Dodoma. Serikali imesema ucheleweshaji wa usajili wa kudumu wa taasisi na madhehebu ya dini nchini unasababishwa na mambo kadhaa, ikiwamo muda wa matazamio kubaini kama hakuna dosari kwa jamii.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema hayo bungeni leo Juni 25, 2024 alipojibu swali la msingi la mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda.
Mbunge huyo amehoji ni nini sababu ya ucheleweshaji wa maombi ya usajili wa taasisi za kidini.
Sillo amesema kabla ya usajili wa kudumu kutolewa, taasisi na madhehebu ya dini huwekwa katika kipindi cha matazamio.
Amesema sababu nyingine zinazochochea ucheleweshaji wa usajili ni kushindwa kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Ofisi ya Msajili kwa wakati.
Naibu waziri amesema wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya inaendelea kushughulikia maombi ya usajili wa taasisi na madhehebu ya dini na kutoa usajili kwa wakati kwa taasisi zenye sifa stahiki.
Katika swali za nyongeza, Ng’enda amehoji kwa nini Serikali haitoi muda maalumu wa kushughulikia maombi ya taasisi za kidini badala yake kuacha hadi miaka mitano.
“Serikali inanufaika nini na taasisi ambazo zinafanya kazi zaidi ya miaka 20 zinahitaji usajili kurasimisha lakini inashindwa kufanya hivyo?” amehoji Ng’enda.
Naibu Waziri Sillo amesema wameweka miaka miwili hadi mitano kuhakikisha wanazichunguza vizuri kabla ya kupatiwa usajili na kwamba, hiyo inatokana na unyeti wa taasisi hizo.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha taasisi hizi zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, na hiyo ni kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi yetu,” amesema.
Amesema kwa taarifa ndani ya wizara kuna taasisi zisizozidi tano zilizokaa muda mrefu wa takribani miaka 20 bila kupata usajili wa kudumu.
Sillo amesema hilo linatokana na kuhamahama kwa ofisi na kusajiliwa kupitia taasisi nyingine.
Amesema jukumu kubwa la Serikali ni kuhakikisha taasisi hizo zinafuata Katiba na sheria.