Sengerema. Kufuatia jaribio la kutaka kuua mtoto mwenye ualbino, Eyani Donad (4) katika Kata ya Kasungumile wilayani Sengerema, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa onyo kwa wote wenye nia ovu kwamba watakamatwa na sheria itachukua mkondo wake.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, Juni 25, 2024 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lwelwe Mpina alipokuwa akizungumza na watendaji wa kata, viongozi wa dini, maofisa polisi, maofisa usafirishaji, polisi jamii na watu wenye ualbino wilayani Sengerema.
Kamanda huyo amesema jaribio hilo lilitokea wiki moja iliyopita saa tano usiku baada ya watu watatu waliofika kwenye nyumba ya familia ya mtoto huyo wakijitambulisha kuwa ni ndugu.
“Mmoja wao alisema anaitwa Amos na akasema amewaletea zawadi. Mama wa familia hiyo, Milembe Manoni hakufungua mlango, badala yake alipiga simu na kutoa taarifa kwa viongozi, walipobaini wanachongewa, watu hao walitoweka kusikojulikana,” amesema Mpina.
Hata hivyo, amesema Jeshi la Polisi kwa sasa linawasaka watu hao huku akitoa wito kwa wakazi wa Sengerema kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama juu ya uwepo wa viashiria vya watu wenye nia ovu dhidi ya watu wenye ualbino.
Wilaya ya Sengerema ni miongoni mwa wilaya ambazo kipindi cha nyuma zilikumbwa na matukio ya watu wenye ualbino kuuawa.
Mpina amewataka wananchi wilayani humo kuwa makini na watoe taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na mauaji au kuwadhuru watu hao.
Amesema hapa nchini hivi sasa kuna matukio ya kuua watu wenye ualbino, hali inayotishia maisha yao.
Pia, amewaonya waganga wa kienyeji, wachimba madini, wavuvi na wafanyabiashara wanaojihusisha na mambo yasiyofaa ili wapate utajiri, kuwa siku zao zinahesabika.
Mmoja wa watu wenye ualbino, Maneno Pelenya ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Sengerema, amesema jamii inatakiwa kubadilika na kuachana na imani potofu za kuua watu wenye ualbino kwa lengo la kupata utajiri au uongozi.
Ameviomba vyombo vya dola kuwa makini na kuwasaka watu wanaofanya vitendo hivyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Sengerema, Haji Mohamed amesema Jeshi la Polisi wilayani Sengerema liko makini kuhakikisha hakutokei mauaji ya watu wenye ualbino huku akiwataka wananchi kuwa walinzi namba moja kwenye maeneo yao.
Baadhi ya wananchi walioshiriki mkutano huo wamesema watakuwa bega kwa bega kuhakikisha wanawalinda watu wenye ualbino.