Dar es Salaam. Mwanasheria Boniface Mwabukusi (Mbeya) ni miongoni mwa mawakili sita waliopitishwa kugombea urais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti 2, mwaka huu jijini Dodoma.
Mbali na Mwabukusi, taarifa iliyotolewa na kamati ya uchaguzi ya TLS jana Juni 24, 2024 imewataja wagombea wengine kuwa ni Ibrahim Bendera (Ilala), Emmanuel Muga (Ilala), Revocatus Kuuli (Mzizima), Paul Kaunda (Kanda ya Magharibi) na Sweetbert Nkuba (Kinondoni).
Mwabukusi ameibuka kuwa wanasheria maarufu baada ya kujitosa kupinga mkataba wa uendelezwaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World, ambao hata hivyo ulipitishwa na kampuni hiyo imeshaanza kazi katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mwabukusi na wenzake walifungua kesi ya kuupinga mkataba huo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, lakini pia walishindwa kesi hiyo.
Kutokana na kampeni yake hiyo, Mwabukusi alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Novemba 2023 kwa madai ya utovu wa nidhamu na Mei 17, 2024 kamati hiyo ilimpa onyo wakili huyo.
Kupitishwa kwa Mwabukusi kumekuja wakati kukiwa na maoni miongoni mwa mawakili ya kushuka kwa hamasa ya uchaguzi katika chama hicho, huku pia ikielezwa kubanwa kwa chama hicho kutokana na marekebisho ya Sheria ya TLS.
Kutangazwa kwa majina hayo kunatoa nafasi ya wateuliwa kuanza kampeni kuanzia Jumamosi ya Julai 6 hadi Agosti 1 mwaka huu huku uchaguzi
Majina hayo yametangazwa leo ikiwa ni baada ya muda wa kutuma maombi wa kuwania nafasi hizo kuongezwa hadi Juni 6 mwaka huu badaka ya Mei 2024.
Walioteuliwa kuwania nafasi ya makamu wa rais ni Laetitia Ntagazwa (Iringa), huku Aziza Msahi (Ilala) taarifa ilieleza kuwa hakustahili kuchaguliwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 (3) (d) cha Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika Sura 307 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Sekta (marekebisho mengineyo) Na. 11 ya 2023.
Sheria hiyo inawataka wagombea kuendesha au kusimamia kampuni ya mawakili ambayo ina wafanyakazi watano au zaidi au wanaohudumu katika bodi yoyote ya uongozi inayotambuliwa.
Nafasi ya mweka hazina walioteuliwa ni Stella Rweikiza (Kinondoni), nafasi ya Mwenyekiti Chama cha Wanasheria Vijana (AYL) walioteuliwa ni Emmanuel Ukashu (Ilala), Denis Eliasaph (Kinondoni) huku Victor Kweka (Dodoma), Joseph Lameck na Moses Misiwa (Mwanza) wakikosa sifa kwa mujibu wa kanuni mbalimbali za chama hicho.
Katika upande wa wagombea wa uongozi kanda mbalimbali waliopitishwa watakaokuwa wajumbe wa baraza ni Godluck Walter (Ilala), Ipilinga Panya (Mzizima), John Nyange (Temeke), mwanachama wa Excom wa kanda kwa wanasheria vijana, Fatuma Thabit.
Bagamoyo, viongozi wa kanda na wajumbe wa baraza waliopitishwa ni Dk Anna Henga (Bagamoyo), Reginald Shirima (Ubungo) huku Grace Nakabugo (Kinondoni) akikosa sifa.
Kanda ya Ziwa walioteuliwa ni Seleman Kassim Gilla (Mwanza), Samwel Angelo (Kagera) na Stephen Kitale Cleophace (Mwanza) akikosa sifa.
Kanda ya kusini, mjumbe wa baraza na viongozi aliyeteuliwa ni Baraka Mbwilo (Mbeya).
Kanda ya magharibi, Emmanuel Thomas Msasa (Kigoma), kanda ya kati Barnabas Pascal Nyalusi (Iringa) na kanda ya kaskazini, David Shilatu (Moshi).