota huyo alikuwa chaguo la kwanza (first draft) wa Spurs kutoka Metropolitans 92 katika msimu huo wa NBA uliofanyika Juni 2023, ingawa tofauti na mastaa wengine waliotangulia walivyochaguliwa jamaa aliwahi kucheza sana  katika nchi yake ya asili, Ufaransa kwenye timu za Nanterre 92, ASVEL, pia Metropolitans 92.

 Unajua jamaa anashangaza katika mengi? Sikia, Wembanyama aliyezaliwa Januari 4, 2004 ni mrefu, pia kiatu chake si mchezo kwani anavaa namba 15. Kwa Wamarekani kiatu hicho kinapatikana katika maduka machache, lakini  mara nyingi wenye miguu ya ukubwa huo hutuma oda viwandani ili kutengenezewa saizi zao.

Wembanyama kwa sasa ni staa mkubwa duniani kutokana na kucheza ligi hiyo na mchezo wa wenye pesa akiwa na kilo 95, kiatu chake kwa sasa anatengenezewa na kampuni ya Nike kwa gharama ya takriban Sh13.4 milioni na kila mchezo anakuwa na kitu kipya kama ilivyo kwa mastaa wa ligi hiyo.

Hata hivyo, upande wa Wembanyama ukubwa wa mguu wake ni wa pili katika ligi hiyo kwenye miaka ya karibuni, kwani yupo mwamba anayeitwa Tacko Fall, Msenegali anayeicheza kwa sasa katika timu ya Piratas de Quebradillas ya Puerto Rico ambayo ni sehemu ya nchi ya Marekani. Fall anavaa namba 17 akiwa na urefu wa futi 7 na inchi 6.

Usishangae sana, kwani mwamba huyo enzi zake akicheza NBA aliwapa kazi ngumu makocha wa timu pinzani na wachezaji wao juu ya upangaji wa namna kumkaba, kwani kwa nafasi yake kama beki iliwalazimu mara nyingi washambuliaji kumzonga wengi ili mmoja apate upenyo wa kutupia nyavuni.

Wembanyama aliingia NBA akiwa mmoja wa wachezaji warefu zaidi katika ligi. Urefu wake umesababisha maswali kuhusu uimara wake. Licha ya ubora wake, Wembanyama mara nyingi anacheza akitokea pembeni mwa uwanja.

Kwa upande wa ulinzi, Wembanyama ni mzuiaji mzuri kutokana na urefu wake. Hata hivyo, kutokana na urefu na kwa staili ya kisasa ya uchezaji kikapu kuna nyakati mchezaji huyo anapata shida katika uzuiaji.

Wakati wachambuzi wengi wakiona mchezo wake kuwa wa kipekee, wengine wanamfananisha na magwiji kama Wilt Chamberlain na Kareem Abdul-Jabbar waliokuwa warefu, lakini enzi zao walicheza kwa ubora wa juu na walikubalika katika ligi hiyo.

Tukirejea kwa Wembanyama, mkali huyo Julai, mwaka jana, alikuwa zake kitaa akikatiza katikati ya Jiji la Las Vegas. Katika pitapita zake wakati akikatiza karibu na casino moja mwanamuziki maarufu wa Marekani, Britney Spears alimuona kwa mbali na kumkimbilia akiwa na walinzi wake ili kwenda kumshangaa kwa karibu.

Baada ya Britney kumfikia Wembanyama alimrukia mgongoni huki akimsalimia, lakini jamaa wala hakuwa na mpango naye kwani aliendelea na safari yake licha ya kwamba alitambua alikuwa akisalimiwa na nyota mkubwa na maarufu wa muziki duniani.

Hata hivyo, haikushia hapo, kwani Wembanyama ambaye pia anatoka familia ya kishua kule kwao Ufaransa, mmoja wa walinzi wake alimrushia kibao cha usoni Britney na nusura walinzi wa pande mbili wazichape, lakini walimalizana wenyewe na kila mmoja akashika hamsini zake.

Tukio hilo ambalo liliwashangaza watu wengi lilimuacha mwanamuziki huyo akiishia zake kitaa huku akitokwa na machozi, kwani kibao kile kilimfanya atoe mlio mkali mithili ya mtu aliyeangukiwa na kitu kizito.

Mastaa wengine walio katika tano bora ya nyota warefu NBA kwa sasa ni pamoja na Giannis Antetokounmpo wa Milwaukee Bucks na Joel Embiid anayeichezea Philadelphia 76ers wote wakiwa na futi 7 na inchi 0, huku Nikola Jokic (Denver Nuggets) akiwa na futi 6 na inchi 11 ilhali Lebron James ana futi 6 na inchi 9.

Wakati Wembanyama akiwa bado kijana anayeendelea kurefuka, anatabiriwa huenda akamfikia au kuvuka urefu wa supastaa wa zamani wa ligi hiyo, Gheorghe Muresan aliyekuwa na urefu wa futi 7 na inchi 7 sambamba na Manute Bol, huku Slavko Vranes na Shawn Bradley akiwa na futi 7 na inchi 6 kila mmoja.

Related Posts