Mashambulizi ya Israel yawaua takribani 24 mjini Gaza – DW – 25.06.2024

Jeshi la Israel, IDF limesema miongoni mwa waliokuwa wakilengwa ni waliohusika katika shambulizi la Oktoba 7 na kuwateka watu. Shambulizi hilo limefanyika Jumatatu usiku katika maeneo ya wakimbizi ya Al-Shati na Daraj Tuffah.

IDF imesema wanamgambo hao walikuwa wakiendesha shughuli zao ndani ya maeneo ya shule ambayo yalikuwa yanatumiwa na kundi la Hamas kujificha na kufanya shughuli zake za kigaidi. Kwa mujibu wa taarifa ambazo hazijathibitishwa, mmoja wa watu waliouawa ni dada wa kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh.

Marekani yaitaka Israel kuzuia vita kusambaa hadi Lebanon

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesisitiza umuhimu wa Israel kuepusha kutanuka kwa vita hivyo hadi Lebanon, na umuhimu wa kufikia azimio la kidiplomasia ambalo litaruhusu familia za Israel na Lebanon kurejea kwao.

Matamshi hayo ameyatoa Jumatatu katika mkutano wake wa Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant aliyeko ziarani Washington, Marekani, wakati wakijadiliana kuhusu juhudi za kufikia makubaliano ya kuwaachia huru mateka wanaoshikiliwa Gaza. Mei 31, Rais wa Marekani Joe Biden, aliweka mpango wa kusitisha mapigano huko Gaza na kuwaachia huru mateka.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony BlinkenPicha: Jacquelyn Martin/Pool/picture alliance

Huku hayo yakijiri, Israel imesema itazitumia wiki zijazo kujaribu kuutatua mzozo na kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran, na ingependelea kupatikana suluhisho la kidiplomasia.

Hayo yameelezwa siku ya Jumanne na mshauri wa usalama wa taifa wa Israel, Tzachi Hanegbi. Mshauri huyo amesema pia Israel ilikuwa ikijadiliana na Marekani kuhusu uwezekano wa juhudi za pamoja zinazofanywa na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa kadhaa ya Kiarabu kutafuta mbadala wa utawala wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Baerbock kukutana na kiongozi wa Mamlaka ya Kipalestina

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, Jumanne anakutana na Waziri Mkuu mpya wa Mamlaka ya Kipalestina, Mohammad Mustafa kujadiliana mustakabali wa jukumu la Mamlaka ya Kipalestina, baada ya vita.

Mazungumzo kati ya Baerbock na Mustafa yanafanyika mjini Ramallah, Ukingo wa Magharibi. Baerbock, anatarajiwa kukutana pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz mjini Jerusalem, huku mazungumzo yao yakiangazia kile ambacho Ujerumani imekielezea kama “hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza” na kuwaachia huru mateka walinaoendelea kushikiliwa.

Gazastreifen | Beerdigung des Al Jazeera-Kameramanns Samer Abu Daqqa in Khan Younis
Waombolezaji katika mazishi ya mpigapicha wa Al Jazeera, Samer Abu Daqqa, miongoni mwa waandishi habari waliouawa GazaPicha: Bassam Masoud/REUTERS

Katika taarifa nyingine, uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari vya kimataifa umegundua kuwa zaidi ya waandishi 100 wa Kipalestina na watu wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari wameuawa Gaza wakati wakitekeleza majukumu yao, huku wengine wakiwa wakiwa wamevalia fulana zinazowatambulisha kama waandishi habari.

Soma zaidi: Waandishi 99 waliuawa katika mzozo wa Israel na Hamas

Uchunguzi huo uliofanywa kwa miezi minne na kuchapishwa Jumanne, uliongozwa na taasisi ya uchunguzi inayohusika na hadithi zilizozuiwa kusimuliwa, na kulihusisha shirika la habari la Ufaransa, AFP, The Guardian na Kundi la waandishi habari wa Kiarabu wanaoandika habari za uchunguzi, ARIJ, miongoni mwa wengine.

Mwanzilishi wa taasisi ya uchunguzi ya hadithi zilizozuiwa kusimuliwa, Laurent Richard, amesema uamuzi huo ulifikiwa mwezi Februari kuzindua ”Mradi wa Gaza,” ushirikiano uliowahusisha waandishi habari 50 na vyumba 13 vya habari vya kimataifa, kuchunguza vifo vya waandishi wa habari katika maeneo ya Palestina.

(AFP, AP, DPA, Reuters)

 

Related Posts