Prince Dube afunguka anavyojifua kwa 2024/25

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Azam FC ambaye kwa sasa anatajwa kujiunga na Yanga msimu ujao, Prince Dube amesema yupo fiti kwa ajili ya mapambano baada ya kukaa nje kwa muda mrefu.

Dube ambaye alionyesha ubora kwenye mchezo wa Wape Tabasamu uliochezwa mjini Morogoro ukizikutanisha timu Job na Kibwana akitupia bao katika ushindi wa mabao 6-2 wa timu Job, ameliambia Mwanaspoti kuwa licha ya kukaa nje kwa muda yupo timamu kimwili.

Dube ambaye mara ya mwisho kucheza mechi ya ligi ilikuwa Februari 9 dhidi ya Simba wakiambulia sare ya bao 1-1, alisema licha ya kutoonekana uwanjani muda mrefu hana wasiwasi na kiwango chake, huku akiweka wazi kuwa amekuwa akifanya mazoezi na kucheza mechi.

“Miezi minne sijacheza mechi za ushindani nimekumbuka sana na nipo tayari kwani nimekuwa nikifanya mazoezi na nacheza mechi za matamasha na ndio maana nimeonekana Morogoro, sijaanzia hapo,” alisema.

“Napenda kazi yangu sio rahisi kusubiri maamuzi. nimekuwa nikipambana kujitengenezea mazingira ya kuwa bora uwanjani. Hii ndio kazi ninayoitegemea, hivyo ni suala la muda tu kurudi kucheza soka la ushindani.”

Dube alisema kukaa nje bila kucheza mpira imekuwa ikimsumbua, lakini anaamini bado ana uwezo wa kufanya vizuri, lakini hawezi kuwa bora bila kuwa na mechi za ushindani. “Kufanya mazoezi ni suala la kawaida tangu nimecheza mechi na Simba nikiwa na timu ya Azam FC sikuwa na nyakati nzuri za kucheza mechi. Ni mazoezi tu hivyo kupitia matamasha haya naongeza ubora wa ushindani uwanjani,” amesema.

Alipoulizwa ni timu gani mashabiki wamtarajie kumuona msimu ujao, amesema hawezi kuweka wazi lakini watarajie kumuona akikipiga katika Ligi Kuu Bara.

Akizungumzia ubora wa Azam FC, alisema ni timu nzuri na imefanya maboresho mengi akiiombea ifanye vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na namna ilivyoboresha kikosi.

Related Posts