Maandamano yapamba moto Kenya, wanaharakati 10 watekwa

MAELFU ya vijana wamefurika katikati mwa barabara za miji nchini Kenya kushiriki maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha 2024 ilihali wabunge wakiendelea kuujadili bungeni. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Milipuko inadaiwa kusikika katikati ya jiji la Nairobi wakati polisi wakifyatua mabomu ya machozi dhidi ya vijana wanaopinga kelele wakielezea kutoridhishwa kwao na muswada huo.

Vijana hao wanaonekana kutiwa mori na kukamatwa kwa wenzao na maafisa wa polisi waliowateka nyara au kuvamia nyumba zao alfajiri leo Jumanne.

Maandamano hayo ya amani yanaendelea katika miji ya Mombasa, Eldoret, Kisumu, Homa Bay na Nyahururu na maeneno mingine.

Polisi wanawafyatulia mabomu ya machozi licha vijana hao kuandamana kwa utulivu huku wakionekana kuwazuia wasielekee majengo ya bunge.

Jana Jumatatu, Waziri wa Usalama wa Ndani nchini humo, Kithure Kindiki alisema waandamanaji wanapaswa kudumisha amani.

Kwa sasa, wanakimbizana na polisi wanaowarushia mabomu ya machozi huku vijana wakipiga mayowe, vuvuzela na filimbi.

Maafisa wa polisi walianza kushika doria katikati mwa jiji la Nairobi kuanzia saa 11 alfajri ya leo.

Polisi walifika katika barabara za Kati ya jiji kuanzia saa 11 alfajiri na kupangwa katika maeneo wanayokutania vijana kuanza maandamano ambayo yamekuwa ya amani.

Hata hivyo, hali hiyo haikuwazuia vijana hao kuandamana huku barabara za jiji hazina shughuli nyingi kama kawaida ikiwa ni ishara kuwa wafanyabiashara wanahofia kufungua biashara zao.

Kuna magari machache katikati mwa jiji kinyume na kawaida ambapo huwa ni vigumu kupata egesho.

Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) kikiongozwa na Rais wake Faith Odhiambo, kimewataka waandamanaji kutohusika na ghasia, uharibifu wa mali, kuchokoza polisi na kutovamia majengo yanayolindwa.

“Tunatoa wito kwa wananchi wote kuwa waangalifu zaidi wakati huu. Wacha tuendelee kushiriki na kuwasiliana habari yoyote ambayo unaweza kuwa nayo ili kujua waliko wenzetu,” alisema.

Mwanaharakati wa kisiasa Gabriel Oguda.

Hayo yanajiri wakati watumiaji kadhaa wa mitandao ya kijamii na wabunifu wa maudhui hawajulikani walipo baada ya kutekwa nyara usiku wa kuamkia leo Jumanne tarehe 25 Juni kabla ya maandamano ya kupinga mswada wa fedha.

Maafisa wa Polisi hiyo walisema hatua hii ni miongoni mwa mikakati inayotumiwa kutuliza maandamano ya kupinga ushuru uliopendekezwa. Miongoni mwa waliochukuliwa ni pamoja na mwanaharakati wa kisiasa Gabriel Oguda.

Polisi wamesema alikuwa miongoni mwa angalau watu 10 ambao wamekusanywa leo Jumanne.

“Ninaweza kuthibitisha kuwa kaka yangu amechukuliwa na watu wasiojulikana kutoka nyumbani kwake dakika 5 zilizopita,” Zachary Oguda, kakake Gabriel, ‘alitweet’ saa 2:53 asubuhi Jumanne.

Osama Otero ambaye amekuwa mstari wa mbele kwenye mtandao wa X kuhusu kupinga mswada wa fedha wa 2024, pia aliripotiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana.

Related Posts